Waamuzi 1

Waamuzi 1

Vita, Wayuda walivyovipiga.

1Yosua alipokwisha kufa, wana wa Isiraeli wakamwuliza Bwana kwamba: Yuko nani kwetu atakayeanza kupanda kwao Wakanaani kupigana nao?[#Amu. 20:18.]

2Bwana akasema: Yuda ndiye atakayepanda, nanyi mtaona, ya kuwa nimeitia nchi hii mikononi mwake.

3Ndipo, Yuda alipomwambia ndugu yake Simeoni: Panda pamoja nami katika nchi hiyo, niliyoipata kwa kura, tupigane na Wakanaani! Kisha nami nitapanda na wewe katika nchi, uliyoipata wewe kwa kura. Kwa hiyo Simeoni akaenda naye.

4Yuda alipopanda, Bwana akawatia Wakanaani na Waperizi mikononi mwao, wakapiga kule Bezeki watu 10000.

5Walipomwona Adoni-Bezeki hapo Bezeki wakapigana naye, wakawapiga Wakanaani na Waperizi.

6Adoni-Bezeki alipokimbia, wakamfuata upesi, wakamkamata; ndipo, walipomkata vidole gumba vya mikono na vya miguu.

7Naye Adoni-Bezeki akasema: Wafalme 70 waliokatwa vidole gumba vya mikono na vya miguu walikuwa wakiokota vyakula vyao chini ya meza yangu, kama nilivyofanya, ndivyo, Mungu alivyonilipisha, kisha wakampeleka Yerusalemu, akafa huko.

8Kisha wana wa Yuda wakapiga vita huko Yerusalemu, wakauteka, wakawapiga wenyeji kwa ukali wa panga, nao mji wakauchoma moto.

9Baadaye wana wa Yuda wakashuka kupigana na Wakanaani waliokaa milimani na kusini na katika nchi ya tambarare.[#Yos. 10:40; 11:22.]

(10-15: Yos. 15:13-19.)

10Kisha Wayuda wakawaendea Wakanaani waliokaa Heburoni, nalo jina la Heburoni kale lilikuwa Kiriati-Arba, wakampiga Sesai na Ahimani na Talmai.

11Walipotoka huko wakawaendea wenyeji wa Debiri, nalo jina la Debiri kale lilikuwa Kiriati-Seferi.

12Hapo Kalebu akasema: Atakayepiga Kiriati-Seferi na kuuteka nitampa mtoto wangu Akisa kuwa mkewe.

13Otinieli, mwana na Kenazi, mdogo wake Kalebu, alipouteka, akampa mtoto wake Akisa kuwa mkewe.

14Ikawa, huyu alipofika kwake akamhimiza mumewe kuomba shamba kwa baba yake Kalebu: basi, Akisa aliposhuka katika punda, Kalebu akamwuliza: Unataka nini?

15Naye akamwambia: Nipe tunzo la kunibariki! Kwa kuwa umenipeleka katika nchi ya kusini, nipe nazo mboji za maji! Ndipo, Kalebu alipompa zile mboji zilizokuwa upande wa juu, nazo zilizokuwa upande wa chini.

16Nao wana wa Keni, shemeji yake Mose, walikuwa wametoka kwao Mjini kwa Mitende, wapande nao wana wa Yuda kukaa katika nyika ya Yuda iliyoko kusini kuelekea Aradi; ndivyo, walivyokuja kukaa na watu wa ukoo huo.[#Amu. 4:11,17; 4 Mose 10:29; Yos. 12:14.]

17Kisha Wayuda wakaenda pamoja na ndugu zao Wasimeoni, wakawapiga Wakanaani waliokaa Sefati, wakauangamiza wote kwa kuutia mwiko wa kuwapo, kisha wakaliita jina la mji huo Horma (Mwiko).[#4 Mose 21:2.]

18Kisha Wayuda wakauteka Gaza na mitaa iliyoko mipakani kwake na Askaloni na mitaa iliyoko mipakani kwake na Ekroni na mitaa iliyoko mipakani kwake.

19Bwana akawa nao Wayuda, akawapa kuichukua milima, lakini waliokaa bondeni hawakuweza kuwafukuza, kwani walikuwa na magari ya chuma.

20Kisha wakampa Kalebu mji wa Heburoni, kama Mose alivyoagiza; naye akawafukuza humo wale wana watatu wa Anaki.[#Yos. 14:6-15.]

21Lakini wana wa Benyamini hawakuwafukuza Wayebusi waliokaa Yerusalemu, kwa hiyo Wayebusi wakakaa Yerusalemu pamoja na wana wa Benyamini mpaka siku hii ya leo.[#Yos. 15:63; 18:28; Amu. 1:8.]

Vita vya wana wa Yosefu.

22Wao wa mlango wa Yosefu walipopanda nao kuujia Beteli, Bwana akawa nao.

23Wao wa mlango wa Yosefu wakaupeleleza Beteli; nao jina la mji huu kale uliitwa jina lake Luzi.[#1 Mose 28:19.]

24Walinzi walipoona mtu, akitoka mjini, wakamwambia: Tuonyeshe pa kuuingilia mji huu, nasi tutakufanyizia mambo ya upole.

25Alipowaonyesha pa kuuingilia mji, wakawapiga wenyeji kwa ukali wa panga, lakini yule mtu wakamwacha, ajiendee na ukoo wake wote.[#Yos. 6:25.]

26Naye huyo mtu akaenda katika nchi ya Wahiti, akajenga mji, akauita jina lake Luzi, ndilo jina lake mpaka siku hii ya leo.

Milango mingine haikuwafukuza Wakanaani wote.

27Wamanase hawakuwafukuza wenyeji wa Beti-Seani na wa mitaa yake, wala wa Taanaki na wa mitaa yake, wala wa Dori na wa mitaa yake, wala wenyeji wa Ibileamu na wa mitaa yake, wala wenyeji wa Megido na wa mitaa yake. Ndivyo, Wakanaani walivyopata kukaa kwanza katika nchi hii.[#Yos. 17:11-13.]

28Lakini Waisiraeli walipopata nguvu, wakawashurutisha Wakanaani kuwafanyia kazi za kutumwa, lakini kufukuza hawakuwafukuza.

29Nao Waefuraimu hawakuwafukuza Wakanaani waliokuwa wenyeji huko Gezeri, ila Wakanaani wakakaa katikati yao huko Gezeri.[#Yos. 16:10.]

30Nao Wazebuluni hawakuwafukuza wenyeji wa Kitironi wala wenyeji wa Nahaloli; lakini wao wakawatumikia.[#Yos. 19:15.]

31Nao Waaseri hawakuwafukuza wenyeji wa Ako, wala wenyeji wa Sidoni, wala wa Alabu, wala wa Akizibu, wala wa Helba, wala wa Afiki, wala wa Rehobu.

32Kwa hiyo Waaseri walikaa katikati ya Wakanaani waliokuwa wenyeji wa nchi hii, kwani hawakuwafukuza.

33Wanafutali hawakuwafukuza wenyeji wa Beti-Semesi, wala wenyeji wa Beti-Anati, wakakaa katikati ya Wakanaani waliokuwa wenyeji wa nchi hii, lakini watu wa Beti-Semesi na wa Beti-Anati wakawatumikia.[#Yos. 19:38.]

34Lakini Waamori wakawatesa wana wa Dani, waende milimani, wakawazuia, wasishuke kukaa bondeni.

35Ndivyo, Waamori walivyopata kukaa kwanza mlimani kwa Heresi na Ayaloni na Salabimu; lakini mikono yao wa mlango wa Yosefu ilipowalemea, wakawatumikia.[#Yos. 19:42.]

36Nayo nchi ya Waamori ilianzia hapo pa kukwelea Akarabimu, ikaendelea kutokea huko gengeni hata juu.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania