Yosua 9

Yosua 9

Wagibeoni wanajipatia kwa ujanja urafiki wa Waisiraeli.

1Walipoyasikia hayo wafalme wote waliokaa ng'ambo ya huku ya Yordani milimani na katika nchi ya tambarare na huko pwani po pote penye Bahari Kubwa panapoelekea Libanoni. Wahiti na Waamori na Wakanaani na Waperizi na Wahiwi na Wayebusi,

2wakakusanyika pamoja kwenda kupigana na Yosua nao Waisiraeli, mioyo yao ikawa kama mmoja.

3Wenyeji wa Gibeoni walipoyasikia, Yosua aliyoutendea Yeriko na Ai,[#Yos. 6:20-21; 8:26,28.]

4wao wakatumia ujanja, wakajifanya kuwa wajumbe, wakawatandika punda wao magunia machakavu, wakachukua viriba vichakavu vya mvinyo vilivyotiwa viraka kwa kupasukapasuka.

5Miguuni wakavaa viatu vichakavu vilivyoshonwashonwa, miilini wakavaa nguo chakavu, nayo mikate yote ya pamba zao za njiani ilikuwa mikavu yenye ukungu.

6Kisha wakaenda Gilgali makambini kwake Yosua, wakamwambia yeye, nao Waisiraeli: Tumetoka nchi ya mbali, sasa fanyeni maagano nasi!

7Waisiraeli walipowaambia hao Wahiwi: Labda ninyi mnakaa katikati yetu, kwa hiyo tutawezaje kufanya maagano nanyi?[#2 Mose 23:32; Yos. 11:19.]

8wao wakamwambia Yosua: Sisi tu watumwa wako, naye Yosua akawauliza: Ninyi m wa nani? Tena mmetoka wapi?

9Wakamwambia: Watumwa wako wametoka nchi iliyo mbali sana kwa ajili ya Jina la Bwana Mungu wako, kwani tumeusikia uvumi wake nayo yote, aliyoyafanya huko Misri,

10nayo yote, aliyowafanyia wale wafalme wawili wa Waamori waliokuwako ng'ambo ya huko ya Yordani, yule Sihoni, mfalme wa Hesiboni, na Ogi, mfalme wa Basani, aliyekaa Astaroti.[#4 Mose 21:21-35.]

11Kwa hiyo wazee wetu na wenyeji wote wa nchi yetu wakatuambia kwamba: Chukueni mikononi mwenu pamba za njiani, mwende kukutana nao, mwaambie: Sisi tu watumwa wenu, sasa fanyeni maagano nasi!

12Hii mikate yetu ilikuwa yenye moto, tulipoichukua nyumbani mwetu kuwa pamba zetu siku hiyo, tulipotoka kwetu kwenda kwenu; sasa itazame, ni mikavu yenye ukungu!

13Hivi viriba vya mvinyo navyo vilikuwa vipya, tulipovijaza, sasa vitazame, vimepasukapasuka. Hizi nguo zetu nazo zimechakaa pamoja na viatu, kwa kuwa njia ni ya mbali sana.

14Ndipo, wale watu wa Kiisiraeli walipoonja pamba zao, lakini kinywa cha Bwana hawakukiuliza.[#4 Mose 27:21.]

15Kisha Yosua akapatana nao kufanya maagano, asiwaue, nao wakuu wa mkutano wakawaapia hivyo.[#Yos. 9:7.]

16Siku tatu zilipopita walipokwisha kufanya hayo maagano nao, wakasikia, ya kuwa wale wanakaa karibu katika nchi iyo hiyo, waliyoikaa wenyewe.

17Ndipo, wana wa Isiraeli walipoondoka, wakaingia siku ya tatu mjini kwao, nayo miji yao ilikuwa Gibeoni na Kefira na Beroti na Kiriati-Yearimu.

18Lakini wana wa Isiraeli hawakuwaua, kwa kuwa wakuu wa mkutano waliwaapia na kumtaja Bwana Mungu wa Isiraeli. Wao wa mkutano wote walipowanung'unikia wakuu,

19wakuu wote wakauambia mkutano wote: Sisi tumewaapia na kumtaja Bwana Mungu wa Isiraeli, kwa hiyo sasa hatuwezi kuwagusa.

20Lakini nao tuwafanyie hivyo: tuache kuwaua, makali yasitujie kwa ajili ya hicho kiapo, tulichowaapia.[#2 Sam. 21:1-2.]

21Kwa hiyo wakuu wakawaambia: Na wakae uzimani! Lakini watakuwa wachanja kuni na wachota maji yao wote wa mkutano huu, kama wakuu walivyowaambia.

22Kisha Yosua akawaita, akawaambia kwamba: Mbona mmetudanganya na kutuambia: Sisi tunawakalia mbali sana? Nanyi mnakaa huku kwetu katikati!

23Sasa mtakuwa mmeapizwa, kwenu wasikoseke watumwa wa kuchanja kuni na wa kuchota maji yao walio mlango wa Mungu wangu!

24Nao wakamjibu Yosua wakisema: Watumwa wako walipashwa habari za kwamba: Bwana Mungu wako alimwagiza mtumishi wake Mose kuwapa ninyi nchi hii yote nzima, mwangamize wenyeji wote wa nchi hii, watoweke mbele yenu. Kwa hiyo tukaingiwa na oga mwingi rohoni mwetu wa kuwaogopa ninyi, kwa hiyo tukalifanya jambo lile.

25Sasa tazama, tumo mkononi mwako! Utakapoyaona kuwa mema yanyokayo, basi, tufanyizie kabisa!

26Kisha akawafanyizia hayo, akawaponya mikononi mwao wana wa Isiraeli, wasiwaue.

27Ndivyo, Yosua alivyowaweka siku hiyo kuwa wachanja kuni na wachota maji wa mkutano na wa mahali hapo pa kutambikia, Bwana atakapopachagua; vikawa hivyo mpaka siku hii ya leo.[#5 Mose 29:11.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania