4 Mose 23

4 Mose 23

Mara mbili Mungu anavigeuza viapizo vya Bileamu kuwa mbaraka.

1Bileamu akamwambia Balaka: Nijengee hapa mahali saba pa kutambikia, kisha nipate hapa madume saba ya ng'ombe na madume saba ya kondoo.

2Balaka akafanya, kama Bileamu alivyosema, kisha Balaka na Bileamu wakatoa kila mahali pa kutambikia ng'ombe mmoja na kondoo mmoja.

3Naye Bileamu akamwambia Balaka: Simama penye ng'ombe yako ya tambiko! Lakini mimi nitakwenda, labda Bwana atakuja kunikuta; ndipo, nitakapokuambia hilo neno, atakalonionyesha. Kisha akaenda kilimani palipo peupe.

4Mungu alipokuja kweli kukutana na Bileamu njiani, huyu akamwambia: Nimetengeneza mahali saba pa kutambikia, nikatoa ng'ombe mmoja na kondoo mmoja kila mahali pamoja pa kutambikia.

5Naye Bwana akampa Bileamu maneno ya kuyasema kwa kinywa chake, kisha akamwambia: Rudi kwa Balaka, uyaseme maneno yayo hayo!

6Aliporudi kwake akamwona, akisimama penye ng'ombe yake ya tambiko, yeye na wakuu wote wa Moabu.

7Ndipo, alipoanza kusema maneno yake kwamba:

Huko Aramu ndiko, alikonichukua Balaka;

mfalme wa Moabu amenitoa milimani

upande wa maawioni kwa jua akisema:

Njoo, uniapizie Yakobo! Njoo, umchafukie Isiraeli!

8Lakini, Mungu asiyemwapiza nitamwapizaje?

Bwana asiyemchafukia nitamchafukiaje?

9Hapa juu miambani ninawaona,

hapa vilimani ninawachungulia;

ndio watu wakaao peke yao,

hawajiwazii kuwa sawa na wamizimu.

10Yuko nani awezaye kuyahesabu mavumbi yake Yakobo

au kujua tu hesabu ya fungu la nne la Isiraeli?

Kama hawa wanyofu wanavyokufa, ningetaka kufa hivyo,

ningependa, mwisho wangu uwe kama mwisho wao.

11Ndipo, Balaka alipomwambia Bileamu: Umenifanyizia nini? Nimekuchukua, uwaapize adui zangu, kumbe umewabariki!

12Akajibu kwamba: Hainipasi kuangalia, niyaseme yaleyale, Bwana aliyoyatia kinywani mwangu?[#4 Mose 22:38.]

13Ndipo, Balaka alipomwambia: Nenda pamoja na mimi mahali pengine, utakapowaona wote; sasa unaona mwisho wao tu, huwaoni wote; hapo ndipo, utakaponiapizia watu hawa.

14Kisha akamchukua, akampeleka juu mlimani kwa Pisiga kulikokuwa uwanda wa wachunguliaji. Huko nako akajenga mahali saba pa kutambikia, kisha akatoa kila mahali pa kutambikia ng'ombe mmoja na kondoo mmoja.

15Kisha Bileamu akamwambia Balaka: Simama hapa penye ng'ombe yako ya tambiko! Lakini mimi nitakwenda huko kumkuta Bwana.

16Naye Bwana akaja kweli kumkuta Bileamu, akampa maneno ya kuyasema kwa kinywa chake, kisha akamwambia: Rudi kwa Balaka, uyaseme maneno yayo hayo!

17Aliporudi kwake akamwona, akisimama penye ng'ombe yake ya tambiko pamoja na wakuu wote wa Moabu. Balaka alipomwuliza: Bwana amesema nini?

18akaanza kusema maneno yake kwamba:

Inuka, Balaka, usikie!

Nitegee sikio lako, mwana wa Sipori!

19Mungu si mtu, aseme uwongo,

si mwana wa mtu, ageuze moyo.

Yeye aseme neno, asilifanye?

Aweke agano, asilitimize?

20Tazameni! Nimepewa kubariki; napo,

alipobariki, siwezi kuyageuza.

21Hakuna aliyepata kutazama mambo

yaliyo ya bure kwake Yakobo,

wala hakuna aliyeona masumbuko kwake Isiraeli;

Bwana Mungu wake yuko pamoja naye,

nayo mashangilio ya mfalme husikilika kwao.

22Mungu ndiye aliyewatoa Misri,

naye anazo nguvu kama za nyati.

23Kweli hakuna uganga wa kumwangamiza Yakobo,

wala hakuna uaguaji wa kumponza Isiraeli,

siku zote Yakobo na Isiraeli huambiwa,

Mungu anayoyafanya.

24Na mwone, watu hawa wakiinuka kama simba mke,

wakijisimamisha kama simba mume!

Halali, mpaka ale nyama zao, aliowararua,

mpaka anywe damu zao, aliowaua.

25Ndipo, Balaka alipomwambia Bileamu: Usipoweza kuwaapiza, uache kuwabariki!

26Lakini Bileamu akamjibu Balaka kwamba: Sikukuambia kwamba: Yote, Bwana atakayoyasema, nitayafanya?[#4 Mose 23:12.]

27Ndipo, Balaka alipomwambia Bileamu: Njoo, nikupeleke mahali pengine, labda huko utanyoka machoni pake Mungu, ukiniapizia huko watu hawa.

28Kisha Balaka akamchukua Bileamu, akampeleka juu mlimani kwa Peori kunakoelekea jangwani.[#4 Mose 25:3.]

29Huko Bileamu akamwambia Balaka: Nijengee hapa mahali saba pa kutambikia! Kisha unipatie hapa madume saba ya ng'ombe na madume saba ya kondoo.[#4 Mose 23:1.]

30Balaka akafanya, kama Bileamu alivyosema, akatoa kila mahali pa kutambikia ng'ombe mmoja na kondoo mmoja.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania