Esteri 5

Esteri 5

Esteri anakwenda kwa mfalme.

1Ikawa siku ya tatu, Esteri akavaa mavazi ya kifalme, akaja kusimama katika ua wa ndani wa nyumba ya mfalme. Naye mfalme alikuwa amekaa katika kiti chake cha kifalme nyumbani mwake mwa kifalme, akajielekeza kuutazama mlango wa hiyo nyumba.

2Ikawa, mfalme alipomwona Esteri, mkewe mfalme, akisimama uani, akaona upendeleo mbele yake, mfalme akampungia Esteri kwa bakora yake ya dhahabu iliyokuwa mkononi mwake. Ndipo, Esteri alipokuja kuugusa upembe wa hiyo bakora.[#Est. 4:11; 8:4.]

3Mfalme akamwuliza: Una shauri gani, Esteri, mkewe mfalme? Unataka nini? Ingawa ni nusu ya ufalme, utapewa.

4Esteri akamjibu: Kama ni vizuri kwake mfalme, mfalme na aje leo pamoja na Hamani kula karamu, Esteri aliyomfanyizia.[#Est. 1:19.]

5Mfalme akaagiza: Mwiteni Hamani, aje upesi, yafanyike Esteri aliyoyasema!

Mfalme na Hamani wakaja kula karamu, Esteri aliyoifanya.

6Walipokunywa mvinyo, mfalme akamwuliza Esteri tena: Unataka nini? Utapewa. Unataka nini? Ingawa ni nusu ya ufalme, itafanyika.[#Est. 9:12.]

7Esteri akajibu akisema: Ninayoyaomba kwa kuyataka ni haya:

8kama nimeona upendeleo mbele ya mfalme, kama ni vizuri kwake mfalme kunipa ninayoyaomba na kuyafanya, mfalme na aje tena pamoja na Hamani kula karamu, nitakayowafanyizia kesho; ndipo, nitakapofanya, kama mfalme alivyosema.

Hamani anataka kumwua Mordekai.

9Hamani akatoka mwake siku hiyo kwa kufurahi na kuchangamka moyoni. Lakini Hamani alipomwona Mordekai langoni kwa mfalme, asiinuke, wala asimwondokee, ndipo, makali yenye moto yalipomjaa Hamani moyoni kwa ajili ya Mordekai,

10lakini Hamani akajizuia. Alipofika nyumbani mwake, akatuma watu kuwaita wapenzi wake na mkewe Zeresi.

11Hamani akawasimulia, jinsi utukufu wa mali zake ulivyo mkubwa, tena jinsi wanawe walivyo wengi, nayo macheo yote, mfalme aliyompa akimweka kuwa mkuu kuliko wakuu na watumishi wa mfalme.

12Kisha Hamani akasema: Naye Esteri, mkewe mfalme, hakualika mwingine, aje na mfalme kula karamu, aliyoifanya, ila mimi peke yangu. Hata kesho mimi nimealikwa naye kuja na mfalme.

13Lakini haya yote hayanitoshei, nikimwona yule Myuda Mordekai, akikaa siku zote langoni kwa mfalme.

14Ndipo, mkewe Zeresi na wapenzi wake wote walipomwambia: Na wasimike mti mrefu wa mikono hamsini! Kisha umwambie mfalme kesho, wamtundike Mordekai, upate kwenda pamoja na mfalme karamuni na kufurahi! Shauri hili likampendeza Hamani, akausimika ule mti.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania