Iyobu 20

Iyobu 20

1Kwa sababu hii mawazo yangu yananishurutisha, nikujibu,

2maana ninachafuka sana moyoni mwangu.

3Ninasikia maneno ya kunikanya, nayo ya kunitukana, lakini kwa utambuzi wangu ninajibiwa mengine rohoni mwangu.

4Je? Hayo huyajui tangu kale, tangu hapo, watu walipokaa katika nchi?

5Ya kuwa shangwe zao wasiomcha Mungu hukoma upesi? Ya kuwa furaha ya mwovu hukaa kitambo kidogo tu?

6Ijapo ayakuze majivuno yake, yafike mbinguni, kichwa chake kiyaguse nayo mawingu,[#Sh. 37:35.]

7hupotelea kale na kale kama mavi yake, waliomwona waulize: yuko wapi?[#1 Fal. 14:10.]

8Hupita kwa kuruka kama ndoto, watu wasimwone tena, hufukuzwa kama ono baya la usiku.[#Sh. 73:20.]

9Jicho lililomchungulia halitomwona tena, wala mahali pake, alipokuwa, hapatamtazama tena.[#Sh. 37:10.]

10Wanawe watabembeleza walio wanyonge, mikono yao itazirudisha mali, alizozinyang'anya.[#Iy. 27:14.]

11Ijapo, mifupa yake izidi kuwa nazo nguvu za ujana, lakini haina budi kulala pamoja naye uvumbini.

12Kama anauona ubaya kuwa mtamu kinywani mwake, aufiche, upate kukaa chini ya ulimi wake,

13autunze vizuri, asitake kuuachilia, ujiendee, ila auzuie, usiondoke penye ufizi wake:

14kisha hicho chakula chake kitageuzwa tumboni mwake kuwa uchungu wa pili mle ndani yake;

15hizo mali nyingi, alizozimeza, hana budi kuzitapika, Mungu akizitoa kwa nguvu tumboni mwake.

16Kwa hivyo, alivyonyonya sumu iliyo ya pili, mwisho ulimi wa moma utamwua,

17asijifurahishe tena kwa kuvitazama vile vijito wala ile mito inayokwenda na kujaa asali na mafuta.

18Aliyoyasumbukia hana budi kuyarudisha, hawezi kuyameza, ijapo mapato yake yawe mengi mno, hayafurahii.[#5 Mose 28:30-33.]

19Kwani alipokwisha kuwaponda wanyonge, aliwaacha papo hapo, akanyang'anya nyumba, asizozijenga.

20Lakini hakujua kutulia ndani yake yeye; kwa hiyo hatapona pamoja nayo, aliyoyatunukia.

21Kwa ulafi wake hakikuwako kitu, asichokichukua; kwa sababu hii hivyo vyema vyake havikai kabisa.

22Hapo atakapofurikiwa, ndipo, atakaposongeka, mikono yao walioteswa naye ikimjia yote.

23Ndipo, Mungu atakapolijaza tumbo lake akituma kwake makali yake yawakayo moto, ayanyeshe juu yake yampatie chakula cha kushiba.

24Itakapokuwa, ayakimbie mata ya chuma, uta wa shaba utampiga, achomwe;

25akitaka kuutoa mshale, utakuwa umetokea mgongoni pake, chembe yake imetukayo itakuwa imeichoma nayo nyongo; basi, mastusho yatamjia vivyo hivyo.[#5 Mose 32:41; Sh. 7:13.]

26Mambo yote ya giza yako tayari kwake kuviangamiza vilimbiko, nao moto uwakao pasipo kupulizwa utamla mwenyewe, nayo yaliyosalia hemani mwake utayamaliza.[#5 Mose 32:22.]

27Mbingu zitazifunua manza, alizozikora, nayo nchi itainuka kumshinda shaurini.

28Nyumba yake iliyompatia yatatekwa, yatakuwa kama maji yakaukayo, siku ya ukali wake Mungu itakapotimia.

29Hilo ndilo fungu, mtu asiyemcha Mungu atakalolipata kwake Mungu, ndio urithi, atakaogawiwa naye Mungu.

Jibu la sita la Iyobu: waovu hutulia, mpaka watakapopatilizwa.

Iyobu akajibu akisema:

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania