The chat will start when you send the first message.
1Tazameni! Jicho langu limeyaona hayo yote pia, sikio langu limeyasikia na kuyatambua.
2Mnayoyajua ninyi, nimeyajua ami, sikupungukiwa na akili, ninyi mnishinde.[#Iy. 12:3.]
3Kweli mimi na niseme naye Mwenyezi, napenda sana kujikania kwake Mungu.
4Kweli ninyi hutunga maneno yaliyo ya uwongo, nyote m waganga wasiofaa.
5Kama mngenyamaza kimya kabisa, mngejitokeza kuwa wenye werevu ulio wa kweli.[#Fano. 17.]
6Sikieni, jinsi ninavyojikania! Yategeni masikio, midomo yangu ikiyasema mashindano yangu!
7Je? Mtamtetea Mungu kwa kusema yaliyo mapotovu? Au mtamtetea kwa kusema yaliyo madanganyifu?
8Je? Mtampendelea Mungu kwa kumgombea magomvi yake?
9Je? Akiwachunguza ninyi, ingekuwa vema? Au mtaweza kumdanganyadanganya, kama watu wanavyodanganyana?
10Atawakemea kwa nguvu, mkipendelea watu na kufichaficha.
11Je? Utukufu wake hautawatia woga? Kitisho chake nacho hakitawaangukia ninyi?
12Makumbusho yenu ni mafumbo ya kijivu, nazo ngome zenu ni ngome za udongo.
13Ninyamazieni mimi, nipate kusema nami! Yatakayonijia na yanijie!
14Ingefaaje, nikiuma nyama za mwili wangu kwa meno yangu? Au nikiiweka roho yangu mikononi mwangu?
15Mtaona, akiniua; hakuna kingine, nikingojeacho; ninataka tu kumwelezea njia zangu usoni pake.
16Hili tu litasaidia kuniokoa, kwani mwovu hatokei usoni pake.
17Lisikilizeni vema neno langu, nayo maelezo yangu na yaingie masikioni mwenu!
18Tazameni! Nimelitengeneza shauri langu, najua, ya kuwa nitajitokeza kuwa asiyekosa.
19Yuko nani atakayebishana na mimi hapa? Kama yuko, ningenyamaza tu, nipate kuzimia.
20Haya mawili ninayataka, unifanyie, nisije kujificha usoni pako:
21uondoe mkono wako, usinilemee! Tena kizuie kitisho chako, kisinistushe![#Iy. 9:34.]
22Kisha hapo, utakaponiita, mimi nitakuitikia! Au mimi niseme, nawe unijibu!
23Maovu yangu na makosa yangu, niliyoyafanya, ni mangapi? Nijulishe mapotovu yangu nayo makosa yangu!
24Mbona unauficha uso wako, ukaniwazia kuwa miongoni mwao wapingani wako?[#Iy. 19:11.]
25Utatetemesha jani lipeperushwalo? Au utakimbiza kibua kilicho kikavu?
26Kwani unaniandikia machungu kama haya, tena unanilipisha manza, nilizozikora nilipokuwa nikingali mwana.[#Sh. 25:7.]
27Nayo miguu yangu unaitia mikatale, ukapaangalia pote, nipitiapo, napo, nyayo za miguu yangu zinapokanyaga, unachora alama zako.
28Nami ninanyauka kama mwenye kibovu, nafanana na nguo iliyoliwa na nondo.