The chat will start when you send the first message.
1Ikawa Dawidi na watu wake waliporudi Siklagi siku ya tatu, Waamaleki walikuwa wameishambulia ile nchi ya kusini, hata Siklagi, wakauteka mji wa Siklagi, wakauteketeza kwa moto.
2Wakawateka wanawake waliokuwamo, wadogo kwa wakubwa, lakini hawakuua mtu, wakawachukua tu, kisha wakaenda zao.
3Dawidi na watu wake walipofika mjini, wakauona mji kuwa umeteketezwa kwa moto, nao wake zao na watoto wao wa kiume na wa kike walikuwa wametekwa.
4Ndipo, Dawidi pamoja na watu waliokuwa naye walipopaza sauti, wakalia, mpaka wasipokuwa na nguvu tena za kulia.
5Nao wale wanawake wawili wa Dawidi walikuwa wametekwa, Ahinoamu wa Izireeli na Abigaili, mkewe Nabali wa Karmeli.[#1 Sam. 25:42-43.]
6Dawidi akasongeka sana, kwani wale watu walitaka kumpiga mawe, kwa kuwa wote pia walikuwa na uchungu rohoni, kila mmoja kwa ajili ya watoto wake wa kiume na wa kike. Ndipo, Dawidi alipojipatia nguvu kwa Bwana Mungu wake.
7Kisha akamwambia mtambikaji Abiatari, mwana wa Ahimeleki: Kilete kisibau cha mtambikaji! Abiatari alipomletea Dawidi hicho kisibau cha mtambikaji,[#1 Sam. 23:9.]
8Dawidi akamwuliza Bwana kwamba: Nikikimbia na kukifuata hicho kikosi nitakipata? Akamwambia: Piga mbio! Kwani utakipata kweli, uwaponye mateka.
9Ndipo, Dawidi alipokwenda yeye na wale watu 600 waliokuwa naye, wakafika mtoni kwa Besori; huko ndiko, walikokaa wao walioachwa nyuma.
10Lakini Dawidi na watu 400 wakaendelea kupiga mbio, waliokaa ni 200 tu, ndio wale waliochoka sana, wasiweze kuvuka mtoni kwa Besori.
11Kisha wakaona mtu wa Misri kule porini, wakamchukua na kumpeleka kwa Dawidi, wakampa chakula, naye akala, kisha wakampa hata maji ya kunywa.
12Walipompa nalo andazi la kuyu na maandazi mawili ya zabibu, roho yake ikamrudia, kwani alikuwa hakula chakula wala hakunywa maji siku tatu mchana kutwa na usiku kucha.[#Amu. 15:19.]
13Ndipo, Dawidi alipomwuliza: Wewe mtu wa nani? Unatoka wapi? Akasema: Mimi ni kijana wa Misri, mtumwa wa mtu wa Amaleki; bwana wangu akaniacha, kwa kuwa naliugua, leo ni siku ya tatu.
14Sisi twaliishambulia nchi ya kusini kwao Wakreti nako kwao Wayuda, tena nchi ya kusini kwao Wakalebu, nao mji wa Siklagi tukauteketeza kwa moto.[#Yos. 14:13; 2 Sam. 8:18.]
15Dawidi akamwuliza: Utatuongoza, tukipate hicho kikosi? Akasema: Niapie na kumtaja Mungu, ya kuwa hutaniua, wala hutanitoa na kunitia mkononi mwa bwana wangu! Kisha nitakuongoza, ukipate hicho kikosi.
16Kisha akawaongoza, wakawakuta; nao walikuwa wametawanyika katika nchi hiyo yote, wakawa wanakula, wanakunywa, maana walikula sikukuu kwa ajili ya hayo mateka yote yaliyokuwa makubwa, waliyoyateka katika nchi ya Wafilisti na katika nchi ya Yuda.
17Dawidi akawapiga kuanzia mapema hata jioni ya kesho yake, kwao asipone mtu, ila ni vijana 400 tu waliopanda ngamia na kukimbia upesi.
18Dawidi akawaponya wote, Waamaleki waliowachukua, nao wakeze wawili Dawidi akawaponya.
19Hakupotea kwao hata mmoja, wadogo kwa wakubwa, watoto wa kiume wala wa kike; nazo nyara zote pia, walizozichukua kupeleka kwao, basi, hizo zote pia Dawidi akazirudisha;
20Dawidi akachukua mbuzi na kondoo na ng'ombe wote, wakawachunga kwenda mbele ya kundi lile la kwao, wakasema: Hizi ndizo nyara za Dawidi.
21Dawidi alipofika kwenye wale watu 200 waliokuwa wamechoka sana, wasiweze kumfuata Dawidi, waliowaacha kule mtoni kwa Besori, wakatoka kumwendea Dawidi njiani nao wale watu waliokwenda naye. Dawidi alipowafikia karibu hao watu, akawaamkia na kuwauliza, kama hawajambo.
22Lakini miongoni mwao waliokwenda na Dawidi watu wote waliokuwa wabaya wasiofaa wakaanza kusema kwamba: Kwa kuwa hawakwenda nasi, wasigawiwe nyara, tulizozipokonya, ila wapewe tu kila mtu mkewe na wanawe, wawapeleke kwenda zao.
23lakini Dawidi akasema: Msifanye hivyo, ndugu zangu, kuyatumia hivyo, Bwana aliyotupa! Naye ametulinda, akakitia kile kikosi kilichotujia mikononi mwetu.
24Yuko nani atakayewaitikia katika jambo hili? Ila fungu lake aliyeshuka kupigana sharti liwe sawa na fungu lake yeye aliyekaa na kulinda mizigo, wote pamoja sharti wagawiwe sawasawa![#4 Mose 31:27.]
25Tangu siku hiyo hata baadaye yakawa vivyo hivyo; watu wakayaweka hayo kuwa maongozi na maamuzi kwao Waisiraeli hata siku hii ya leo.
26Dawidi alipofika Siklagi akatuma watu kuwapelekea wazee wa Yuda waliokuwa rafiki zake fungu moja la hizo nyara na kuwaambia: Tazameni! Hili ni gawio lenu la nyara zitokazo kwao wachukivu wake Bwana.
27Waliopewa ndio wa Beteli na wa Ramoti wa kusini na wa Yatiri
28na wa Aroeri na wa Sifumoti na wa Estemoa
29na wa Rakali, na wa miji ya Wayerameli na wa miji ya Wakeni
30na wa Horma na wa Kori-Asani na wa Ataki
31na wa Heburoni na wa mahali pote, Dawidi na watu wake walipotembeatembea.