The chat will start when you send the first message.
1Bwana akamwambia Mose na Haroni kwamba:[#4 Mose 1.]
2Wana wa Isiraeli na wapige makambi yao kila mtu penye bendera yake, vielekezo vya mlango wa baba zao vilipo; nayo makambi, watakayoyapiga, sharti yalielekee Hema la Mkutano na kulizunguka.
3Watakaopiga makambi upande wa mashariki wa maawioni kwa jua ndio hawa: bendera ya makambi ya vikosi vyake Yuda iwe huko kwa mkuu wa wana wa Yuda. Nasoni, mwana wa Aminadabu;
4vikosi vyake jumla yao ni watu 74600.
5Watakaopiga makambi kando yake ndio wao wa shina la Isakari, naye mkuu wa wana wa Isakari ni Netaneli, mwana wa Suari.
6Vikosi vyake jumla yao ni watu 54400.
7Tena wao wa shina la Zebuluni, naye mkuu wa wana wa Zebuluni ni Eliabu, mwana wa Heloni.
8Vikosi vyake jumla yao ni watu 57400.
9Jumla yao wote watakaokuwa makambini kwa Yuda ni watu 186400 kwa vikosi vyao, nao ndio wa kwanza watakaoondoka.
10Upande wa kusini itakuwako bendera ya makambi ya vikosi vya Rubeni, naye mkuu wa wana wa Rubeni ni Elisuri, mwana wa Sedeuri.
11Vikosi vyake jumla yao ni watu 46500.
12Watakaopiga makambi kando yake ndio wao wa shina la Simeoni, naye mkuu wao wana wa Simeoni ni Selumieli, mwana wa Surisadai.
13Vikosi vyake jumla yao ni watu 59300.
14Tena wao wa shina la Gadi, naye mkuu wa wana wa Gadi ni Eliasafu, mwana wa Reueli.
15Vikosi vyake jumla yao ni watu 45650.
16Jumla yao wote watakaokuwa makambini kwa Rubeni ni watu 151450 kwa vikosi vyao, nao ndio wa pili watakaoondoka.
17Kisha Hema la Mkutano na liondoke pamoja nao wakaao makambini kwa Walawi, liwe katikati ya makambi; kama walivyopanga makambini ndivyo waondoke kwenda kusafiri, kila mtu mahali pake penye bendera ya kwao.
18Upande wa baharini itakuwako bendera ya makambi ya vikosi vya Efuraimu, naye mkuu wa wana wa Efuraimu ni Elisama, mwana wa Amihudi.
19Vikosi vyake jumla yao ni watu 40500.
20Kando yake watakuwako wao wa shina la Manase, naye mkuu wa wana wa Manase ni Gamulieli, mwana wa Pedasuri.
21Vikosi vyake jumla yao ni watu 32200.
22Tena wao wa shina la Benyamini, naye mkuu wa wana wa Benyamini ni Abidani, mwana wa Gideoni.
23Vikosi vyake jumla yao ni watu 35400.
24Jumla yao wote watakaokuwa makambini kwa Efuraimu ni watu 108100 kwa vikosi vyao, nao ndio wa tatu watakaoondoka.
25Upande wa kaskazini itakuwako bendera ya makambi ya vikosi vya Dani, naye mkuu wa wana wa Dani ni Ahiezeri, mwana wa Amisadai.
26Vikosi vyake jumla yao ni watu 62700.
27Watakaopiga makambi yao kando yake ni wao wa shina la Aseri, naye mkuu wa wana wa Aseri ni Pagieli, mwana wa Okrani.
28Vikosi vyake ni watu 41500.
29Tena wao wa shina la Nafutali, naye mkuu wa wana wa Nafutali ni Ahira, mwana wa Enani.
30Vikosi vyake jumala yao ni watu 53400.
31Jumla yao wote watakaokuwa makambini kwa Dani ni watu 157600, nao ndio wa mwisho watakaoondoka wakizifuata bendera zao.
32Hii ndiyo jumla yao wana wa Isiraeli wa milango ya baba zao. Wote waliohesabiwa makambini kwa vikosi vyao jumla yao walikuwa watu 603550.[#4 Mose 1:46.]
33Lakini Walawi hawakuhesabiwa kwao wana wa Isiraeli, kama Bwana alivyomwagiza Mose.[#4 Mose 1:48-49.]
34Wana wa Isiraeli wakayafanya yote; kama Bwana alivyomwagiza Mose, ndivyo, walivyoyapiga makambi yao penye bendera zao, tena ndivyo, walivyoondoka kwenda kusafiri kila mtu na ndugu zake penye milango ya baba zao.[#4 Mose 2:2.]