Ezekieli 6

Ezekieli 6

Jinsi nchi ya Isiraeli itakavyoangamizwa.

1Neno la Bwana likanijia la kwamba:[#Ez. 36:1; Mika 6:1.]

2Mwana wa mtu, ielekezee milima ya Isiraeli uso wako, uifumbulie yatakayokuwa!

3Useme: Milima ya Isiraeli, lisikieni neno la Bwana Mungu! Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema, mvisikie ninyi milima na vilima na vijito na mabonde: Mtaniona, nikileta panga kwenu, niyakomeshe matambiko yenu ya vilimani.

4Ndipo, penu pa kutambikia patakapokuwa peke yao, navyo vinyago vyenu vya jua vitavunjwa, nao wenzenu watakaopigwa na panga nitawatupa mbele ya magogo, mnayoyatambikia.[#3 Mose 26:30.]

5Kweli mizoga ya wana wa Isiraeli nitaikusanya mbele ya magogo, waliyoyatambikia, nayo mifupa yenu nitaitupatupa pande zote palipo penu pa kutambikia.

6Pote mnapokaa miji yenu itabomoliewa, navyo vilima, mlikotambikia, vitakuwa peke yao, kusudi penu pa kutambikia pabomolewe, pawe peke yao, nayo magogo, mliyoyatambikia, yavunjwe na kukomeshwa, hata vinyago vyenu vya jua vikatwekatwe, kazi zenu zifutwe.

7Nao watakaouawa wataanguka katikati yenu; ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana.

8Lakini wako wa kwenu, nitakaowasaza, wakipona panga, wakae kwa wamizimu katika zile nchi, mtakakotupwatupwa.[#Yes. 6:13.]

9Hao wenzenu watakaopona watanikumbuka huko kwa wamizimu, watakakohamishwa kwa kutekwa, kwani nitaivunja mioyo yao yenye ugoni iliyoondoka kwangu, hata macho yao nitayavunja yaliyoyatazama na kuyatamani magogo yao ya kutambikia. Ndiko, watakakojichukia machoni pao wenyewe kwa ajili ya mabaya, waliyoyafanya na kuyatumia yale matapisho yao yote.[#5 Mose 30:2.]

10Ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana, sikusema bure, ya kuwa nitawafanyizia hayo mabaya.

11Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Yapige makofi yako na kupiga shindo kwa miguu yako! Kaulilie mlango wa Isiraeli kwa ajili ya matapisho mabaya yote, kwa kuwa watauawa kwa panga na kwa njaa na kwa magonjwa mabaya.

12Alioko mbali atakufa kwa ugonjwa mbaya, alioko karibu atakufa kwa upanga, aliyesalia kwa kufungiwa mjini atakufa kwa njaa. Hivyo nitawatimilizia makali yangu yenye moto.

13Ndipo, mtakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana, mizoga yao waliouawa itakapochanganyika na magogo, waliyoyatambikia po pote pa kutambikia pao: pote vilimani juu nako vileleni juu kwenye milima mikubwa yote, hata chini ya miti yote yenye majani mengi na chini ya mivule yote iliyo minene, walipoyavukizia magogo yao yote manukato ya kupendeza.[#1 Fal. 14:23.]

14Nitawakunjulia mkono wangu, nchi hii niigeuze kuwa mapori yaliyo peke yao kuanzia kwenye nyika kufikisha kwenye Dibula po pote, wanapokaa; ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana.[#Ez. 6:7.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania