The chat will start when you send the first message.
1Neno la Bwana likanijia la kwamba:[#Yes. 6:9-10.]
2Mwana wa mtu unakaa katikati ya mlango mkatavu, wako na macho yaonayo, lakini hawaoni, wako na masikio yasikiayo, lakini hawasikii, kwani hawa ndio mlango mkatavu.
3Basi, wewe mwana wa mtu, jifanyizie vyombo vya kuhama navyo! Kisha hama mchana machoni pao, ukuhama mahali pako na kuhamia pengine machoni pao, labda wataona, ya kuwa ndio mlango mkatavu.
4Navyo vyombo vyako utavitoa nyumbani mchana machoni pao, kama ni vyombo vya kuhama navyo, nawe utatoka nyumbani jioni machoni pao, kama watu wanavyotoka mwao wakitaka kuhama.
5Machoni pao bomoa bomani kwa mji, pawe tundu, ndipo uvitolee vyombo vyako!
6Machoni pao uviweke begani, uvitoe, giza ikiwa kuu! Nao uso wako uufunike, usiione nchi! Kwani nimekuweka kuwa kielekezo cha mlango wa Isiraeli.[#Ez. 24:24,27.]
7Nikafanya hivyo, nilivyoagizwa: vyombo vyangu nikavitoa mchana, kama ni vyombo vya kuhama navyo, kisha nikajibomolea kwa mikono tundu bomani kwa mji, nikavitoa, giza ilipokuwa kuu, nikiviweka begani machoni pao.
8Asubuhi neno la Bwana likanijia la kwamba:
9Mwana wa mtu, wao wa mlango wa Isiraeli walio mlango mkatavu hawakukuuliza: Wewe unafanya nini?
10Waambie: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Tamko hili zito ni la mkuu wa Yerusalemu, tena la mlango wote wa Isiraeli uliomo humu mjini.
11Sema: Mimi ni kielekezo chenu; kama mimi nilivyofanya, ndivyo, nao watakavyofanyiziwa, watahamishwa kwenda kifungoni.[#Ez. 12:6.]
12Naye mkuu aliomo mwao mjini atavichukua vyombo vyake begani, giza ikiwa kuu, akitoka katika tundu la bomani kwa mji, walilombomolea, wapate kumtoa hapohapo; uso wake utaufunika, kusudi asiione nchi kwa macho yake.[#Yer. 39:7.]
13Nami nitamtegea wavu wangu, anaswe katika tanzi langu; kisha nitampeleka Babeli katika nchi ya Wakasidi, lakini hataiona; nako ndiko, atakakokufa.[#Ez. 17:20; 32:3-6.]
14Nao wote wamzungukao kuwa wasaidiaji wake nao wa vikosi vyake vyote nitawatupatupa pande zote za upepo, nazo panga nitazichomoa, ziwafuate nyuma.
15Ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana, nitakapowatupatupa kwenye wamizimu na kuwatawanya katika nchi hizo.
16Lakini nitasaza kwao wachache wanaohesabika, wasiuawe na panga, wala na njaa, wala na magonjwa mabaya, wapate kuyasimulia machukizo yao yote kwenye wamizimu, watakakopelekwa, nao wajue, ya kuwa mimi ni Bwana.[#Ez. 6:8.]
17Neno la Bwana likanijia la kwamba:
18Mwana wa mtu, sharti ukile chakula chako kwa kutetemeka! Nayo maji yako sharti uyanywe kwa kustuka na kwa kuyahangaikia.
19Kisha waambie watu wa nchi hii: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyowaambia wakaao Yerusalemu katika nchi ya Isiraeli: Vyakula vyenu mtavila na kuvihangaikia, nayo maji yenu mtayanywa kwa kupigwa na bumbuazi, kwani nchi yao itaangamia, yote yaliyojaa mle yakipotea kwa ajili ya ukorofi wao wote waliokaa huko.
20Nayo miji inayokaa watu itabomolewa, nchi hii iwe peke yake tu; ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana.
21Neno la Bwana likanijia la kwamba:
22Mwana wa mtu, ni fumbo gani hili lililoko kwenu katika nchi ya Isiraeli la kusema: Siku hukawia, nayo maono yote hupotea?[#2 Petr. 3:4.]
23Kwa hiyo waambie: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Nitalikomesha fumbo hilo, wasilitumie tena kwao Waisiraeli; kwa hiyo waambie: Siku hizo ziko karibu kweli, maono yote yatimie.[#Hab. 2:3.]
24Kwani hakuna tena ono lo lote litakalokuwa la bure, wala ufumbuaji wa kupendeza watu tu kwao wa mlango wa Isiraeli.
25Kwani mimi Bwana nitasema, nayo nitakayoyasema yatafanyizwa pasipo kukawia kabisa, kwani katika hizi siku zenu, mngalipo bado, ninyi mlio mlango mkatavu, nitasema neno, kisha nitalifanya! Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.
26Neno la Bwana likanijia la kwamba:
27Mwana wa mtu, tazama, wao wa mlango wa Isiraeli husema: Ono, analoliona yeye, ni la siku nyingi, nayo maneno, anayoyasema yeye, wakati wao wa kutimia uko mbali.
28Kwa hiyo waambie: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Maneno yangu yote yahatakawia tena; neno, nitakalolisema, litafanyizwa; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.