The chat will start when you send the first message.
1Mimi Yakobo niliye mtumwa wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo nawasalimu ninyi mlio mashina kumi na mawili yaliyotawanyika.[#1 Petr. 1:1.]
2Ndugu zangu, mnapotumbukia katika majaribu yaliyo mengi na mengi yawazieni kuwa machangamko tu![#Rom. 5:3-5.]
3Yatambueni: Kumtegemea Mungu kukijulishwa hivyo kuwa kwa kweli huwaletea uvumilivu.
4Nao uvumilivu sharti uitimize kazi yake, ninyi mpate kutimilika, mwe Wakristo wazima wasioachwa nyuma katika jambo lo lote.
5Lakini kama kwenu yuko akosaye werevu wa kweli, na amwombe Mungu anayependezwa kuwapa watu wote pasipo mawazo ya kinyuma; ndipo, atakapopewa.[#Yak. 3:17; Fano. 2:3-6.]
6Lakini sharti aombe kwa kumtegemea, asiwe na mambo mawili moyoni! Kwani mwenye mambo mawili hufanana na wimbi la bahari linalorushwarushwa na upepo na kutupwatupwa.[#Mar. 11:24.]
7Mtu aliye hivyo asidhani, ya kuwa kiko, atakachokipata kwake Bwana!
8Mtu mwenye mioyo miwili hugeukageuka katika njia zake zote.
9Lakini ndugu mnyenyekevu na ajivunie ukuu wake,[#Yak. 2:5.]
10naye mwenye mali na ajivunie unyenyekevu wake, kwani atanyauka kama maua ya majani.[#1 Petr. 1:24.]
11Kwani jua likicha na kuwaka kwa ukali huyakausha majani, maua yaanguke, uzuri wao uliofurahisha macho uangamie. Vivyo hivyo naye mwenye mali hunyauka katika mienendo yake.[#Yes. 40:6-7.]
12Mwenye shangwe ni mtu anayevumilia akijaribiwa. Kwani akiisha kushinda atapewa kilemba chenye uzima, Mungu alichowaagia wale wampendao.[#2 Tim. 4:8.]
13Mtu akijaribiwa asiseme: Najaribiwa na Mungu! Kwani Mungu hajaribiki nayo maovu, naye mwenyewe hajaribu mtu.
14Ila kila mtu hujaribiwa akivutwa na kuhimizwa na tamaa yake mwenyewe.[#1 Mose 3:6; Rom. 7:7-8.]
15Kisha tamaa ikijitunisha huzaa makosa, nayo makosa yakikomaa huzaa kufa.[#Rom. 7:10.]
16*Msidanganyike, ndugu zangu wapendwa![#Mat. 7:11; 1 Yoh. 1:5.]
17Kila kipaji kizuri na kila gawio timilifu hutoka juu kwa Baba alie mwenye mianga. Yeye hageuki, wala kwake hakupokeani mwanga na giza.
18Kwa hayo, ayatakayo, alituzaa sisi kwa nguvu ya Neno lililo kweli, tupate kuwa kama malimbuko ya viumbe vyake.[#Yoh. 1:13; 1 Petr. 1:23.]
19Mwajua, ndugu zangu wapendwa: kila mtu awe mwepesi, apate kusikia, lakini awe mpole, asiseme upesi, tena mpole, asipatwe na makali upesi![#Mbiu. 7:9.]
20Kwani makali ya mtu hayafanyi yaongokayo mbele ya Mungu.[#Ef. 4:26.]
21Kwa hiyo uvueni uchafu wote na ule uovu mwingi uliowashika! Lipokeeni kwa upole Neno lililopandwa mwenu, liwezalo kuziokoa roho zenu!*[#Kol. 3:8; 1 Petr. 2:1.]
22*Mwe wafanyaji wa Neno, msiwe wasikiaji tu! Kwani hivyo mwajidanganya wenyewe.[#Mat. 7:26; Rom. 2:13.]
23Kwani mtu akiwa msikiaji wa Neno, asiwe hata mfanyaji, huyo amefanana na mtu aliyetazama katika kioo, uso wake ulivyo;
24akiisha kujitazama huenda zake, akasahau upesi, alivyokuwa.
25Lakini achunguliaye, aone, Maonyo yalivyotimilika hapo, tulipokombolewa, akishikamana navyo, hawezi kuwa msikiaji asahauye upesi, aliyoyasikia, ila huwa mfanyaji wa kazi yake, naye atakuwa mwenye shangwe kwa kule kufanya kwake.[#Yak. 2:12; Yes. 48:18; Yoh. 13:17; Rom. 8:2.]
26Mtu akijiwazia kuwa mwenye kumtumikia Mungu, lakini haushindi ulimi wake, anaudanganya moyo wake mwenyewe, kwa hiyo matumikio yake ni ya bure.[#Sh. 34:14.]
27Matumikio yatakatayo yasiyo yenye doa hata machoni pa Mungu Baba ndiyo haya: kukagua watoto waliofiwa na wazazi na kukagua nao wanawake wajane katika maumivu yao na kujilinda wenyewe, tusijitie katika machafu ya ulimwwengu huu.*