The chat will start when you send the first message.
1Bwana akamwambia Mose na Haroni kwamba:
2Fanyeni hesabu ya wana wa Kehati na kuwatoa kwao wana wa Lawi walio wa udugu wao wa milango ya baba zao.
3Wao wa miaka thelathini na zaidi mpaka miaka hamsini ndio wanaofaa wote kuuingia utumishi huo, wafanye kazi za humo Hemani mwa Mkutano.[#4 Mose 8:24.]
4Nazo kazi za utumishi za wana wa Kehati za humo Hemani mwa Mkutano ziwe za Patakatifu Penyewe.
5Makambi yatakapovunjwa, Haroni na wanawe na waingie Hemani, walishushe lile guo kubwa la pazia, wafunike nalo Sanduku la Ushahidi.
6Kisha waweke juu yake blanketi la ngozi za pomboo, juu yake tena watandaze nguo nyeusi iliyo ya kifalme yote nzima, kisha na walitie mipiko yake.
7Hata meza yenye mikate ya kuwa usoni pa Bwana na waifunike kwa nguo nyeusi ya kifalme na kuweka juu yake vyano na vijiko na vikombe na madumu ya vinywaji vya tambiko, nayo mikate, wasiyokoma kumwekea Bwana, sharti iwe juu yake.
8Kisha na watandaze nguo nyekundu ya kifalme, kisha waifunike kwa blanketi la ngozi za pomboo, kisha na waitie mipiko yake.
9Kisha na wachukue nguo nyeusi ya kifalme, wakifunike kinara kiangazacho pamoja na taa zake na koleo zake na makato yake na vyombo vyake vyote vya mafuta, wanavyovitumia vya kazi yake.[#2 Mose 25:31.]
10Kisha na wakifunike pamoja na vyombo vyake vyote kwa blanketi la ngozi za pomboo, kisha na wakiweke juu ya miti ya kukichukulia.
11Kisha watandaze nguo nyeusi ya kifalme juu ya meza ya dhahabu ya kuvukizia, kisha waifunike kwa blanketi la ngozi za pomboo na kuitia mipiko yake.
12Kisha na wachukue vyombo vyote, wanavyovitumia Patakatifu, wavifunge katika nguo nyeusi ya kifalme na kuvifunika tena kwa blanketi la ngozi za pomboo, kisha waviweke juu ya miti ya kuvichukulia.
13Kisha na wazoe majivu mezani pa kuteketezea ng'ombe za tambiko, kisha watandaze juu yake nguo nyekundu ya kifalme.
14Kisha na waweke juu yake vyombo vyake vyote, wanavyovitumia wakifanya kazi za hapo, sinia na nyuma na majembe na vyano na vyombo vyote vya meza ya kuteketezea ng'ombe za tambiko, wavifunike juu kwa blanketi la ngozi za pomboo, kisha na waitie mipiko yake.
15Haroni na wanawe watakapokwisha kupafunika Patakatifu na vyombo vyake vyote wakitaka kuvunja makambi, ndipo, wana wa Kehati watakapoingia kuvichukua, lakini wasiguse vitu vitakatifu, wasife. Hii ndiyo mizigo yao wana wa Kehati, watakayoichukua Hemani mwa Mkutano.[#4 Mose 7:9; 2 Sam. 6:6-7.]
16Tena kazi yake Elazari, mwana wa mtambikaji Haroni, ni kuyaangalia mafuta ya kinara na mavukizo yanukayo vizuri na vilaji vya tambiko vya kila siku na mafuta ya kupaka, tena kuliangalia Kao lote zima na vyote vilivyomo ndani ya Patakatifu, maana ndivyo vyombo vyake.
17Bwana akamwambia Mose na Haroni kwamba:
18Angalieni, shina la udugu wa Wakehati lisitoweke kwao Walawi!
19Ila yafanyeni haya, wapate kuwapo, wasife, watakapopakaribia Patakatifu Penyewe: Kwanza Haroni na wanawe na waingie, kisha wawaweke kila mtu penye kazi yake na kumpa mzigo wake.
20Lakini wasiingie kamwe kupatazama tu Patakatifu, ijapo iwe kitambo kidogo kabisa, wsife.[#1 Sam. 6:19.]
21Bwana akamwambia Mose kwamba:
22Fanya hesabu ya wana wa Gersoni nao walio wa milango ya baba zao na wa udugu wao.
23Uwakague walio wenye miaka thelathini na zaidi mpaka miaka hamsini, ndio wanaofaa wote kuuingia utumishi, wafanye kazi za kutumikia Hemani mwa Mkutano.
24Hizi ndizo kazi zao walio wa udugu wa Gersoni za kutumika na za kuchukua mizigo:
25na wayachukue mazulia ya Kao, na Hema la Mkutano na chandalua chake na chandalua cha ngozi za pomboo kilichoko juu yake na pazia la hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano,
26na nguo za uani na pazia la hapo pa kuingia langoni kwa ua, unaolizunguka Kao na meza ya kuteketezea ng'ombe ya tambiko, na kamba zao na vyombo vyote vya utumishi wao, nayo yote yapasayo kufanywa nao na wayafanye.
27Utumishi wote wa wana wa Gersoni, kama ni kuichukua mizigo iwapasayo yote, au kama ni kuzifanya kazi ziwapasazo zote, ufanyike kwa kuagizwa na Haroni na wanawe; ninyi mwaweke kwa kuzignlia kazi za mizigo yao yote.
28Hizi ndizo kazi za utumishi wao walio wa udugu wa wana wa Gersoni wa kutumikia Hemani mwa Mkutano, naye atakayewaangalia ni Itamari, mwana wa mtambikaji Haroni.
29Uwakague nao wana wa Merari walio wa udugu wao wa milango ya baba zao:
30uwakague walio wa miaka thelathini na zaidi mpaka miaka hamsini, ndio wanaofaa wote kuuingia utumishi, wafanye kazi za kutumikia Hemani mwa Mkutano.
31Hizi ndizo kazi zao za kuiangalia mizigo yao, nao huo ndio utumishi wao wote wa kufanya Hemani mwa Mkutano: kuzichukua mbao za Kao na misunguo yake na nguzo zake na miguu yake,
32na nguzo zinazouzunguka au na miguu yao na mambo zao na kamba zao na vyombo vyao vyote, wafanye yote yaupasayo utumishi wao. Navyo vyombo vya kuviangalia, wakivichukua, mwape na kuvitaja kila kimoja jina lake.
33Hizi ndizo kazi za utumishi wao walio wa udugu wa wana wa Merari, wazifanye za kutumikia Hemani mwa Mkutano, naye mkuu wao awe Itamari, mwana wa mtambikaji Haroni.
34Kwa hiyo Mose na Haroni na wakuu wa mkutano wakawakagua wana wa Kehati walio wa udugu wao na wa milango ya baba zao;
35waliokuwa wenye miaka thelathini na zaidi mpaka miaka hamsini, ndio waliofaa wote kuuingia utumishi, wafanye kazi za kutumikia Hemani mwa Mkutano.
36Jumla yao walio wa udugu wao walikuwa watu 2750.
37Hii ndiyo jumla yao wote wa udugu wa Wakehati waliotumikia Hemani mwa Mkutano, Mose na Haroni waliowakagua kwa amri, Bwana aliyompa Mose.
38Wana wa Gersoni wakakaguliwa nao walio wa udugu wao na wa milango ya baba zao,
39waliokuwa wenye miaka thelathini na zaidi mpaka miaka hamsini, ndio waliofaa wote kuuingia utumishi, wafanye kazi za kutumikia Hemani mwa Mkutano.
40Jumla yao walio wa udugu wao na wa milango ya baba zao walikuwa watu 2630.
41Hii ndiyo jumla yao wote wa udugu wa wana wa Gersoni waliotumikia Hemani mwa Mkutano, Mose na Haroni waliowakagua kwa amri ya Bwana.
42Ndugu za wana wa Merari wakakagulia nao walio wa udugu wao na wa milango ya baba zao,
43waliokuwa wenye miaka thelathini na zaidi mpaka miaka hamsini, ndio waliofaa wote kuuingia utumishi, wafanye kazi za kutumikia Hemani mwa Mkutano.
44Jumla yao walio wa udugu wao walikuwa watu 3200.
45Hii ndiyo jumla yao walio wa udugu wa wana wa Merari, Mose na Haroni waliowakagua kwa amri, Bwana aliyompa Mose.
46Hawa ndio Walawi wote waliokaguliwa, Mose na Haroni na wakuu wa Waisiraeli waliowakagua, waliokuwa wa udugu wao na wa milango ya baba zao,
47ndio waliokuwa wenye miaka thelathini na zaidi mpaka miaka hamsini, nao ndio wote waliofaa kufanya kazi za kuutumikia huo utumishi nao utumishi wa kuchukua mizigo Hemani mwa Mkutano.
48Jumla yao walikuwa watu 8580.
49Kwa amri, Bwana aliyompa Mose, aliwakagua na kumweka kila mtu mmoja penye kazi yake ya utumishi na penye mzigo wake wa kuuchukua; nao wakawekwa vivyo hivyo, kama Bwana alivyomwagiza Mose.