Esteri 1

Esteri 1

Wasti, mkewe mfalme wa Persia, anafukuzwa na mfalme.

1Ahaswerosi alikuwa akitawala majimbo 127 kutoka nchi ya Uhindi mpaka nchi ya Nubi. Ikawa katika siku zake Ahaswerosi

2hapo, yeye mfalme Ahaswerosi alipokaa katika kiti chake cha kifalme jumbani mwake huko Susani,

3katika mwaka wa tatu wa ufalme wake ndipo, alipowafanyia wakuu wake wote pamoja na watumishi wake karamu kubwa. Wakawako mbele yake wakuu wa vikosi vya Persia nao vya Media, hata wenye macheo na wakuu wa majimbo.

4Akawaonyesha mali na malimbiko ya ufalme wake nayo marembo na utukufu wake mwingi siku nyingi, yaani siku 180.

5Siku hizo zilipokwisha kupita, mfalme akawafanyia watu wote pia waliopatikana mle Susani penye jumba lake, wakubwa kwa wadogo, karamu ya siku saba uani penye bustani ya jumba la mfalme.

6Mazulia meupe na meusi mazuri mno yalikuwa yamefungwa kwa kamba za pamba nyeupe na nyekundu katika pete za fedha penye nguzo za mawe meupe. Nayo magodoro ya kukalia yaliyofumwa kwa nyuzi za dhahabu na za fedha yalikuwa yametandikwa sakafuni palipotengenezwa kwa mawe mekundu na meupe na ya manjano na meusi.

7Vyombo, watu walivyovipata vya kunywea, vilikuwa vya dhahabu; hivyo vyombo navyo vilipitanapitana kwa namna zao, nazo mvinyo za kifalme zilikuwa nyingi, kama inavyoupasa utu wa mfalme.

8Kama ilivyoagizwa, watu wakanywa, kama walivyotaka pasipo kushurutishwa; kwani nidvyo, mfalme alivyowaagiza wakuu wote wa nyumbani mwake, waache, kila mtu anywe, kama anavyopendezwa.

9Naye Wasti, mkewe mfalme, alifanya karamu ya wanawake mle ndani ya jumba la kifalme la mfalme Ahaswerosi.

10Siku ya saba, moyo wa mfalme ulipochangamshwa na mvinyo, akawaambia akina Mehumani, Bizita, Harbona, Bigita, Abagita, zetari, na Karkasi, watumishi wake saba wa nyumbani waliomtumikia mfalme Ahaswerosi mwenyewe,

11wamlete Wasti mkewe mfalme, amtokee mfalme na kuvaa kilemba cha kifalme, awaonyeshe watu wote nao wakuu uzuri wake, kwani alikuwa kweli mwenye sura nzuri.

12Lakini Wasti, mkewe mfalme, akakataa kuja kwa ile amri, mfalme aliyompelekea kwa vinywa vya wale watumishi wa nyumbani. Ndipo, mfalme alipokasirika sana, makali yake yakawaka moto moyoni mwake.

13Basi, mfalme akafanya shauri na mafundi wa kuvijua vielekezo vya siku, kwani ilikuwa desturi yake mfalme kuulizana nao wote waliozijua amri na hukumu za serikali.[#1 Mambo 12:32.]

14Waliomfuata kwa ukuu walikuwa Karsina, Setari, Adimata, Tarsisi, Meresi, Marsina na Memukani, ndio wakuu saba wa Persia na wa Media waliotokea usoni pa mfalme, nao walikuwa wa kwanza katika ufalme huo.

15Akawauliza: Ndio nini inayopasa kwa amri za serikali kumfanyizia wasti, mkewe mfalme, kwa kuwa hakuifanya amri ya mfalme Ahaswerosi, aliyompelekea kwa vinywa vya wale watumishi wa nyumbani?

16Memukani akasema mbele ya mfalme na mbele ya hao wakuu: Siye mfalme peke yake, Wasti, mkewe mfalme, aliyemkosea, ila amewakosea nao wakuu wote na watu wote pia walioko katika majimbo ya mfalme Ahaswerosi.

17Kwani jambo hili la mkewe mfalme litatoka, lifike kwa wanawake wote, liwabeue bwana zao machoni pao, maana watasema: Mfalme Ahaswerosi aliagiza kumleta Wasti, mkewe mfalme, aje usoni pake, naye hakuja.

18Leo hivi wake wakuu wa Wapersia na wa Wamedia waliolisikia hilo jambo la mkewe mfalme watalisimulia wakuu wote wa mfalme; ndipo, yatakapokuwa mabezo na mateto ya kutosha.

19Mfalme akiyaona kuwa mema, na kutoke kwake amri ya kifalme, iandikwe katika amri za Wapersia na za Wamedia, isitanguke tena, kwamba: Wasti asitokee tena usoni pa mfalme Ahaswerosi, nao utukufu wake wa kifalme mfalme na ampe mwenzake aliye mwema kuliko yey.[#Dan. 6:8.]

20Mbiu hiyo, mfalme atakayoitoa, itakapotangazwa katika ufalme wake wote ulio mkubwa, ndipo, wanawake wote watakapowapa bwana zao macheo, wakubwa kwa wadogo.

21Neno hili mfalme na wakuu wakaliona kuwa jema, mfalme akafanya, kama Memukani alivyosema.

22Akatuma barua katika majimbo yote ya mfalme, kwa kila jimbo katika maandiko yao na kwa kila kabila katika msemo wa kwao kwamba: Kila mume sharti awe mkuu nyumbani mwake, akate mashauri, kama yanavyosemwa kwao.[#Est. 3:12; 8:9; 1 Mose 3:16.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania