Iyobu 18

Iyobu 18

1Hata lini mtatanda matanzi, yanase maneno?

2Itambueni maana, kisha tusemeane!

3Tukiwaziwa kuwa kama nyama, ni kwa sababu gani? Mbona tunawaziwa kuwa wenye uchafu machoni penu?[#Iy. 17:4,10.]

4Wewe unajirarua mwenyewe kwa ukali wako? Je? Kwa ajili yako wewe nchi itaachwa, isikae mtu? Au mwamba utaondoka mahali, ulipokuwa?

5Kweli mwanga wake asiyemcha Mungu utazima, nazo cheche za moto wake hazitaangaza.[#Iy. 18:18; 21:17; Sh. 73:18-20; Fano. 13:9; 24:20.]

6Mwanga utakuwa giza hemani mwake, nacho kinara chake kilichomo kitazima.

7Miguu yake iliyokwenda kwa nguvu itasongeka, mashauri yake, aliyowapa wengine, yatambwaga chini.

8Kwani atanaswa miguu yake kwa wavu akitembea penye matanzi yaliyofichwa.

9Itakayokikamata kisigino chake ni kamba, itamshika kwa nguvu, mtambo ukifyatuka.

10Kitanzi cha kumnasia kimefichwa mchangani, hata njiani amewekewa mtego wa kumkamatia.

11Vitisho humstusha po pote na kuitia miguu yake woga, ikimbie sana.[#3 Mose 26:36.]

12Mabaya yanayomtaka ni yenye njaa ya kumla, mwangamizo uko tayari, upate kumwangusha,

13utavila viungo vya kuungia mwili ngozini mwake; mwana wa kwanza wa kifo atavila kweli hivyo viungo vyake.

14Atatolewa kwa nguvu hemani mwake, alimokimbilia, aendeshwe kufika kwake mfalme aliye mwenye mastusho.

15Hemani mwake watakaa wasio wa ukoo wake, nayo mawe ya kiberiti yatamwagwa juu ya kao lake.

16Chini mizizi yake itakauka, hata juu matawi yake yatanyauka.

17Ukumbuko wake utapotea, utoweke huku nchini, hatakuwa kabisa na sifa yo yote kwao walioko nje.[#Fano. 10:7.]

18Watamkumba, atoke mwangani, aje gizani, watamfukuza, atoke kabisa humu ulimwenguni.

19Hatakuwa na mwana wala mjukuu katika ukoo wake, wala hatakuwako atakayesalia katika makao yake.

20Siku yake wataistukia sana watakaotokea nyuma, kama wao waliokuwa mbele walivyokufa ganzi.[#Sh. 37:13.]

21Hayo ndiyo yatakayoyapata makao ya mpotovu napo mahali pake yeye asiyemjua Mungu.

Jibu la tano la Iyobu: Katika mateso yake anamkumbuka mwokozi wake.

Iyobu akajibu akisema:

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania