The chat will start when you send the first message.
1Hapo, walipoukaribia Yerusalemu na kufika Beti-Fage mlimani pa michekele, ndipo, Yesu alipotuma wanafunzi wawili,
2akawaambia: Nendeni katika kijiji kinachowaelekea! Mara mtaona punda, amefungwa, hata mtoto wake yuko pamoja naye; mfungueni, mniletee!
3Kama mtu atawaambia neno, mwambieni: Bwana wetu anamtakia kazi! mara atawapani.[#Mat. 26:18.]
4Haya yote yamekuwapo, lipate kutimizwa neno la mfumbuaji la kwamba:
5Mwambieni binti Sioni: Tazama, mfalme wako anakujia,
ni mpoke, amepanda mwana punda aliye na mama yake,
mwenye kuchukua mizigo.
6Wanafunzi wakaenda, wakafanya, kama Yesu alivyowaagiza.
7Wakamleta punda na mwanawe, wakatandika nguo juu yao, kisha wakampandisha.
8Nayo makundi ya watu wengi sana wakatandika nguo zao njiani, wengine wakakata matawi ya miti, wakayatandika njiani,[#2 Fal. 9:13.]
9nao wale watu wengi waliomtangulia, nao waliomfuata wakapaza sauti wakisema:
Hosiana, mwana wa Dawidi!
Na atukuzwe ajaye kwa Jina la Bwana!
Hosiana juu mbinguni!*
10Alipoingia Yerusalemu, mji wote ukatukutika, wakisema: Nani huyu?
11Makundi ya watu wakasema: Huyu ndiye mfumbuaji Yesu wa Nasareti wa Galilea.
12Yesu akapaingia Patakatifu, akawafukuza wote wenye kuuzia na kununulia hapo Patakatifu, akaziangusha meza za wavunja fedha na viti vya wachuuzi wa njiwa,[#Yoh. 2:14-16.]
13akawaambia: Imeandikwa: Nyumba yangu itaitwa nyumba ya kuombea, lakini ninyi mnaigeuza kuwa pango la wanyang'anyi.[#Yes. 56:7; Yer. 7:11.]
14Kisha wakamwendea hapo Patakatifu vipofu na viwete, naye akawaponya.
15Lakini watambikaji wakuu na waandishi walipoyaona mataajabu, aliyoyafanya, tena waliposikia, watoto wakipaza sauti hapo Patakatifu na kusema: Hosiana, mwana wa Dawidi! ndipo, walipokasirika,[#Sh. 118:25.]
16wakamwambia: Unasikia, hawa wanavyosema? Yesu akawaambia: Ndio. Hamjalisoma bado neno lile la kwamba:
Vinywani mwao watoto wachanga
namo mwao wanyonyao ulitengeneza tukuzo?
17Kisha akawaacha, akatoka mjini, akaenda Betania, akalala huko.
18Asubuhi alipokuwa akirudi mjini akaona njaa.[#Luk. 13:6.]
19Alipoona mkuyu kando ya njia akauendea, asione kitu kwake, ila majani matupu, akauambia: Kale na kale lisipatikane tena tunda kwako! Mara mkuyu ukawa umenyauka.
20Wanafunzi walipoviona wakastaajabu, wakasema: Mkuyu huu umenyaukaje mara?
21Yesu akajibu akiwaambia: Kweli nawaambiani: Mkimtegemea Mungu pasipo mashaka hamtafanya kama hili tu la huu mkuyu, ila hata mkiuambia mlima huu: Ondoka hapa, ulipo, ujitupe baharini! basi itatendeka.[#Mat. 17:20.]
22Nayo yo yote, mtakayoyaomba katika maombo, mtayapata mkiwa mnamtegemea Mungu.[#Yoh. 14:13.]
23Alipokwisha ingia Patakatifu, akiwa akifundisha, wakamjia watambikaji wakuu na wazee wa huku kwao, wakamwuliza: Hayo unayafanya kwa nguvu gani?[#Mat. 7:29; Yoh. 2:18.]
24Tena ni nani aliyekupa nguvu hii? Yesu akajibu akiwaambia: Hata mimi nitawauliza neno moja; mtakaponijibu neno hilo, basi, hata mimi nitawaelezea nguvu yangu ya kuyafanya hayo.
25Ubatizo wake Yohana ulikuwa umetoka wapi? Mbinguni au kwa watu? Nao wakafikiri mioyoni mwao kwamba: Tukisema: Ulitoka mbinguni, atatuuliza: Mbona hamkumtegemea?
26Lakini tukisema: Ulitoka kwa watu, tunawaogopa watu; kwani wote wanamshika Yohana kuwa mfumbuaji.[#Mat. 14:5.]
27Kwa hiyo wakamjibu Yesu wakisema: Hatujui. Ndipo, alipowaambia: Basi, hata mimi siwaambii nguvu inayonifanyisha hayo.
28*Lakini mwaonaje? Kulikuwa na mtu mwenye wana wawili. Akamwendea mkubwa, akasema: Mwanangu, nenda leo kufanya kazi mizabibuni!
29Akamjibu, akasema: Sitaki; lakini halafu alijuta akaenda.
30Alipomwendea wa pili na kumwambia yaleyale, yeye akajibu akisema: Ndio, bwana; lakini hakuenda.[#Mat. 7:21.]
31Katika hao wawili aliyeyafanya, baba aliyoyataka, ni yupi? Wakasema: Ni wa kwanza. Yesu akawaambia: Kweli nawaambiani: Watoza kodi na wenye ugoni watawatangulia ninyi kuingia katika ufalme wa Mungu.[#Luk. 18:14.]
32Kwani Yohana alikuja kwenu, akafuata njia yenye wongofu, nanyi hamkumtegemea, lakini watoza kodi na wenye ugoni walimtegemea. Lakini ninyi mlipoviona, hata hapo hamkujuta na kumtegemea.*[#Luk. 7:29.]
33Sikilizeni mfano mwingine! Kulikuwa na mtu mwenye nyumba aliyepanda mizabibu, akaizungusha ugo, akachimbua humo kamulio la kuzikamulia zabibu, akajenga dungu, akaipangisha wakulima, kisha akaenda katika nchi nyingine.[#Mat. 25:14; Yes. 5:1-2.]
34Siku za kuiva zabibu zilipotimia, akatuma watumwa wake kwa wale wakulima, wapewe zabibu zake.
35Nao wakulima wakawakamata watumwa wake, mmoja wakampiga, mmoja wakamwua, mmoja wakamtupia mawe.
36Akatuma tena watumwa wengine walio wengi kuliko wa kwanza. Wakawatendea vilevile.
37Mwisho akamtuma mwanawe kwao akisema: Watamcha mwanangu.
38Lakini wakulima walipomwona mwanawe wakasemezana wao kwa wao: Huyu ndiye kibwana, njoni, tumwue, tuupate urithi wake![#Mat. 27:18; Yoh. 1:11.]
39Kwa kiyo wakamkamata, wakamsukuma sukuma mpaka nje ya mizabibu, wakamwua.
40Basi, mwenye mizabibu atakapokuja wakulima wale atawafanyia nini?
41Wakamwambia: Hao wabaya atawaangamiza vibaya, nayo mizabibu atawapangisha wakulima wengine watakaompa zabibu zake, zitakapoiva.
42*Yesu akawaambia: Hamjasoma katika Maandiko ya kuwa:
Jiwe, walilolikataa waashi, hilihili limekuwa la pembeni?
Hivyo vimefanywa na Bwana; nasi tukivitazama, ni vya kustaajabu.
43Kwa sababu hiyo nawaambiani: Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu
taifa jingine litakalozaa matunda yake liupate.
44Naye atakayeanguka juu ya jiwe hilo atapondeka, naye litakayemwangukia, litambana tikitiki*.[#Dan. 2:34-35,44-45.]
45Watambiakaji wakuu na Mafariseo walipoisikia mifano yake wakatambua, ya kuwa anawasema wao.
46Kwa hiyo wakatafuta kumkamata, lakini waliwaogopa makundi ya watu, kwani walimwona kuwa mfumbuaji.