Wafilipi 3

Wafilipi 3

Waepukeni wapotezaji!

1Mwisho, ndugu zangu, furahini kuwa wa Bwana! Kuwaandikia ninyi neno lilo hilo moja tu hakunichokeshi, nanyi huwashupaza.[#Fil. 2:18; 4:4.]

2Jiangalieni mbwa! Jiangalieni watenda kazi waovu! Jiangalieni nao wanaojikatakata tu![#2 Kor. 11:13; Gal. 1:9; 5:12; Ufu. 22:15.]

3Kwani sisi ndio wenye kutahiriwa tunaomtumikia Mungu rohoni; tunajivunia kuwa wake Kristo Yesu, hatujishikizii mambo ya mwili.[#Rom. 2:29.]

4Hata mimi kama ningetaka, ningeweza kujishikizia mambo ya mwili, mtu mwingine akijiwazia kuwa na sababu ya kujishikizia mambo ya mwili, mimi namshinda:[#2 Kor. 11:18,22.]

5nilitahiriwa siku ya nane ya kuzaliwa; kabila langu ni Mwisiraeli wa shina la Benyamini, ni Mwebureo mwenyewe, kwa chama cha Maonyo nalikuwa Fariseo,[#Tume. 26:5.]

6nikajipingia kuwafukuza wateule; hivyo ndivyo, nilivyoutimiza wongofu unaotakwa katika Maonyo, mtu asione la kunionya.

Vitu vyote ni maponzo kwa ajili ya Kristo.

7Lakini hayo, niliyoyawazia kwamba: Ni mapato, yayo hayo nimeyawazia kwamba: Ni maponzo, maana humzuia Kristo.[#Mat. 13:44,46.]

8Kweli nayawazia yote kuwa maponzo, kwani kumtambua Bwana wangu Yesu Kristo ni neno kubwa kuliko yote. Kwa ajili yake yeye niliyaacha yote, kwa kuwa huniponza, nikayawazia kuwa taka, nimpate Kristo tu,[#Mat. 16:26.]

9nionekane kuwa mwake yeye, maana wongofu wangu utokao penye Maonyo sinao tena, ila wongofu nilio nao ni ule utokao kwa kumtegemea Kristo, ni uleule, mtu anaopewa na Mungu akimtegemea.[#Rom. 3:21-22.]

10Huko ndiko kumtambua yeye na nguvu ya ufufuko wake na ya mateso yake, nikiyapata nami kama yeye, hata kufa kwangu kufanane na kufa kwake,[#Rom. 6:3-5; 8:17; 2 Kor. 4:10; Gal. 6:17.]

11nipate kufika kwenye ufufuko katika wafu.

Kuyasahau yaliyoko nyuma.

12Sivisemi hivi kwamba: Nimekwisha kumshika, wala kwamba: nimekwisha kutengenezeka, lakini nakaza mwendo, kwamba nipate kumshika, kama nilivyoshikwa mwenyewe na Kristo Yesu.[#Tume. 6:9; 1 Tim. 6:12.]

13Ndugu, mimi sijiwazii bado, ya kuwa nimwkisha kumshika. Lakini neno moja nalisema: Yaliyoko nyuma mimi huyasahau, kisha hujipingia yaliyoko mbele.[#Luk. 9:62.]

14Nakaza mbio, nifike upesi kwenye mwisho wa kushindania, kwenye tunzo lililoko juu kwake Kristo Yesu, nililoitiwa na Mungu.[#1 Kor. 9:24.]

15Basi, sote tulio watimilifu tuyafuate mawazo hayo! Kama liko, mwawazalo kuwa jinginejingine, hilo nalo Mungu atawafunulia.[#1 Kor. 2:6.]

16Lakini kwanza: hapo, tulipofikia, sharti tupaendelee papo hapo![#Gal. 5:1; 6:16.]

Wachukivu wa msalaba wake Kristo.

17*Niigeni mimi, ndugu, mwakague wale wanaofanya mwendo kama huu, mnaouona kwetu sisi![#1 Kor. 11:1.]

18Kwani wengi huendelea, kama nilivyowaambia mara nyingi, lakini sasa nawaambia kwa kuwalilia: Ndio wachukivu wa msalaba wake Kristo.[#1 Kor. 1:23; Gal. 6:12.]

19Mwisho wao ni kuangamia, mungu wao ni tumbo, utukufu wao umo katika mambo yenye soni, ndio wanaoyawaza tu yaliyopo nchini.[#Rom. 16:18.]

20Lakini wenyeji wetu uko mbinguni, tunakomtazamia hata mwokozi Yesu Kristo.[#Ef. 2:6; Kol. 3:1; Ebr. 12:22.]

21Yeye ataigeuza miili yetu yenye manyonge, ipate kufanana na mwili wake wenye utukufu kwa hiyo nguvu yake iwezayo kuvishinda vyote, vimtii.*[#1 Kor. 15:43,49,53; 2 Kor. 5:1-4.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania