The chat will start when you send the first message.
1Kweli, ninyi tu ndio walio watu,
2werevu wa kweli utakufa nao, mtakapokufa ninyi.
3Mimi nami ninazo akili kama ninyi, sikupungukiwa na akili, ninyi mnishinde, yuko nani asiyeyajua mambo kama hayo?
4Mtu wa kuchekwa na wenziwe ni mimi, mimi niliyemwita Mungu, akaniitikia; kweli mwongofu asiyekosa kabisa ni mtu wa kuchekwa.
5Atesekaye hubezwa moyoni mwake naye akaaye na kutulia, yuko tayari kuwasukuma wajikwaao miguu.
6Mahema yao wapokonyi hutengemana, nao wamkasirishao Mungu hukaa na kutulia, ndio, Mungu anaowatia mengi mikononi mwao.
7Haya! Uliza nyama, wakufundishe, nao ndege wa angani, wakueleze!
8Au sema na nchi yenyewe, nayo itakufundisha! Hata samaki wa baharini watakusimulia mambo.
9Yuko nani asiyeyajua haya yote, ya kuwa mkono wa Mungu ndio ulioyatengeneza haya?
10Mkononi mwake zimo roho zao hao nyama wote, zimo nazo pumzi zao wote wenye miili ya kimtu.[#4 Mose 16:22.]
11Sikio silo linaloyajaribu yanayosemwa, kama ufizi unavyovionja vyakula vyake?
12Werevu wa kweli uko kwao walio wazee, siku zikiwa nyingi, mtu hupata utambuzi.[#Iy. 8:8.]
13Werevu wa kweli na uwezo uko kwake Mungu, tena wongozi na utambuzi.
14Tazama: Akibomoa, hapajengwi tena; akimfunga mtu, hafunguliwi tena.
15Tazama: Akiyazuia maji, hukauka; tena akiyaachia huifudikiza nchi.[#1 Mose 7:19-23; 1 Fal. 17:1,7.]
16Yeye ni mwenye nguvu na uwezo wa kufanya mambo, wake yeye ni apoteaye naye apotezaye.
17Wenye kukata mashauri huwapeleka kuwa mateka, nao waamuzi huwapumbaza.
18Mafungo ya wafalme huyafungua, tena huwafunga wenyewe kwa kamba viunoni pao.
19Nao watambikaji huwapeleka kuwa mateka, nao wenye nguvu huwaangamiza.
20Waliotegemewa kuwa mafundi wa kusema huwasemesha kibubu, nazo akili zao wazee huzipumbazisha.
21Huwamwagia mabezo walio wakuu, nao wenye nguvu huwalegeza mikanda.
22Huvumbua yaliyofichwa ndani ya nchi na kuyatoa gizani, nacho kivuli kiuacho hukitokeza mwangani.
23Hukweza mataifa, kisha huyaangamiza, hueneza mataifa mahali, kisha huyaacha, yatekwe.
24Wakuu wa makabila ya huku nchini huwatia kichaa, kisha huwapoteza nyikani pasipo na njia,
25wapapasepapase gizani pasipo na mwanga, huwaacha, wapepesuke kama mlevi.[#Iy. 5:14.]