Maombolezo 2

Maombolezo 2

Kuyalilia mabomoko ya Yerusalemu na ya Yuda.

1Kumbe Bwana kwa makali yake anamkalisha binti Sioni chini! Utukufu wa Isiraeli uliofika hata mbinguni ameubwaga chini, alipokasirika hakukumbuka, ya kuwa ni pake pa kuiwekea miguu yake.[#1 Mambo 28:2.]

2Bwana ameyameza makao yote ya Yakobo pasipo kuyaonea uchungu, kwa machafuko yake akayabomoa maboma ya binti Yuda, mfalme nao wakuu wake akawakumba, waanguke, kisha akawachafua.

3Makali yake yalipowaka moto, ndipo, alipokata pembe zote za Isiraeli, akaurudisha nyuma mkono wake wa kuume, uondoke usoni pa adui, akachoma moto kwake Yakobo, ukawa wenye miali iliyokula po pote.

4Akaupinda upindi wake, akawa kama adui,

akajipanga na kuutumia mkono wake wa kuume, kama mwenye

kusonga,

akawaua wote walipendeza macho;

hemani mwake binti Sioni ndimo, alimoyaeneza makali

yake kama moto.

5Bwana akawa kama adui, alipommeza Isiraeli,

akayameza majumba yake, akayaangamiza maboma yake,

akamfurikishia binti Yuda kupiga kite na kuugua.

6Akakivunja kitalu chake kama cha bustanini,

akauangamiza ua wake uliokuwa wa kukusanyikia;

kisha Bwana akawasahaulisha Wasioni sikukuu nazo za

mapumziko,

akamtupa mfalame na mtambikaji, makali yake

yalipowapatiliza.

7Pake pa kutambikiwa Bwana akapaona kuwa pabaya,

napo Patakatifu pake, akapaacha.

Akazitia mikononi mwa adui kuta za majumba yake,

wakapiga makelele Nyumbani mwa Bwana kama yale ya

sikukuu.

8Bwana amewaza moyoni kuziangamiza kuta za binti Sioni,

akapapitisha kamba ya kupimia, hakuurudisha mkono,

usipatoweshe,

akalisikitisha boma pamoja na kuta zake, sasa zinatia

uchungu.

9Malango yake yamezama, yamo mchangani ndani,

makomeo yake akayaharibu kwa kuyavunja.

Mfalme wake pamoja na wakuu wako kwa wamizimu,

huko hawasikii, Maonyo yakisomwa,

wala wafumbuaji wake hawafumbuliwi maono naye Bwana.

10Wazee wake binti Sioni hukaa chini na kunyamaza kimya,

hujitupia mavumbi vichwani na kujifunga magunia,

wanawali wa Yerusalemu huvielekeza vichwa vyao chini.

11Macho yangu yamezimia kwa kulia machozi,

matumbo yangu nayo huchafuka;

maini yangu yamemwagika chini

kwa ajili ya mavunjiko yao walio wazaliwa wa ukoo wangu,

kwani wachanga na wanyonyaji huzimia roho barabarani

mjini.

12Nao huwauliza mama zao: Mikate na mvinyo iko wapi?

wanapozimia barabarani mjini kama wenye kupigwa kwa

panga,

au wanapokata roho vifuani kwa mama zao.

13Nikutolee ushuhuda gani? Nikufananishe na nini, binti

Yerusalemu?

Nikulinganishe na nini, nikutulize moyo, mwanamwali binti

Sioni?

Kwani vunjiko lako ni kubwa kama bahari, atakayekuponya

ni nani?

14Wafumbuaji wako waliyoyaona yalikuwa uwongo na

upumbavu,

hawakuyafunua maovu yako, uliyoyafanya, wayafungue

mafungo yako,

ila walipokuambia: Tumeona, yalikuwa uwongo, wakupatie

kutekwa.

15Wote wapitao njiani wanakupigia makofi,

hukuzomea, binti Yerusalemu, wakivitingisha vichwa vyao,

kwamba: Je? Huu ni ule mji, watu waliouita:

Timilizo la uzuri, tena: Furaha ya nchi zote?

16Adui zako wote wakaviasama vinywa vyao, wakakuzomea wakikukerezea meno na kusema: Tumemmeza!

Hii ni siku, tuliyoingojea, tumeipata, tumeiona!

17Bwana ameyafanya aliyoyawaza, akalitimiza neno lake,

aliliagiza tangu siku za kale, akabomoa pasipo kuona

uchungu,

adui zako wakakufurahia, alipozikuza pembe zao

waliokusonga

18Mioyo yao ikamlilia Bwana: Ninyi kuta za binti Sioni,

churuzisheni machozi mchana na usiku kama ni mto!

Usijipatie pumziko! Mboni ya jicho lako isinyamaze!

19Inuka, ulie usiku kucha, zamu za usiku zikipokeana!

Umwage moyo wako, kama ni maji mbele ya uso wake Bwana!

Mnyoshee mikono yako kwa ajili ya roho za watoto wako

wachanga

wanaozimia kwa njaa po pote barabarani pembeni!

20E Bwana, tazama, uone! Ni nani, uliyemfanyizia hivyo?

Je? Wanawake wayale mazao yao, watoto wao waliolelewa

nao?

Je? Watambikaji na wafumbuaji wauawe Patakatifu pake

Bwana?

21Wana wa wazee hulala barabarani chini,

wasichana na wavulana wangu wameuawa kwa panga;

umewaua siku ile, makali yako yalipotokea,

ukawachinja pande zote pasipo kuwaonea uchungu!

22Ukawaita wote walionitia woga, watoke pande zote,

kama ni siku ya mkutano, lakini ilikuwa siku ya makali

ya Bwana,

napo hapo hawakuwako walioona pa kuponea wala pa

kukimbilia,

nao, niliowalea na kuwakuza, adui wakawamaliza.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania