Amosi 3

Amosi 3

Mapatilizo yatakayowajia Waisiraeli bado kidogo.

1Lisikieni neno hili, Bwana alilolisema

kwa ajili yenu, ninyi wana wa Isiraeli,

kwa ajili ya huu ukoo wote,

nilioutoa katika nchi ya Misri na kuuleta huku:

Amesema:

2Niliwajua ninyi tu katika koo zote zilizoko nchini,

kwa hiyo nitawapatilizia ninyi manza zote, mlizozikora.

3Je? Wako wawili wanaosafiri pamoja,

isipokuwa wamepatana?

4Je? Simba ananguruma mwituni, asipokuwa amepata windo?

Je? Mwana wa simba analia pangoni mwake, asipokuwa amekamata?

5Au ndege anawezaje kuanguka tanzini chini, isipokuwa mtu amelitega?

Au tanzi linafyatuka na kuruka juu, lisipokuwa limekamata?

6Au baragumu la vita likipigwa mjini,

watu waliomo mjini hawashikwi na woga?

Au yako mabaya mjini, Bwana asiyoyafanya?

7Kweli Bwana Mungu hafanyi neno,

asipokuwa amewafunulia njama yake watumishi wake wafumbuaji.

8Simba akinguruma, yuko nani asiyeogopa?

Bwana Mungu akisema neno, yuko nani asiyetaka kulifumbua?

9Yatangazeni majumbani mwa Adodi!

Namo majumbani mwa nchi ya Misri!

Semeni: Kusanyikeni milimani kwa Samaria!

Itazameni mivurugo, jinsi inavyozidi katikati yao!

Yatazameni nayo makorofi yaliyoko huko kwao!

10Ndivyo, asemavyo Bwana:

Hawakujua kufanya yaliyo sawa

wao waliolimbika majumbani mwao makorofi na mapokonyo.

11Kweli hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema:

Yuko atakayeisonga nchi hii po pote

na kuvibwaga chini vilivyokuwa nguvu zako,

majumba yako yapate kutekwa.

12Hivi ndivyo, Bwana anavyosema:

Kama mchungaji anavyoopoa kinywani mwa simba

mifupa miwili ya mguu au kipande cha sikio,

ndivyo, watakavyojiponya wana wa Isiraeli wakaao sasa Samaria

pembeni kitandani juu ya mito ya hariri ya malalo.

13Yasikieni, myashuhudie nyumbani mwa Yakobo!

ndivyo, asemavyo Bwana Mungu aliye Mungu Mwenye vikosi.

14Kwani siku hiyo, nitakayowapatilizia Waisiraeli mapotovu yao,

ndipo, nitakapowapatilizia napo pa kutambikia Beteli,

pembe za hiyo meza ya kutambikia zivunjwe, zianguke chini.

15Ndipo, nitakapozibomoa nyumba za kupupwe pamoja nazo za kiangazi,

navyo vyumba vilivyopambwa na pembe za tembo vitaangamia,

hizo nyumba nyingi zitakapotoweka;

ndivyo, asemavyo Bwana.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania