Iyobu 15

Iyobu 15

1Yuko mwerevu wa kweli atakayejibu yenye ujuzi ulio kama upepo?

2Au yuko atakayelijaza tumbo lake upepo utokao maawioni kwa jua?

3Atamwonya mwenziwe kwa maneno yasiyofaa? Au atajisemea tu kwa mapuzi yasiyompatia mtu kitu?

4Kisha wewe unatangua kicho kiwacho chote, nayo mawazo ya kumnyenyekea Mungu unayabeua.

5Manza, ulizozikora, zinakifunza kinywa chako, ukachagua ulimi usemao yenye ujanja.

6Kinachokuumbua kuwa mwovu, si mimi, ni kinywa chako, nayo midomo yako ndiyo inayokusuta.

7Je? Mtu wa kwanza aliyezaliwa ni wewe? Au ulitoka tumboni mwa mama, milima ilipokuwa haijawa?

8Je? Ulizisikiliza njama za Mungu? Je? Ndiko, ulikouvuta werevu wa kweli, ukujie wewe?[#Iy. 11:7; Rom. 11:33.]

9Unajua mambo gani, tusiyoyajua nasi? Unao utambuzi gani usiopatikana kwetu?[#Iy. 13:2.]

10Wenye mvi walio wazee nako kwetu sisi wako, siku zao ni nyingi sana kuliko hizo za baba yako.

11Je? Hivyo, Mungu anavyotuliza mioyo, unaviwazia kuwa vidogo? Nalo neno la upole si kitu kwako?

12Mbona moyo wako unakuchukua, ukupeleke penginepo? Mbona macho yako unayang'arisha hivyo?

13Inakuwaje, ukiigeuza roho yako, ije kumpingia Mungu, ukamtolea maneno kama hayo kinywani mwako?

14Mtu ndio nini, aweze kutakata? Aliyezaliwa na mwanamke awezaje kuongoka?[#Iy. 14:4.]

15Kumbuka hili tu: nao watakatifu wake hawezi kuwategemea, nazo mbingu hazitakati machoni pake![#Iy. 4:18-19.]

16Sembuse mtu amchukizaye kwa upotevu, yeye mtu afanyaye maovu, kama ni kunywa maji tu!

17Nitakufunza, nisikilize! Niliyoyaona, na niyasimulie.

18Werevu wa kweli wanayoyatangaza ni yayo hayo, kwani waliyoambiwa na baba zao hawakuyasahau;

19walikuwa wamepewa nchi hii wao peke yao tu, wala hakuwako mgeni aliyepita kwao.

20Walisema: Asiyemcha Mungu hukaa siku zote na uchungu wake, vilevile mkorofi miaka yote, aliyowekewa na kuhesabiwa.[#1 Mose 4:14.]

21Sauti za mastusho huingia masikioni mwake, akikaa na kutengemana, mwangamizaji humjia.

22Hayategemei, ya kwamba atatoka gizani, hujiwazia kuwa amechaguliwa kuuawa na upanga.

23Hutangatanga kujipatia chakula, lakini akione wapi? Anajua, ya kuwa kando yake imekwisha kuwekwa siku ya giza.

24Mateso na masongano humtia woga, nayo humshinda kwa nguvu kama za mfalme aliyejiweka tayari kupiga vita.

25Kwa kuwa ameukunjua mkono wake, ampingie Mungu, akajivunia kuwa mwenye uwezo mbele yake Mwenyezi.

26Akapiga mbio na kunyosha shingo, aje kumshinda, akijikingia ngao yake yenye vitovu

27Akaunonesha uso wake kuwa wenye mafuta, navyo viuno vyake akavinenepesha.[#Sh. 73:7,18-20.]

28Katika miji iliyotakiwa kuwa mahame ndimo, alimotua, akakaa katika nyumba, ambazo watu hawazikai, ndizo zinazongoja tu kuwa machungu ya mawe.[#Yos. 6:26.]

29Kwa hiyo hatapata mali nyingi, nazo atakazozipata hazitakaa, wala mazao yake hayatafurikia katika nchi hii.

30Hatapata kuondoka mle gizani, nayo machipukizi yake hukaushwa na ndimi za moto, naye atatoweshwa kwa nguvu za pumzi za kinywa chake Mungu.

31Asitegemee mambo yaliyo ya bure, maana atadanganyika, nayo yatakayokuwa malipo yake yatakuwa ya bure.

32Siku yake ikiwa haijatimia bado, hayo yatatimia, shina lake halitapata kabisa, litakapochipuka tena.

33Kama mizabibu inavyopukutisha mapooza yao, au kama michekele inavyopakatisha maua yao,

34hivyo utakuwa mlango wake ambezaye Mungu, utakosa wazao wo wote, nao moto utayala mahema yao waliowapenyezea watu.

35Mateso ndio mimba zao, kwa hiyo huzaa maovu, hivyo matumbo yao hutoa udanganyifu.[#Sh. 7:15; Yes. 59:4.]

Jibu la nne la Iyobu: Anamtolea Mungu ukiwa wake.

Iyobu akajibu akisema:

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania