2 Petero 2

2 Petero 2

Wafumbuaji wa uwongo.

1Lakini kulikuwako hata wafumbuaji wa uwongo kwao wa ukoo wetu; vivyo hivyo hata kwenu wafunzi wa uwongo watakuwako, wataleta mafundisho wa kuangamiza watu, wamkane naye Bwana aliyewakomboa; hivyo watajiletea wenyewe mwangamizo utakaowafikia upesi.[#Mat. 24:11; 1 Tim. 4:1.]

2Lakini wengi watayafuata mambo ya uasherati wao, ndio watakaoibezesha njia ya kweli.

3Kwa choyo chao watawachuuza nanyi na kuwaambia maneno ya udanganyi. Lakini kuhukumiwa kwao hakukawilii tangu kale, nao mwangamizo wao hausinzii.

4Kwani hata malaika waliokosa Mungu hakuwalimbika, ila aliwakumba kuzimuni, wakiwa wamefungwa na minyororo ya giza, akawatoa, walindwe, mpaka watakapohukumiwa.

5Nao ulimwengu wa kale hakuulimbika, ila alileta mafuriko ya maji, akayaeneza ulimwenguni kwao wasiomcha Mungu, akamponya Noa tu pamoja na wenzake saba, maana alikuwa mwenye kutangaza wongofu.[#2 Petr. 3:6; 1 Mose 8:18; 1 Petr. 3:20.]

6Nayo miji ya Sodomu na Gomora aliiteketeza kuwa majivu tu; alipoipatiliza hivyo aliiweka kuwa kielezo cha kuwatisha watakaoacha tena kumcha Mungu.[#1 Mose 19:25.]

7Lakini Loti aliyekuwa mwongofu alimwokoa, kwani aliumia sana kwa kuuona mwenendo wao wasioonyeka wakipenda mambo ya uasherati.

8Kwani huyo mwongofu alikaa katikati yao, nayo matendo mapotovu, aliyoyaona, nayo aliyoyasikia siku kwa siku, yaliuumiza moyo wake mwongofu.[#Ez. 9:4.]

9Bwana hujua kuwaokoa majaribuni wenye kumcha, lakini wapotovu huwaweka, wapatilizwe siku ya hukumu.[#1 Kor. 10:13; Ufu. 3:10.]

10Watakaopata makali kupita wengine ndio wale wanaofuata miili migeni kwa kuwa na tamaa chafu; nao ndio wenye kubeza ukuu pasipo kuogopa, hujivuna wenyewe tu, nako kuwatukana wenye utukufu hakuwatetemeshi.[#Yuda 8-10.]

11Lakini malaika wawapitao uwezo na nguvu hawapeleki masuto ya kuwatukana mbele ya Bwana.

12Lakini hao hufanana na nyama wasiojua kitu; hao hivyo, walivyoumbwa, huzaliwa, wakamatwe au waoze tu. Vivyo hivyo hata wale watapata kuoza kwa uovu wao, maana huvitukana, wasivyovijua;

13kisha watalipizwa mapotovu yao. Hushangilia malafi na malevi ya kila siku, huwa kama madoa yachukizayo wakijiingiza kwa udanganyi wao hapo, mnapogawiana vyakula, tena napo hapo hula vibaya.

14Wana macho yajaayo matongozi, yasiyokoma kukosa; huiponza mioyo ya watu wasioshupaa; mioyo yao huijua mizungu yote ya kuonea mali; maana ni wana wa apizo.

15Walipoiacha njia iliyonyoka walijipoteza, wakaishika njia ya Bileamu, mwana wa Beori, aliyependa malipo, yangawa mapotovu.[#4 Mose 22:7; Ufu. 2:14.]

16Lakini alikemewa alipokataa kuonyeka mwenyewe: punda asiyeweza kusema alisema kwa sauti ya kimtu, akamzuia yeye aliyekuwa mfumbuaji, asifanye lisilofanywa.[#4 Mose 22:28.]

17Hawa huwa kama visima visivyo na maji, tena kama mawingu yanayokimbizwa na ukali wa upepo; fungu lao, walilowekewa, ni lile giza jingi.

18Husema maneno makuu yasiyo na maana; hivyo, walivyozifuata tamaa za miili na kupitisha kiasi, huwaponza walioanza kuwakimbia wale wanaoendelea kujipoteza.

19Huwaagia uungwana, nao wenyewe wamo katika utumwa uuao; kwani mtu akitekwa huwa mtumwa wake yeye aliyemteka.[#Yoh. 8:34,36.]

20Kwani hapo walipomtambua Bwana na mwokozi Yesu Kristo waliyakimbia machafu ya ulimwengu; lakini sasa walipoingia penye matanzi tena wakatekwa, mambo yao ya mwisho yakawa mabaya kuliko ya kwanza.[#Mat. 12:45.]

21Kwani kama wasingaliitambua njia ya wongofu, ingaliwafalia, kuliko kuitambua, kisha kuliacha tena agizo takatifu, walilopewa.[#Luk. 12:47-48.]

22Ilikuwa kwao, kama fumbo la kweli linavyosema:

Mbwa huyarudia matapiko yake,

naye nguruwe aliyekoga hugaagaa tena matopeni.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania