The chat will start when you send the first message.
1Bwana akamwambia Mose kwamba:
2Sema na wana wa Isiraeli, uwaambie: Mtakapoingia katika nchi yenu ya kukaa, ninayotaka kuwapa,
3hapo mtakapomtolea Bwana ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima au za kuchinjwa, kama ni za kuyalipa, mtu aliyoyaapa, au kama ni za kupenda kwa moyo tu, au kama ni za sikukuu zenu, amtengenezee Bwana mnuko wa kumpendeza, kama anatoa ng'ombe au mbuzi au kondoo,
4basi, huyo mwenye kumtoa na ampelekee Bwana toleo lake pamoja na kilaji cha tambiko, nacho kiwe vibaba vitatu vya unga mwembamba wa ngano uliochanganywa na kibaba kimoja cha mafuta,[#3 Mose 6:14.]
5tena kibaba kimoja cha mvinyo kuwa kinywaji cha tambiko, kama ni cha ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima, au kama ni ya kuchinjwa, nacho kiwe hivyo cha kila mwana kondoo mmoja.[#4 Mose 28:14.]
6lakini kama ni dume la kondoo, utengeneze kilaji chake cha tambiko kuwa vibaba sita vya unga mwembamba wa ngano uliochanganywa na kibaba kimoja na nusu cha mafuta.
7Nacho kinywaji chake cha tambiko kiwe kibaba kimoja na nusu cha mvinyo; ukimtolea Bwana hivi, vitakuwa mnuko wa kumpendeza.
8Lakini kama utatengeneza ndama kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima au ya kuchinjwa ya kuyalipa, aliyoyaapa, au ya kumshukuru Bwana,
9utoe pamoja na ndama kilaji cha tambiko cha vibaba tisa vya unga mwembamba wa ngano uliochanganywa na vibaba viwili vya mafuta.
10Tena utoe vibaba viwili vya mvinyo kuwa kinywaji cha tambiko; ukivichoma moto vitakuwa mnuko wa kumpendeza Bwana.
11Hivi uvitengenezee kila ng'ombe mmoja au kila dume moja la kondoo au kila mwana kondoo au kila mwana mbuzi.
12Kwa hesabu yao hao, mtakaowatengeneza, kwa hesabu iyo hiyo sharti mmtengenezee kila mmoja kilaji na kinywaji chake cha tambiko.
13Kila mwenyeji sharti avitengeneze vivyo hivyo akitaka kumtolea Bwana ng'ombe ya tambiko kuwa mnuko wa moto wa kumpendeza.
14Kama kwenu yuko mgeni au mwingine anayekaa siku zote kwao walio vizazi vyenu, naye akitaka kumtengenezea Bwana ng'ombe ya tambiko kuwa mnuko wa moto wa kumpendeza, na aitengeneze vivyo hivyo, kama ninyi mnavyoitengeneza.
15Maongozi yawe yayo hayo ya mkutano wote, kama ni ninyi wenyewe au kama ni mgeni akaaye ugenini kwenu; maongozi haya yawe ya kale na kale ya kuviongoza vizazi vyenu; kama ninyi mlivyo mbele ya Bwana, ndivyo, naye mgeni atakavyokuwa mbele yake.[#2 Mose 12:49.]
16Nayo maonyo na maamuzi yawe yayo hayo ya ninyi wenyewe na ya mgeni atakayekaa ugenini kwenu.
17Bwana akamwambia Mose kwamba:
18Sema na wana wa Isiraeli, uwaambie: Mtakapoingia katika nchi ile, mimi nitakakowaingiza,
19mtakapokula mikate ya nchi hiyo, sharti mmtolee Bwana vipaji vya tambiko vya kunyanyuliwa.[#2 Mose 23:16,19.]
20Mlimbuko wa unga wenu wa chengachenga uwe andazi, mtakalolitoa kuwa kipaji cha tambiko cha kunyanyuliwa, nacho mkitoe vivyo hivyo, kama mnavyokitoa kipaji cha tambiko cha kunyanyuliwa kitokacho penye kupuria ngano.[#5 Mose 26:1-2.]
21Hivyo ndivyo, mtakavyompa Bwana malimbuko ya unga wenu wa chengachenga kuwa vipaji vya tambiko vya kunyanyuliwa.
22Ikiwa kwa kupotelewa, msiyafanye hayo maagizo yote, Bwana aliyomwambia Mose,[#3 Mose 4:2,13.]
23nayo hayo yote, Bwana aliyowaagiza ninyi kinywani mwa Mose tangu siku ile, Bwana alipoanza kuwaagiza maneno, nayo aliyoyaagiza baadaye kwa vizazi na vizazi,
24kama ni makosa yaliyofanyika kwa kupotelewa tu, ikiwa wao wa mkutano hawakuyaona, basi, mkutano wote na utengeneze dume moja la ng'ombe aliye kijana bado kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima kuwa mnuko wa kumpendeza Bwana; waitoe pamoja na kilaji na kinywaji chake cha tambiko, kama ilivyo desturi, tena watoe dume moja la mbuzi kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo.
25Naye mtambikaji na aupatie upozi mkutano wote wa wana wa Isiraeli, waondolewe hayo makosa, kwani walipotelewa tu. Nao wenyewe na wayapeleke matoleo yao kuwa ng'ombe za tambiko za Bwana za kuteketezwa, nazo ng'ombe za tambiko za weuo wao na wamtolee Bwana usoni pake kwa ajili ya kupotelewa kwao.
26Hivyo ndivyo, wao wa mkutano wote wa wana wa Isiraeli pamoja na wageni watakaokaa ugenini kwao watakavyoondolewa makosa, kwa kuwa watu wote walikuwa wamepotelewa.
27Kama mtu mmoja anakosa kwa kupotelewa, na atoe mbuzi jike wa mwaka mmoja kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo.[#3 Mose 4:27-28.]
28Naye mtambikaji na ampatie upozi mtu huyo aliyepotelewa, akitoa mbele ya Bwana ng'ombe ya tambiko ya kumweua kwa ajili ya kupotelewa kwake; akimpatia upozi hivyo, ataondolewa kosa lake.
29Kama ni mwenyeji wa wana wa Isiraeli, au kama ni mgeni atakayekaa ugenini kwenu, maongozi yawe yayo hayo ya kuwafanyizia waliokosa kwa kupotelewa.
30Lakini mtu akikosa kwa kusudi, kama ni mwenyeji, au kama ni mgeni, huyo anamtukana Bwana, kwa hiyo mtu aliye hivyo sharti ang'olewe katikati yao walio ukoo wake,[#Tume. 13:38; Ebr. 10:26-27.]
31kwani amelibeza Neno la Bwana na kuyavunja maagizo yake. Mtu aliye hivyo hana budi kung'olewa kabisa na kutwikwa manza, alizozikora.
32Wana wa Isiraeli walipokuwa nyikani waliona mtu, akiokota kuni siku ya mapumziko.[#2 Mose 20:8.]
33Waliomwona, alivyookota kuni, wakampeleka kwa Mose na Haroni na kwa mkutano wote.
34Wakamweka kifungoni, kwani haijaelekea bado, mtu kama huyu atakayofanyiziwa.[#3 Mose 24:12; 2 Mose 31:14; 35:2.]
35Bwana akamwambia Mose: Mtu huyu hana budi kuuawa, wao wote wa mkutano na wampige mawe nje ya makambi.
36Ndipo, wao wote wa mkutano walipomtoa na kumpeleka nje ya makambi, wakampiga mawe, hata akafa, kama Bwana alivyomwagiza Mose.
37Bwana akmwambia Mose kwamba:
38Sema na wana wa Isiraeli, uwaambie, wajifanyizie vishada penye ncha za mavazi yao, wao na vizazi vyao, kisha juu ya hivyo vishada watie nyuzi za rangi za nguo za kifalme.[#5 Mose 22:12; Mat. 23:5.]
39Maana ya hivyo vishada vyenu ni hii: mtakapoviona, myakumbuke maagizo yote ya Bwana, myafanye, msizifuate tamaa za mioyo yenu na za macho yenu, kwani mkizifuata hufanya ugoni.
40Kwa hiyo yakumbukeni maagizo yangu na kuyafanya, mpate kuwa watakatifu wa Mungu wenu.
41Mimi Bwana ni Mungu wenu aliyewatoa ninyi katika nchi ya Misri, niwe Mungu wenu; kweli mimi Bwana ni Mungu wenu.