Yeremia 2

Yeremia 2

Waisiraeli wamemwacha Mungu wakikataa kumshukuru.

1Neno la Bwana likanijia kwamba:

2Nenda kutangaza masikioni mwao Wayerusalemu kwamba: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Nayakukumbukia magawio ya ujana wako na upendo wa uchumba wako, uliponifuata nyikani katika nchi isiyowezekana kupandwa mbegu.

3Hapo Waisiraeli walikuwa wamejitakasa kuwa wa Bwana, wakawa malimbuko ya mavuno yake; wote waliotaka kuwala wakakora manza, mabaya yakawajia; ndivyo, asemavyo Bwana.

4Lisikilizeni Neno la Bwana ninyi wa mlango wa Yakobo nanyi vizazi vyote vya mlango wa Isiraeli!

5Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Baba zenu waliona mapotovu gani kwangu wakiniacha mbali wakaja kuyafuata yasiyo maana na kufanya wenyewe yasiyo maana?[#Mika 6:3-5.]

6Hawakuuliza: Bwana yuko wapi aliyetutoa katika nchi ya Misri, aliyetuongoza nyikani katika nchi zenye jangwa na makorongo, katika nchi kavu ziuazo, katika nchi zisizopitwa na mtu, zisizokaa mtu?

7Nilipowapeleka katika nchi ichipukayo vizuri, myale matunda yake na mema yake, basi, hapo mlipoiingia mliitia nchi yangu machafu, iliyokuwa fungu langu mkaigeuza kuwa tapisho.

8Watambikaji hawakuuliza: Bwana yuko wapi? Wala wenye kazi za Maonyo hawakunijua, wabaya wakanikosea, wafumbuaji wakafumbua mambo ya Baali, wakayafuata yasiyofaa.

9Kwa hiyo Bwana asema: Kweli inanipasa kufuliza kuwagombeza ninyi, nao wana wa wana wenu nitawagombeza.

10Haya! Vukeni, mfike pwani kwa Wakiti, mwone! Tumeni watu, waje Kedari, mtambue vema na kuona, kama yamekuwako mambo kama hayo!

11Mwone, kama liko taifa lililoiacha miungu ya kwao na kufuata mingine, nayo siyo miungu! Nao walio ukoo wangu wameuacha utukufu wao wakifuata yasiyofaa.[#Rom. 1:23.]

12Yastukeni, ninyi mbingu, mambo kama hayo! Zizimukeni kwa kushangaa kabisa! ndivyo, asemavyo Bwana.

13Kwani walio ukoo wangu wamefanya mabaya mawili: wameniacha mimi niliye kisima chenye maji ya uzima, kisha wakajichimbia visima vingine, navyo ni visima vyenye nyufa visivyoweza kushika maji.[#Yer. 17:13; Sh. 36:10.]

14Je? Isiraeli ni mtumwa au mzalia wa nyumbani? Mbona wamekuwa mateka?

15Simba wanamngurumia na kupaza sauti zao, wakaigeuza nchi yake kuwa mapori tu, miji yake imeteketezwa, haina mwenye kukaa humo.

16Kisha Wamisri wa Nofu na wa Tahapanesi wakaulisha utosi wako.[#Yer. 44:1.]

17Kulikokupatia hayo siko kumwacha Bwana Mungu wako, alipotaka kukuongoza njiani?[#Hos. 13:9.]

18Na sasa kwa sababu gani unakwenda Misri kunywa maji ya Sihori? Tena kwa sababu gani unakwenda Asuri kunywa maji ya lile jito kubwa?

19Ubaya wako ndio unaokupiga, ubishi wako ndio unaokupatiliza. Yajue, yatazame, ya kuwa kumwacha Bwana Mungu wako ndiko kubaya kwenye uchungu! Nawe hukumwogopa kamwe. Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu wako Mwenye vikosi.

Kutambikia vinyago huangamiza.

20Kwani tangu kale ulivivunja vyuma vyako, ukazikata kamba zako, ukasema: Sitaki kumtumikia, ila kila kilima kirefu ulikipanda, hata kivulini kwa kila mti wenye majani mengi ukajilaza chini ukifuata ugoni.[#Yer. 3:6; Yes. 57:5; Ez. 6:13.]

21Nami ndimi, niliyekupanda, ulipokuwa tawi zuri lenyewe la mzabibu uliozaa matunda yaliyo mazuri kweli; sasa inakuwaje, ukinigeukia na kuleta machipukizi ya mzabibu mgeni?[#Yes. 5:1-4.]

22Ijapo ujioshe kwa magadi na kutumia hata sabuni nyingi, uchafu wa ubaya ulioufanya hautoki machoni pangu; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.

23Unasemaje? Sikujichafua, sikuyafuata mambo ya Baali? Itazame njia yako ya kwenda bondeni! Yajue, uliyoyafanya huko kwa kuwa kama jike la ngamia ajiendeaye huko na huko kwa nyege zake.

24Ukawa kama kihongwe cha kike azoeaye nyika, naye hutwetea upepo kwa kukimbizwa na tamaa ya roho yake; tena yuko nani awezaye kuzituliza nyege zake? Lakini amtafutaye hajichokeshi: mwezi wake unapotimia, humwona upesi.

25Iangalie miguu yako, usivichakaze viatu! Liangalie nalo koo lako, lisipatwe na kiu! Lakini wewe hujibu: Ni kazi bure kunionya, sionyeki, kwani ninapenda wageni, nitawafuata.

26Kama mwizi anavyoona soni akikamatwa, vivyo hivyo nao wa mlango wa Isiraeli sharti waone soni, wafalme wao na wakuu wao na watambikaji wao na wafumbuaji wao.

27Maana huuambia mti: Wewe ndiwe baba yangu. Hata jiwe huliambia: Wewe ulinizaa. Lakini mimi wamenigeukia migongo, sizo nyuso; lakini siku za kupatwa na mabaya huniambia: Inuka, utuokoe!

28Basi, miungu yako, uliyojifanyizia, iko wapi? Na iinuke, kama inaweza kukuokoa, unapopatwa na mabaya! Kama miji yako ilivyo mingi, ndivyo, nayo miungu yako, wewe Yuda, ilivyo mingi.[#Amu. 10:14; Yer. 11:13.]

29Mbona unanigombeza? Ninyi nyote mmenitengua; ndivyo, asemavyo Bwana.

30Imekuwa ya bure, nikiwapiga wana wenu, maana hawakuonyeka, panga zenu zikawala wafumbuaji wenu, kama simba wanavyoangamiza.[#Yes. 1:5.]

31Ninyi mlio uzao mbaya, liangalieni Neno la Bwana! Je? Nimegeuka kuwawia Waisiraeli kama nyika au kama nchi yenye giza? Kwa sababu gani walio ukoo wangu husema: Tumekwisha kujiendea, haturudi kwako tena.

32Je? Yuko mwanamwali asahauye kujipamba au mchumba asahauye kuvaa yapasayo ndoa? Nao walio ukoo wangu wamenisahau siku zisizohesabika.

33Unajuaje kuitengeneza njia yako vizuri ukitafuta wapenzi? Kweli hivyo ndivyo, ulivyojifundisha mabaya nayo katika njia zako.

34Kumbe hata mapindo ya nguo zako yameshikwa na damu zao wakiwa waliouawa pasipo makosa yao yo yote. Nao hukuwapata, wakipokonya, ila ni mambo yayo hayo.

35Kisha ukasema: Sikukosa kamwe: Kwa hiyo makali yake yameondoka kwangu. Na unione, nikikupatiliza kwa kusema kwako: Sikukosa![#Yes. 43:26.]

36Mbona unatangatanga sana, uigeuze njia yako? Hata Wamisri watakutia soni, kama Waasuri walivyokutia soni.

37Huko nako utatoka, mikono yako ikiwa kichwani, kwani Bwana amewakataa, uliowakimbilia; kwa hiyo hakuna, utakachokipata kwao.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania