4 Mose 16

4 Mose 16

Upingani wa Kora na wa wenzake.

1Kora, mwana wa Isihari, mwana wa Kehati, mwana wa Lawi, akachukua watu, yeye na Datani na Abiramu, wana wa Eliabu, na Oni, mwana wa Peleti, waliokuwa wana wa Rubeni.[#2 Mose 6:18,21; 4 Mose 26:9; Yuda 11.]

2Hawa wakamwinukia Mose pamoja na wana wa Isiraeli 250 waliokuwa wakuu mashaurini na wateule wa mkutano wenye jina kuu.[#4 Mose 12:1-2.]

3Wakakusanyika kutetana na Mose na Haroni, wakawaambia: Maneno yenu ni mengi, kwani wao wote wa mkutano wetu mzima ni watakatifu, naye Bwana yuko katikati yao. Mbona mnajikweza kuwa wakuu wao wa mkutano wa Bwana?

4Mose alipoyasikia akaanguka kifudifudi,[#4 Mose 14:5.]

5akamwambia Kora nao wenzake wote, aliowakusanya, kwamba: Kesho Bwana atamjulisha aliye wake naye aliye mtakatifu akimfikisha kwake; kwani atakayemchagua atamfikisha kwake.[#2 Tim. 2:19.]

6Fanyeni haya: jichukulieni vyetezo, wewe Kora na wenzako wote, uliowakusanya!

7Tieni moto humo, kisha wekeni kesho mavukizo juu yao mbele ya Bwana! Naye mtu, Bwana atakayemchagua, na awe mtakatifu. Maneno yenu ni mengi, ninyi wana wa Lawi.

8Kisha Mose akamwambia Kora: Sikieni, ninyi wana wa Lawi!

9Je? Ni kidogo kwenu, Mungu wa Isiraeli akiwatenga ninyi kwao wa mkutano wa Waisiraeli na kuwafikisha kwake, mwutumikie utumishi wa Kao lake Bwana na kusimama mbele ya mkutano kwa kuutumikia?[#4 Mose 3:6-13; 4:4-20.]

10Wewe na ndugu zako wote walio wana wa Lawi amewafikisha kwake pamoja na wewe, tena mnautafutiaje utambikaji nao?

11Kweli wewe pamoja na wenzako wote mnafanya shauri la kumpingia Bwana, kwani Haroni ni nani, mkimnung'unikia?[#2 Mose 16:7.]

12Kisha Mose akatuma kumwita Datani na Abiramu, wana wa Eliabu, lakini wakasema: Hatuji.

13Ni kidogo, ukitutoa katika nchi ichuruzikayo maziwa na asali, utuue huku nyikani? Unajikuzaje tena kuwa mkuu wa kututawala?

14Kweli umetuingiza katika nchi ichuruzikayo maziwa na asali! Kweli umetugawia mashamba na mizabibu kuwa yetu! Watu hawa unataka kuwachoma macho? Hatuji.[#2 Mose 3:8,17.]

15Ndipo, Mose alipokasirika sana, akamwambia Bwana: Usigeuke kuvitazama vilaji vyao vya tambiko! Sikuchukua kwao hata punda mmoja tu, wala mtu wa kwao sikumfanyizia mabaya hata mmoja tu.[#1 Sam. 12:3; Tume. 20:33.]

16Kisha Mose akamwambia Kora: Wewe na wenzako wote, uliowakusanya, sharti mwe kesho mbele ya Bwana, wewe nao wale na Haroni.

17Mchukue kila mmoja chetezo chake, mtie humo mavukizo, kisha mmtokee Bwana kila mmoja na chetezo chake, vyote viwe vyetezo 250, wewe nawe na Haroni, kila na chake chetezo.

18Wakachukua kila mtu chetezo chake, wakatia moto humo, juu ya moto wakaweka mavukizo, wakaja kusimama hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano, hata Mose na Haroni walikuwako.

19Lakini Kora alikuwa aliwakusanya hao wa mkutano wote hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano; ndipo, utukufu wa Bwana ulipoutokea huo mkutano wote.[#4 Mose 14:10.]

20Naye Bwana akamwambia Mose na Haroni kwamba:

21Jitengeni na kutoka katikati yao wa mkutano huu! Kwani nitawamaliza kwa mara moja.

22Wakaanguka kifudifudi, wakasema: Mungu uliye Mungu wa roho zao wote walio wenye miili, mtu mmoja akikosa, utawachafukia wote wa mkutano huu?

23Ndipo, Bwana alipomwambia Mose kwamba:

24Waambie wao wa mkutano huu kwamba: Epukeni kabisa po pote panapoyazunguka makao ya Kora na ya Datani na ya Abiramu!

25Kisha Mose akainuka, akaenda kwao Datani na Abiramu, nao wazee wa Waisiraeli wakamfuata.

26Akasema nao wa mkutano kwamba: Ondokeni penye mahema ya watu hawa wasiomcha Mungu! Wala msiguse cho chote kilicho chao, msiangamizwe kwa ajili ya makosa yao yote.

27Ndipo, walipoepuka po pote palipoyazunguka makao ya Kora na ya Datani na ya Abiramu, lakini Datani na Abiramu wakatoka, wakasimama hapo pa kuyaingilia mahema yao pamoja na wake zao na wana wao na watoto wao wachanga.

28Kisha Mose akasema: Hivi ndivyo, mtakavyotambua, kama Bwana alinituma, niyafanye hayo matendo yote, au kama ni moyo wangu ulionituma:

29watu hawa watakapokufa, kama watu wote wanavyokufa, au watakapopatwa na mambo, watu wote wanayopatwa nayo, Bwana hakunituma.

30Lakini Bwana akiumba jambo jipya, nchi ikiasama na kuwameza wao pamoja navyo vyote vilivyo vyao, washuke kuzimuni wakiwa wazima, ndipo, mtakapotambua, ya kuwa watu hao wamemtukana Bwana.

31Ikawa, alipokwisha kuyasema maneno haya, ndipo, nchi ilipoatuka chini yao,[#5 Mose 11:6.]

32maana nchi ikaasama, ikawameza wao pamoja na nyumba zao, nao watu wote waliokuwa upande wa Kora, nazo mali zao zote.

33Ndivyo, walivyoshuka kuzimuni pamoja navyo vyote vilivyokuwa vyao wakiwa wazima, kisha nchi ikawafunika, wakawa wametoweka katikati yao wa mkutano huu.

34Nao Waisiraeli wote waliosimama hapo na kuwazunguka wakakimbia kwa makelele yao, kwani walisema: Nchi isitumeze na sisi!

35Kisha moto ukatoka kwake Bwana, ukawala wale watu 250, walipokuwa wanavukiza.[#3 Mose 10:1-2; Sh. 106:18.]

Vyetezo vyao wenzake Kora navyo vya Haroni.

36Bwana akamwambia Mose kwamba:

37Mwambie Elazari, mwana wa mtambikaji Haroni, aviokote vyetezo hapo, wale walipoteketezwa, kwani ni vitakatifu; nayo makaa ya moto uyamwage huko na huko.

38Kisha hivyo vyetezo vya hao wakosaji waliojipatia kufa wenyewe vitengenezeni kuwa mabati mapana ya kuifunikiza meza ya kutambikia. Kwa kuwa walivitokeza mbele ya Bwana, ni vitakatifu, navyo sharti viwe kielekezo kwao wana wa Isiraeli.

39Naye mtambikaji Elazari akavichukua hivyo vyetezo vya shaba, wao walioteketea walivyovitokeza mbele ya Bwana, wakavisana, viwe kifuniko cha meza ya kutambikia.

40Hivyo vikawa ukumbusho wa wana wa Isiraeli, kwa kwamba mtu mgeni asiye wa uzao wa Haroni, asije kuvukiza mavukizo mbele ya Bwana, asipatwe na mambo kama Kora na wenzake, aliowakusanya, maana Bwana alivyomwambia kinywani mwa Mose yalimpata.

Mapatilizo yao walionung'unikia kufa kwao wa Kora.

41Kesho yake wao wote wa mkutano wa wana wa Isiraeli wakamnung'unikia Mose na Haroni kwamba: Mmewaua watu wa Mungu.

42Ikawa, huo mkutano ulipokusanyika kutetana na Mose na Haroni, nao hao walipoligeukia Hema la Mkutano, mara lile wingu likalifunika, nao utukufu wa Bwana ukatokea.[#4 Mose 14:10.]

43Mose na Haroni walipokwenda kufika hapo mbele ya Hema la Mkutano,

44Bwana akamwambia Mose kwamba:

45Jiepusheni katikati ya mkutano huu, niwamalize kwa mara moja! Ndipo, walipoanguka kifudifudi,[#4 Mose 16:4,22.]

46naye Mose akamwambia Haroni: Chukua chetezo, utie humo moto wa mezani pa kutambikia, kisha weka mavukizo juu yake, uende upesi kwenye mkutano, uwapatie upozi, kwani makali yamekwisha kutoka kwake Bwana, nalo pigo limekwisha kuwaanzia.[#2 Mose 28:38; 3 Mose 16:13.]

47Haroni akachukua chetezo, kama Mose alivyosema, akapiga mbio kufika katikati ya mkutano, akaona, ya kuwa pigo limeanza kweli kupiga watu; ndipo, alipotia mavukizo juu ya moto, awapatie watu upozi.

48Aliposimama katikati yao waliokufa nao walio wazima bado, hilo pigo likakomeshwa.

49Nao waliouawa na hilo pigo walikuwa watu 14700, wasipohesabiwa waliokufa kwa ajili ya Kora.

50Kisha Haroni akarudi kwa Mose hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano, hilo pigo lilipokuwa limekomeshwa.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania