Hosea 4

Hosea 4

Waisiraeli wanaonywa kwa kukosa kwao.

1lisikieni neno la Bwana, ninyi wana wa Isiraeli!

Kwani Bwana yuko na neno la kuwagombeza wakaao katika nchi hii,

kwa kuwa hakuna welekevu wala huruma,

wala ujuzi wa Mungu katika nchi hii.

2Huapiza, huongopa, huua, huiba,

huvunja unyumba, hukorofisha;

ndivyo, damu zinavyoshikamana na damu nyingine.

3Kwa hiyo nchi hii inasikitika,

wakafifia wote wakaao humo,

nyama wa porini na ndege wa angani,

nao samaki wa baharini wanatoweka.

4Lakini hawataki, mtu awagombeze, wala mtu awaonye,

walio ukoo wako hufanana nao, wanaowagombeza watambikaji.

5Kwa hiyo utajikwaa mchana,

naye mfumbuaji atajikwaa pamoja na wewe usiku,

nami nitamwangamiza mama yako.

6Walio ukoo wangu wanaangamia kwa kukosa ujuzi,

kwa kuwa wewe umeukataa ujuzi, nami nakukataa, usinitambikie tena;

kwa kuwa umeyasahau Maonyo ya Mungu wako, nami nitawasahau wanao.

7Hivyo, walivyoendelea kuwa wengi, ndivyo, walivyoendelea kunikosea,

kwa sababu hii nitaugeuza utukufu wao kuwa mambo yatiayo soni.

8Hujilisha makosa yao walio ukoo wangu,

namo rohoni mwao hutamani kukora manza kama wao.

9Kwa hiyo watu na watambikaji watapatwa na mambo yaleyale,

nitawapatilizia njia zao, nayo matendo yao nitawarudishia.

10Watakapokula, hawatashiba; watakapofanya ugoni hawatapata wana,

kwa kuwa wameacha kushikana na Bwana.

11Ugoni na mvinyo na pombe huichukua mioyo yao.

12Walio ukoo wangu huzipiga mbao zao,

nazo fimbofimbo zao huziagulia,

kwani roho ya ugoni imewapoteza,

wakafanya ugoni papo hapo walipomwacha Mungu wao.

13Hutambika milimani juu, kwenye vilima huvukiza

kuliko na mvule au mgude au mkwaju, kwani kivuli chake ni chema.

Kwa hiyo wana wenu wa kike huzini,

nao wachumba wenu huvunja unyumba.

14Sitawapatiliza wana wenu wa kike, ya kuwa huzini,

wala wachumba wenu, ya kuwa huvunja unyumba;

kwani wenyewe hujitenga, wawe nao wanawake wagoni,

hutambika pamoja na wanawali watakatifu wa kimizimu;

ndivyo, watu wasiotambua maana wanavyoponzwa.

Wayuda wanaonywa, wasijitie katika makosa hayo.

15Wewe Isiraeli, ukiwa unafanya ugoni, usimkoseshe Yuda! Msije Gilgali! Wala msipande kwenda Beti-Aweni! Wala msiape na kusema: Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima![#Hos. 9:15; 10:5; Amo. 5:5.]

16Ikiwa Isiraeli ameshupaa vibaya kama ndama wenye ushupavu, je? Bwana atamchunga kama kondoo penye lisho pana?

17Efuraimu ni mpenda vinyago, mwache tu!

18Wakiisha kulewa hufuata ugoni, nao watu wake walio washika ngao hupenda sana mambo yenye soni.

19Upepo utawakamata kwa ajili ya matambiko yao.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania