The chat will start when you send the first message.
1Ikawa, Adoni-Sedeki, mfalme wa Yerusalemu, aliposikia, ya kuwa Yosua ameuteka Ai na kuutia mwiko wa kuwapo, ya kuwa Waai na mfalme wao amewafanyizia yaleyale, aliyoufanyizia Yeriko na mfalme wake, tena ya kuwa wenyeji wa Gibeoni wamepatana nao Waisiraeli, wakapata kukaa katikati yao:[#Yos. 8:9.]
2wakaingiwa na woga kabisa, kwani Gibeoni ulikuwa mji mkubwa kama mji mwingine wo wote katika ufalme wake, tena ni mkubwa kuliko Ai, nao watu wake wote walikuwa mafundi wa vita.
3Kwa hiyo Adoni-Sedeki, mfalme wa Yerusalemu, akatuma kwa Hohamu, mfalme wa Heburoni, na kwa Piramu, mfalme wa Yarmuti, na kwa Yafia, mfalme wa Lakisi, na kwa Debiri, mfalme wa Egloni, kwamba:
4Pandeni kuja kwangu, mnisaidie, tuwapige Wagibeoni, kwa kuwa wamepatana naye Yosua nao wana wa Isiraeli!
5Ndipo, walipokusanyika kwenda vitani hawa wafalme watano wa Waamori, mfalme wa Yerusalemu na mfalme wa Heburoni na mfalme wa Yarmuti na mfalme wa Lakisi na mfalme wa Egloni, wao na majeshi yao, wakapiga makambi huko Gibeoni kuupelekea vita.
6Ndipo, watu wa Gibeoni walipotuma Gilgali makambini kwa Yosua kwamba: Usiilegeze mikono yako ukiacha kuwasaidia watumwa wako! Ila panda upesi kuja kwetu, utuokoe na kutusaidia! Kwani wafalme wote wa Waamori wanaokaa milimani wametukusanyikia.
7Ndipo, Yosua alipotoka Gilgali kupanda kwao, yeye nao wapiga vita wote waliokuwa naye, nao hao wote walikuwa mafundi wa vita wenye nguvu.
8Naye Bwana akamwambia Yosua: Usiwaogope! Kwani nimewatia mikononi mwako, hakuna mtu wa kwao atakayesimama usoni pako.
9Ndipo, Yosua alipowaendea akitoka Gilgali kwenda usiku kucha, awashambulie kwa mara moja.
10Naye Bwana akawastusha, walipowaona Waisiraeli, wakawapiga kule Gibeoni pigo kubwa wakiwafukuza, waikimbilie njia ya kupandia Beti-Horoni, wakawapiga hata kufika Azeka na Makeda.
11Ikawa, walipowakimbia Waisiraeli, walipofika pa kushukia Beti-Horoni, Bwana akawanyeshea mvua ya mawe makubwa toka mbinguni, mpaka wafike Azeka na kuuawa vivyo hivyo; nao waliouawa na mvua ya mawe walikuwa wengi kuliko wao, wana wa Isiraeli waliowaua kwa panga.[#2 Mose 9:22-25.]
12Siku hiyo, Bwana alipowatoa Waamori machoni pa wana wa Isiraeli, ndipo, Yosua alipomwomba Bwana akisema masikioni pa Waisiraeli:
Jua, simama kimya huko Gibeoni!
Nawe mwezi, bondeni kwa Ayaloni!
13Ndipo, jua liliposimama kimya, nao mwezi ukasimama, hata watu wawalipize adui zao. Kumbe haya hayakuandikwa katika kitabu cha Mnyofu? Basi, jua likasimama katikati ya mbinguni, lisijihimize kuchwa muda kama wa siku nzima.[#2 Sam. 1:18; Hab. 3:11.]
14Siku ndefu kama hiyo haikuwa mbele yake wala nyuma yake, Bwana alipoisikia sauti ya mtu wake, kwani ndivyo, Bwana alivyowagombea Waisiraeli.[#Yos. 10:42; 2 Mose 14:25.]
15Kisha Yosua akarudi makambini kwa Gilgali pamoja na Waisiraeli wote waliokuwa naye.
16Wale wafalme watano wakakimbia, wakajificha pangoni kule Makeda.
17Yosua alipopashwa habari kwamba: Hao wafalme watano wameonekana, wamejificha pangoni huko Makeda,
18Yosua akaagiza: Poromosheni mawe makubwa hapo pa kuliingilia lile pango, kisha wekeni hapo watu wa kuwaangalia!
19Lakini ninyi msisimame bure! Ila pigeni mbio kuwafuata adui zenu, mwaue walio nyuma yao, msiwaache, waingie mjini kwao! Kwani Bwana Mungu wenu amewatia mikononi mwetu.
20Ikawa, Yosua na wana wa Isiraeli walipokwisha kuwapiga pigo hili kubwa sana, hata wamalizike, nao waliopona kwa kukimbia walipokwisha kuingia miji yenye maboma,
21ndipo, watu wote waliporudi salama makambini kwa Yosua kule Makeda, hakuna mtu tena aliyeuchongoa ulimi wake kuwasimanga wana wa Isiraeli.
22Kisha Yosua akaagiza: Pafungueni pa kuliingilia lile pango, mwatoe wale wafalme watano mle pangoni na kuwaleta kwangu!
23Wakafanya hivyo, wakawatoa wale wafalme watano pangoni, wakawapeleka kwake; ni mfalme wa Yerusalemu na mfalme wa Heburoni na mfalme wa Yarmuti na mfalme wa Lakisi na mfalme wa Egloni.
24Ikawa, walipowatoa hawa wafalme na kuwapeleka kwa Yosua, Yosua akawaita Waisiraeli wote, akawaambia wakuu wa wapiga vita waliokwenda naye: Karibuni, mwiweke miguu yenu juu ya kosi za wafalme hawa! Ndipo, walipowakaribia, wakaiweka miguu yao juu ya kosi zao.
25Yosua akawaambia: Msiogope, wala msiingiwe na vituko! Jipeni mioyo, mpate nguvu! Kwani hivyo ndivyo, Bwana atakavyowafanyizia adui zenu wote, mtakapopigana nao.
26Baadaye Yosua akawapiga na kuwaua, kisha akawatungika katika miti mitano; nao wakawa wakining'inia mpaka jioni.
27Ikawa hapo, jua lilipokuchwa, Yosua akatoa amri, ndipo, walipowashusha katika hiyo miti, wakawatupa mle pangoni, walimokuwa walijificha, wakaweka mawe makubwa hapo pa kuliingilia lile pango, nayo yako palepale hata siku hii ya leo.[#Yos. 8:29; 5 Mose 21:23.]
28Siku hiyo Yosua akauteka Makeda; waliokuwamo akawaua kwa ukali wa panga, hata mfalme wake, akiwatia mwiko wa kuwapo wao wote pia waliokuwamo, wasiachwe kabisa, hakusaza hata mmoja aliyekimbia; naye mfalme wa Makeda akamfanyizia yaleyale, aliyomfanyizia mfalme wa Yeriko.[#Yos. 6:21.]
29Yosua na Waisiraeli wote waliokuwa naye walipoondoka Makeda, wakaenda Libuna, wakapiga vita nao Walibuna.
30Bwana akautia nao mji huu pamoja na mfalme wake mikononi mwa Waisiraeli, wakawapiga kwa ukali wa panga wote pia waliokuwamo, hawakusaza hata mmoja aliyekimbia; naye mfalme wake wakamfanyizia yaleyale, waliyomfanyizia mfalme wa Yeriko.
31Yosua na Waisiraeli wote waliokuwa naye walipoondoka Libuna wakaenda Lakisi, wakapiga makambi huko, wapigane nao.
32Bwana akautia Lakisi mikononi mwa Waisiraeli, wakauteka siku ya pili, wakawapiga kwa ukali wa panga wote pia waliokuwamo, wakawafanyizia yote, waliyowafanyizia Walibuna.
33Siku hizo ndipo, Horamu, mfalme wa Gezeri, alipopanda kuusaidia mji wa Lakisi, lakini Yosua akampiga pamoja na watu wake, asisaze kwake hata mmoja aliyekimbia.
34Yosua na Waisiraeli wote waliokuwa naye walipoodoka Lakisi wakaenda Egloni, wakapiga makambi huko, wapigane nao.
35Wakauteka siku hiyo, wakawapiga kwa ukali wa panga wakiwatia mwiko wa kuwapo wao wote pia waliokuwamo, wasiachwe kabisa siku hiyo, wakawafanyizia yote, waliyowafanyizia Walakisi.
36Yosua na Waisiraeli wote waliokuwa naye walipoondoka Egloni wakaenda Heburoni, wakapiga vita nao.
37Walipouteka wakawapiga watu kwa ukali wa panga pamoja na mfalme wa huko, hata miji yake yote; kwao wote waliokuwamo hawakusaza hata mmoja aliyekimbia, wakiyafanya yote, waliyowafanyizia Waegloni na kuwatia mwiko wa kuwapo wao wote waliokuwamo, wasiachwe kabisa.
38Kisha Yosua na Waisiraeli wote waliokuwa naye wakaurudia Debira, wakapiga vita nao.
39Akamkamata mfalme na kuiteka miji yake yote, nao watu wakawapiga kwa ukali wa panga, wakiwatia mwiko wa kuwapo wao wote pia waliokuwamo, wasiachwe kabisa, hawakusaza hata mmoja aliyekimbia; kama walivyowafanyizia Waheburoni, ndivyo, walivyowafanyizia Wadebira nao; naye mfalme wa huko wakamfanyizia yaleyale, waliyowafanyizia Walibuna na mfalme wao.
40Ndivyo, Yosua alivyoipiga hiyo nchi yote, ile ya milimani nayo ya kusini nayo ya nchi ya tambarare nayo ya matelemko pamoja na wafalme wao, hakusaza hata mmoja aliyekimbia. Wenye kuvuta pumzi wote akawatia mwiko wa kuwapo, wasiachwe kabisa, kama Bwana Mungu wa Isiraeli alivyoagiza.[#4 Mose 21:2; 5 Mose 20:16-18.]
41Yosua akawapiga kutoka Kadesi-Barnea mpaka Gaza, nayo nchi yote ya Goseni mpaka Gibeoni.[#Yos. 11:16.]
42Wafalme hao wote Yosua akawateka pamoja na nchi zao kwa mara moja, kwani Bwana Mungu wa Isiraeli aliwapigia Waisiraeli vita.[#Yos. 10:14.]
43Kisha Yosua na Waisiraeli wote waliokuwa naye wakarudi Gilgali makambini.[#Yos. 10:15.]