The chat will start when you send the first message.
2Niseme nini, mwanangu? Niseme nini, mwanangu, niliyekuzaa?
Niseme nini, mwanangu, niliyemwapia viapo?
3Usiwape wanawake nguvu zako!
Wala usizishike njia zao, maana huangamiza wafalme.
4Wafalme, Lemweli, wafalme hawapaswi na kunywa mvinyo,
wala wakuu haiwapasi kuuliza: Vileo viko wapi?
5Wasije kusahau maongozi kwa kunywa kwao,
wakayapotoa mashauri yao wote walio wanyonge.
6Wapeni vileo wanaokwenda kujipoteza,
wapeni mvinyo walio wenye uchungu rohoni mwao!
7Wanywe, wakausahau umaskini wao,
wasiyakumbuke tena masumbuko yao!
8Kifunue kinywa chako kuwatetea wasioweza kusema,
uwasaidie shaurini wote walioachwa peke yao!
9Kifunue kinywa chako, ukate mashauri yaongokayo,
uwapatie wanyonge na maskini shaurini yawapasayo.
10Yuko nani aonaye mwanamke mwenye uwezo mwema?
Kima chake ni kikubwa kuliko kina cha lulu.
11Moyo wa mumewe huweza kumtegemea,
nayo mapato hayakoseki.
12Humfanyizia mema tu, mabaya hayafanyi
siku zote za maisha yake.
13Hutafuta manyoya ya kondoo na pamba,
kisha hufanya kazi za kuzitumia kwa mikono ipendayo kufanya kazi.
14Hufanana na merikebu za mchuuzi,
akileta vyakula vyake toka mbali.
15Huamka usiku, ukiwa haujaisha bado,
huwapa chakula waliomo nyumbani mwake,
nao vijakazi huwapa kazi ziwapasazo.
16Akiviwaza moyoni kuwa vema hivyo hununua shamba,
tena hupanda mizabibu kwa mapato ya mikono yake.
17Hujifunga kiunoni kwa nguvu,
kisha huishupaza mikono yake, ifanye kazi.
18Huona, ya kuwa anafanikiwa vema kwa kujikaza hivyo,
kwa hivyo hata usiku taa yake haizimiki.
19Hutengeneza kitanda cha kufumia kwa mikono yake,
kisha vidole vyake huvifumisha nguo.
20Wanyonge huwashika kwa mkono wake,
nao wakiwa huwapokea kwa mikono yake miwili.
21Haogopi, ya kuwa baridi kali iwapate waliomo nyumbani mwake,
kwani wa nyumbani mwake wote hupata mavazi mekundu ya sufi.
22Hujitengenezea mazulia,
hujivika nguo nzuri za pamba, hata za rangi.
23Mumewe hujulika malangoni mashaurini
akikaa pamoja na wazee wa nchi.
24Hutengeneza fulana, akaziuza,
nayo mishipi huwapa wachuuzi.
25Uwezo na utukufu ndio mavazi yake,
kwa hiyo huyacheka mambo ya siku ijayo.
26Kinywa hukifunua, kiseme maneno yenye werevu wa kweli,
nayo maonyo yenye upole yamo katika ulimi wake.
27Huangalia sana mwenendo wao waliomo nyumbani mwake,
vilaji vya uvivu havili kabisa.
28Wanawe hutokea na kumtukuza,
mumewe naye humshangilia kwamba:
29Wako wanawake wengi wenye uwezo wa kufanya mema,
lakini wewe umewapita wote pia.
30Upendezi hudanganya, nao uzuri ni wa bure,
lakini mwanamke amchaye Bwana hupasa kutukuzwa.
31Mpeni mapato ya mikono yake,
matendo yake yamtukuze malangoni!