Waebureo 4

Waebureo 4

Kiko kituo cha watu wa Mungu.

1Kwa kuwa kile kiagio cha kuingia kwenye kituo chake kiko bado, na tuogope, pasionekane hata mmoja wenu ajiwaziaye kwamba: Nimekikosa!

2Kwani nasi tumepigiwa hiyo mbiu njema kama wale. Lakini wale lile neno, waliloambiwa, halikuwafalia, kwani hawakulitegemea, wajiunge nao walisikiao.

3Maana sisi tumtegemeao Mungu twaingia kwenye kituo kile, kama alivyosema:

Kwa hiyo nilijiapia kwa makali yangu kwamba:

Hawataingia kamwe kwenye kituo changu!

Nazo kazi zake zilikuwa zimekwisha kufanyika hapo, alipokwisha kuumba ulimwengu,

4kwani pako mahali, alipoisema maana ya siku ya saba kwamba:

Siku ya saba Mungu alizipumzikia kazi zake zote.

5Napo pale alisema:

Hawataingia kamwe kwenye kituo changu!

6Hivyo vinajulika: wako bado watakaokiingia; lakini wale walioanza kupigiwa mbiu yake njema hawakukiingia, kwani walikataa kutii.

7Miaka ilipokwisha kupita mingi mno, akaweka tena siku, ni hii ya leo, alipomwambia Dawidi, kama alivyosema kale:

Leo, mtakapoisikia sauti yake,

msiishupaze mioyo yenu!

8Kwani kama Yosua angalikuwa amewapeleka kwenye kituo, asingalisema siku nyingine iliyoko nyuma bado.[#5 Mose 31:7; Yos. 22:4.]

9*Kwa hiyo twasema: Liko pumziko, watu wa Mungu walilowekewa bado.

10Kwani aliyeingia kwenye kituo chake, huyo kuzipumzikia kazi zake yeye, kama Mungu alivyozipumzikia kazi zake mwenyewe.[#Ufu. 14:13.]

Nguvu na makali ya Neno la Mungu.

11Sasa tujihimize kuingia kwenye kituo kile, pasipatikane mtu atakayeangushwa akiyafuata mafunzo yao walewale waliokataa kutii![#Ebr. 3:16-19.]

12Kwani neno la Mungu ni lenye uzima na nguvu, tena ni lenye makali kupita ya upanga wenye makali pande mbili. Nalo hupenya, mpaka litenge moyo na roho, nacho kiini na mifupa. Nalo huyaumbua mapenzi na mawazo yaliyomo moyoni.[#Yer. 23:29.]

13Hakuna kiumbe kiwezacho kujitowesha mbele yake yeye, ila vyote viko uchi na waziwazi machoni pake yeye, naye ndiye, ambaye tunatangaza Neno lake.*

Mtambikaji wetu mkuu.

14Tunaye mtambikaji mkuu kupita wengine aliyepaa mbinguni, ndiye Yesu, Mwana wake Mungu; kwa hiyo na tuyashike, tunayoyaungama![#Ebr. 3:1; 6:20; 7:26; 8:1; 9:11; 2 Kor. 12:2.]

15*Kwani hatuna mtambikaji mkuu asiyeteseka pamoja na sisi kwa ajili ya manyonge yetu. Maana naye alijaribiwa katika mambo yote kama sisi, lakini hakukosa.[#Ebr. 2:17; Luk. 4:13; Yoh. 8:46.]

16Kwa hiyo twende, tufike pasipo woga penye kiti chake cha kifalme, tutakapogawiwa huruma na upole, tumwone yeye atakayetusaidia hapo, tutakapomtakia!*[#Rom. 3:25; 1 Yoh. 3:21.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania