The chat will start when you send the first message.
1Baada ya mambo hayo mfalme Ahaswerosi akampa Hamani, mwana wa Hamedata wa Agagi, kuwa mkuu akimwinua na kukiweka kiti cha ukuu wake juu zaidi kuliko vyao wakuu wote waliokuwa naye.
2Kwa hiyo watumishi wote wa mfalme waliokuwako kule langoni kwa mfalme wakampigia Hamani magoti na kumwangukia, kwani hivyo ndivyo, mfalme alivyoagiza kwa ajili yake. Lakini Mordekai hakumpigia magoti, wala hakumwangukia.
3Watumishi wa mfalme waliokuwako langoni kule kwa mfalme wakamwuliza Mordekai: Mbona unaikosea amri ya mfalme?
4Ikawa, walipomwambia haya siku kwa siku, asiwasikie, basi, wakamsimulia Hamani, waone, kama maneno ya Mordekai yataweza kusimama, kwani aliwaambia, ya kuwa yeye ni Myuda.
5Hamani alipoona, ya kuwa Mordekai hampigii magoti, wala hamwangukii, ndipo, makali yenye moto yalipomjaa Hamani moyoni.
6Lakini akaona, ya kama haimpasi kumkamata Mordekai peke yake, kwani walimwambia nao ukoo wake Mordekai; kwa hiyo Hamani akatafuta njia ya kuwaangamiza Wayuda wote pia waliokuwa katika ufalme wote wa Ahaswerosi, kwa kuwa ukoo wake Mordekai.
7Katika mwezi wa kwanza, ndio Nisani, katika mwaka wa kumi na mbili wa mfalme Ahaswerosi wakapiga Puri, ndio kura, machoni pake Hamani siku kwa siku, hata mwezi kwa mwezi mpaka mwezi wa kumi na mbili, ndio Adari.[#Est. 9:24.]
8Kisha Hamani akamwambia mfalme Ahaswerosi: Liko kabila moja lililotawanyika katikati ya makabila mengine katika majimbo yote ya ufalme wako, nao wanakaa na kujitenga kabisa, nayo maongozi yao ni mengine kabisa, siyo ya makabila yote mengine, nayo maagizo ya mfalme hawayafanyi. Kwa hiyo haimpasi mfalme kuwaacha, wajikalie tu.
9Ikiwa, mfalme avione kuwa vema, na viandikwe kwamba: Watu na wawaangamize! Kisha mimi nitawapimia wenye kazi hiyo mikononi mwao mizigo ya fedha elfu kumi, waipeleke na kuitia katika malimbiko ya mfalme.
10Ndipo, mfalme alipoitoa pete yake yenye muhuri kidoleni pake, akampa Hamani, mwana wa Hamedata wa Agagi, aliyekuwa mpingani wao Wayuda.[#Est. 8:2.]
11Mfalme akamwambia Hamani: Zile fedha umepewa kukaa nazo, nao watu wa ule ukoo uwafanyizie yaliyo mema machoni pako.
12Kisha waandishi wa mfalme wakaitwa katika mwezi wa kwanza siku ya kumi na tatu; yote, Hamani aliyoyaagiza, yakaandikwa baruani kwa watawala nchi wa mfalme na kwa wenye amri wa kila jimbo moja na kwa wakuu wa kila kabila moja, kwa kila jimbo katika maandiko yao na kwa kila kabila katika msemo wa kwao. Hizo barua zikaandikwa katika jina la mfalme Ahaswerosi, zikatiwa muhuri kwa ile pete ya mfalme yenye muhuri,[#Est. 1:22.]
13kisha zikapewa wapiga mbio, wazipeleke katika majimbo yote ya mfalme kwamba: Siku hiyo moja ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari, Wayuda wote pia, vijana na wazee, wachanga na wanawake, watoweshwe kwa kuuawa na kwa kuangamizwa, nazo mali zao zitekwe.
14Mwandiko wa pili wa hizo barua ukatangazwa katika kila jimbo moja kuwa amri iliyotolewa na mfalme, watu wote pia wakaelezwa vema, wapate kuwa tayari siku hiyo.
15Wapiga mbio wakatoka upesi kwa lile neno la mfalme. Namo mjini mwa Susani, mlimokuwa na jumba la mfalme, ile amri ya mfalme ikatangazwa. Kisha mfalme na Hamani wakakaa, wanywe, lakini mji wa Susani ukawa umevurugika.