Mifano 3

Mifano 3

Mbaraka ya kumcha Mungu.

1Mwanangu, usiyasahau maonyo yangu!

Nao moyo wako na uyalinde maagizo yangu!

2Kwani yatakupatia siku nyingi na miaka mingi

ya kukaa mwenye uzima na mwenye utengemano.

3Upendo wa kweli usikuache, uufunge shingoni pako,

tena uuandike katika kibao cha moyo wako!

4Ndivyo, utakavyoona upendeleo na akili njema

machoni pake Mungu napo machoni pa watu.

5Mjetee Bwana kwa moyo wako wote,

usijiegemeze utambuzi wako!

6Katika njia zote umjue yeye!

Ndivyo, atakavyokunyoshea mapito yako.

7Usijiwazie mwenyewe kuwa mwenye werevu wa kweli,

ila umche Bwana, uepuke penye mabaya!

8Hii itakuwa dawa ya kitovu chako

na kunywaji cha kuitia mifupa yako nguvu.

9Mheshimu Bwana ukimtolea vipaji vya mali zako

na malimbuko ya mapato yako yote!

10Ndipo, vyanja vyako vitakapojazwa,

nayo makamulio yako yatafurikiwa na pombe mbichi.

11Mwanangu, usiseme: Si kitu, ukichapwa na Bwana!

Wala usilegee, unapokanywa naye!

12Kwani Bwana humchapa anayempenda,

kama baba anavyomchapa mwanawe ampendezaye.

Mbaraka ya ujuzi.

13Mwenye shangwe ni mtu aonaye werevu wa kweli,

naye mtu apataye utambuzi,

14kwani kuupata ni kwema kuliko kupata fedha,

nayo faida yake ni kubwa kuliko dhahabu tupu;

15maana una kima kuliko lulu,

nayo yote pia yapendezayo watu hayalingani nao.

16Siku nyingi za kuwapo zimo kuumeni mwake,

namo kushotoni mwake umo utajiri na utukufu.

17Njia zake ni njia za kupendeza,

nayo mikondo yake ni yenye utengemano.

18Ndio mti wenye uzima kwao walioushika,

mwenye shangwe ni mtu anayeshikamana nao.

19Bwana aliuweka msingi wa nchi kwa werevu wa kweli,

nazo mbingu alizishupaza kwa utambuzi.

20Kwa ujuzi wake vilindi vya maji vikatokea kuwa mboji,

nayo mawingu hudondoka umande.

21Mwanangu, haya yasitoweke machoni pako!

uangalie ujuzi wa kweli na mawazo ya moyo!

22Ndivyo, utakavyoipatia roho yako uzima,

tena utakuwa pambo zuri shingoni pako.

23Ndivyo, utakavyokwenda katika njia yako na kutulia,

nao mguu wako hautajikwaa.

24Utakapolala hutapatwa na woga,

kweli utakapolala, usingizi wako utakuwa mtamu,

25usiyaogope mastusho yatakayokutukia,

wala mwangamizo wao wasiomcha Mungu utakapotimia.

26Kwani Bwana atakuwa egemeo lako,

ataulinda mguu wako, usinaswe.

Watu wasifanyiane mabaya!

27Chema cho chote usimnyime mwenzio apaswaye nacho,

ikiwa, mkono wako unaweza kumpatia.

28Usimwambie mwenzio: Nenda, urudi! nitakupa kesho,

nawe hicho cha kumpa unacho hapo hapo!

29Usiwaze kumfanyizia mwenzio mabaya,

yeye akikaa na wewe pasipo kuogopa kitu!

30Usigombane na mtu bure tu,

kama hakukufanyizia kibaya!

31Mkorofi usimwonee wivu,

wala njia zake usizichague kuwa za kuzishika!

32Kwani mpotovu humtapisha Bwana,

lakini wanyokao ndio, ambao anakula njama nao.

33Kiapizo cha Bwana huzikalia nyumba zao wasiomcha,

lakini makao ya waongofu huyabariki.

34Akijia wafyozaji huwafyoza naye,

lakini wanyenyekevu huwapatia huruma.

35Werevu wa kweli watapata utukufu, uwe fungu lao,

lakini matukuzo yao wapumbavu ndio matwezo yatakayowapata.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania