The chat will start when you send the first message.
1Je? Mtu hashurutishwi kufanya kazi ya vita huku nchini? Siku zake si sawa kama siku zake mkibarua?[#Iy. 14:6.]
2Huwa kama mtumwa atweteaye kivuli, au kama mkibarua aungojeaye mshahara wake.
3Vivyo hivyo nami nimepewa miezi ya kuteseka, iwe fungu langu, nikagawiwa masumbuko usiku kwa usiku.
4Ninapolala nasema: Nitainuka lini? kwani saa za usiku huwa ndefu sana, nikazidi kujigeuzageuza kitandani, mpaka kuche.
5Nyama za mwili wangu zimevikwa funyo na maganda yenye vumbi, ngozi yangu inapopona kidonda, papo hapo hutumbuka jipu tena.
6Siku zangu hupita upesi sana kuliko chombo cha kufumia, sinacho kingojeo cho chote, ila zimalizike tu.[#Yes. 38:12.]
7Kumbuka, ya kuwa siku zangu za kuwapo ni pumzi tu, jicho langu halitarudi huku, lipate kuona mema.
8Jicho lake anionaye sasa halitanitazama tena, macho yako yatakaponielekea, nitakuwa sipo.
9Kama wingu linavyopoteleapotelea, mpaka litoweke, vivyo hivyo naye ashukaye kuzimuni hatokei tena;
10hawezi kurudi tena, aingie nyumbani mwake, wala mahali pake, alipokuwa, hapamtambui tena.[#Iy. 10:21; 14:10-12; 16:22; Sh. 103:16.]
11Kwa hiyo mimi sitakizuia kinywa changu, niseme kwa kusongeka rohoni mwangu, nilie kwa uchungu wa moyo wangu.
12Je? Mimi ni kama bahari au kama nyangumi, ukiniwekea watu wa kuniangalia?
13Nikisema: Kilalo changu ndicho kitakachonituliza moyo, kitanda changu kitanipunguzia vilio vyangu,
14ndipo, unaponitisha kwa kuniotesha ndoto, kwa kunionyesha maono unanistusha.
15Kwa hiyo roho yangu inapenda kunyongwa tu, kuliko kuwa gofu la mtu, kama nilivyo, inapenda kufa kweli.
16Nimekata tamaa kwa kukataa kuwapo kale na kale; kwa sababu siku zangu ni za bure, uniache tu![#1 Fal. 19:4.]
17Mtu ndio nini, ukimkuza, ukimwelekezea moyo wako, umwangalie?[#Iy. 14:1-5; Sh. 8:5.]
18Ukimkagua kila kunapokucha? Ukimjaribu punde kwa punde?
19Mbona hutakoma kunitazama? Hutaniacha peke yangu, niyameze mate yangu?
20Kama nimekosa, nimekufanyia nini, wewe mlinda watu? Mbona umeniweka kuwa shabaha yako ya kuipiga, mpaka nikijiona mwenyewe kuwa mzigo?
21Mbona huniondolei maovu yangu, ukazitowesha nazo manza, nilizozikora? Kwani sasa ninakwenda zangu kulala uvumbini; utakaponitafuta mapema utaniona, sipo.