4 Mose 9

4 Mose 9

Pasaka ya kwanza ya nyikani.

1Bwana akamwambia Mose nyikani kwa Sinai katika mwezi wa kwanza wa mwaka wa pili tangu hapo, walipotoka katika nchi ya Misri kwamba:

2Wana wa Isiraeli na waitengeneze kondoo ya Pasaka, siku zake zilizowekwa zitakapotimia.[#2 Mose 12.]

3Siku ya kumi na nne ya huu mwezi wakati wa jioni mwitengeneze saa zizo hizo zilizowekwa, myafuate maongozi yake yote na desturi zake zote zipasazo. Mwitengeneze vivyo hivyo.[#3 Mose 23:5.]

4Kwa hiyo Mose akawaambia wana wa Isiraeli, waitengeneze kondoo ya Pasaka.

5Nao wakaitengeneza kondoo ya Pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza wakati wa jioni kule nyikani kwa Sinai; yote, Bwana aliyomwagiza Mose, wana wa Isiraeli wakayafanya vivyo hivyo sawasawa.

Pasaka yao wenye uchafu nayo yao wasafiri.

6Wakawako watu waliokuwa wenye uchafu kwa ajili ya kufiwa; kwa hiyo hawakuweza kuitengeneza kondoo ya Pasaka siku hiyo, wakamtokea Mose na Haroni siku hiyo.[#4 Mose 19:11.]

7Hao watu wakawaambia: Sisi tu wenye uchafu kwa ajili ya kufiwa; mbona tunakatazwa kumtolea Bwana matoleo katikati ya wana wa Isiraeli siku hiyo iliyowekwa?

8Mose akawaambia: Ngojeni, nisikie, Bwana atakayoyaagiza kwa ajili yenu.

9Bwana akamwambia Mose kwamba:

10Waambie wana wa Isiraeli kwamba: Kila mtu wa kwenu au wa vizazi vyenu, kama ni mwenye uchafu kwa kufiwa au kama yuko mbali safarini, naye ataweza kuitengeneza kondoo ya Pasaka ya Bwana.

11Na aitengeneze siku ya kumi na nne ya mwezi wa pili wakati wa jioni, tena na waile pamoja na mikate isiyochachwa na mboga zenye uchungu.

12Lakini wasisaze nyama mpaka kesho, tena watu wasivunje mifupa, ila waile na kuyafuata maongozi yote ya Pasaka.

13Lakini mtu asipokuwa mwenye uchafu, wala asipokuwa safarini, akiacha tu kuitengeneza kondoo ya Pasaka, mtu aliye hivyo sharti ang'olewe kwao walio ukoo wake, kwani hakumtolea Bwana matoleo siku hiyo iliyowekwa. Mtu aliye hivyo sharti atwikwe kosa lake.

14Kama kwenu atakuwako mgeni, naye akitaka kuitengeneza kondoo ya Pasaka ya Bwana, basi, na aitengeneze na kuyafuata maongozi ya Pasaka na desturi zake ziipasazo; maongozi ya kwenu yawe yaleyale, nayo huwapasa wageni na wenyeji wa nchi hiyo.

Wingu lenye utukufu wa Bwana hulikalia Hema Takatifu.

15Siku hiyo, walipolisimamisha Kao, lile wingu likalifunika Kao kuwa juu yake Hema la Ushahidi; lakini jioni likaonekana juu ya Kao kuwa kama moto mpaka asubui.[#2 Mose 40:34-38.]

16Vikawa hivyo siku zote: hilo wingu lililifunika Kao, tena usiku likaonekana kuwa kama moto.

17Napo, hilo wingu lilipoondoka penye Hema, likiisha, ndipo, wana wa Isiraeli walipoondoka kwenda safari yao; napo mahali, hilo wingu lilipotua, ndipo, wana wa Isiraeli walipopiga makambi.

18Hivyo wana wa Isiraeli waliondoka kusafiri kwa kuagizwa na Bwana, tena kwa kuagizwa na Bwana walipiga makambi. Siku zote, hilo wingu lilipokaa juu ya Kao, nao walikaa makambini.

19Napo hapo, wingu lilipokawilia na kukaa siku nyingi juu ya Kao, wana wa Isiraeli wakamwangalia Bwana, kama ilivyowapasa kumwangalia, lakini hawakuondoka kwenda safari yao.

20Wingu lilipokuwa juu ya Kao siku chache tu, walikaa makambini kwa kuagizwa na Bwana; tena kwa kuagizwa na Bwana waliondoka kwenda safari yao.

21Wingu lilipokaa tu toka jioni hata asubuhi, kisha wingu lilipoondoka asubuhi, nao waliondoka kwenda safari yao; au lilipokaa tu mchana na usiku pamoja, basi, hapo wingu lilipoondoka, nao waliondoka kwenda safari yao.

22Lakini wingu lilipokaa juu ya Kao siku mbili au mwezi au siku nyingi zaidi, nao wana wa Isiraeli walikaa makambini, hawakuondoka kwenda safari yao; lakini lilipoondoka, nao waliondoka kwenda safari yao.

23Hivyo walikaa makambini kwa kuagizwa na Bwana, tena waliondoka kwenda safari yao kwa kuagizwa na Bwana. Ndivyo, walivyomwangalia Bwana, kama ilivyowapasa kuyaangalia, Bwana atakayoyaagiza kinywani mwa Mose.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania