Mashangilio 16

Mashangilio 16

Mungu ni mali kuzipita zote.

1Unilinde, Mungu! Kwani nimekukimbilia.

2Nimemwambia Bwana: Wewe u bwana wangu; hakuna nionacho kuwa chema kisichotoka kwako.[#Sh. 73:25.]

3Nao watakatifu waliopo katika nchi nimewaambia: Hawa ndio wakuu wa kweli, ndio wanipendezao kabisa.

4Maumivu yao wakimbiliao mwingine yatakuwa mengi; sitavimimina vinywaji vyao vya tambiko, maana ni vyenye damu, wala majina yao sitayatia tena midomoni mwangu.

5Bwana ni fungu langu, nililolitwaa, tena ni kinyweo, nilichopewa; wewe unanishikizia niliyopatiwa nilipopigiwa kura;[#Omb. 3:24.]

6kamba zake ziliponiangukia niligawiwa pazuri, hilo fungu, nililolitwaa, linapendezeka kweli.

7Nitamkuza Bwana aniongozaye, mafigo yangu hunionya hivyo hata usiku.[#Sh. 4:5; 17:3.]

8*Bwana na anisimamie kila, nitakapokuwa, awe kuumeni kwangu, nisitikisike.

9Kwa hiyo moyo wangu hufurahi, nayo yaliyo utukufu wangu hushangilia, hata mwili wangu utatulia kwa kuwa na kingojeo.[#1 Mose 49:6.]

10Kwani hutaiacha roho yangu, ipotee kuzimuni, wala hutamtoa akuchaye, apate kuoza kaburini.[#Tume. 2:25-32; 13:35-37.]

11Unanitambulisha njia iendayo penye uzima, utanishibisha furaha zilizopo usoni pako; mkono wako wa kuume hutoa kale na kale yapendezayo.*

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania