Hosea 7

Hosea 7

Kuwalilia Waisiraeli.

1Ninapotaka kumponya Isiraeli,

ndipo, panapotokea wazi manza za Efuraimu na mabaya ya Samaria,

kwani hutenda ya uwongo, nao wezi hujipenyeza nyumbani,

nako nje huenea wanyang'anyi.

2Hawasemi mioyoni mwao, ya kama nayakumbuka mabaya yao yote;

sasa matendo yao yanawazunguka, yako wazi usoni pangu.

3Kwa mabaya yao huwafurahisha wafalme wao,

nao wakuu wao kwa kuongopa kwao.

4Wao wote ni wazinzi,

hufanana na jiko lililowashwa moto na mchoma mikate,

naye akiisha kukanda unga, hupumzika kwa kuchochea moto,

hata unga uwe umechachuka.

5Wakisema: Leo ni sikukuu ya mfalme wetu,

ndipo, wakuu wanapojiwasha kwa ukali wa mvinyo;

naye mwenyewe hushikana mikono na wafyozaji.

6Kwa hivyo, wanavyomvizia, humkaribishia mioyo yao,

ikiwa yenye moto ulio kama wa jiko la mikate:

mchocheaji akiwa amelala usiku kucha,

asubuhi huwaka kama moto wenye miali.

7Hivyo wao wote hupata moto ulio kama wa jiko la mikate,

wakawala waamuzi wao, wafalme wao wote wakaangushwa nao,

lakini kwao hao hakuonekana aliyenililia mimi.

Mapatilizo yatakayokuja.

8Efuraimu hujichanganya na mataifa mengine,

Efuraimu huwa kama andazi lisilogeuzwa.

9Wageni wamezila nguvu zake, mwenyewe asipovijua;

mvi zimemtoka mojamoja, lakini mwenyewe havijui.

10Majivuno yao Waisiraeli yanawasuta machoni pao,

lakini hawarudi kwake Bwana Mungu wao,

wala hawamtafuti katika mambo hayo yote.

11Efuraimu huwa kama hua pumbavu, asiye na akili:

mara anamwita Mmisri, mara anakwenda Asuri.

12Kila mara walipokwenda, niliwatandia wavu wangu,

niwanase kama ndege wa angani,

kisha nikawapatiliza, kama mkutano wao ulivyoambiwa.

13Yatawapata, kwa kuwa wamenikimbia!

Maangamizo yatawapata, kwa kuwa wamenikosea!

Nami nilipotaka kuwakomboa, wao waliniambia ya uwongo tu,

14hawakunilalamikia kwa mioyo yao, walipolia vitandani

kwao.

Ni ngano na pombe tu, wanazozikusanyikia,

lakini kwangu mimi wameondoka.

15Tena ni mimi niliyewafunza kuitumia mikono, nikaitia

nguvu,

lakini huniwazia mabaya tu.

16Wanaporudi, hawaji kwangu nilioko huku juu,

hufanana na upindi uliolegea.

Wakuu wao wataangushwa na panga kwa ajili ya ukali wa

ndimi zao;

kwa hiyo watafyozwa katika nchi ya Misri.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania