Mashangilio 35

Mashangilio 35

Maombo ya mtu aumizwaye vibaya na wachukivu wake.

1Bwana, gombana nao wanigombezao! Pigana nao wanipiganishao!

2Shika ngao na kingio! Inuka, unisaidie![#Sh. 7:13-14.]

3Chezesha mkuki, uwakinge wao wanikimbizao! Iambie roho yangu kwamba: Wokovu wako ni mimi.

4Sharti watwezwe kwa kuumbuka waitafutao roho yangu, sharti warudi nyuma na kuinamisha vichwa waniwaziao vibaya;[#Sh. 40:15.]

5sharti wawe kama makapi, yakipatwa na upepo, malaika wa Bwana akiwakumba, waanguke.

6Njia yao sharti iwe yenye giza pamoja na utelezi, atakapowakimbiza malaika wa Bwana.

7Kwani wamenitegea tanzi lao, linikamate, pasipo sababu yo yote, wakaichimbia roho yangu miina pasipo sababu yo yote.[#Sh. 35:19.]

8Na uwajie mwangamizo wa kustusha, ambao walikuwa hawaujui, nalo tanzi lao, walilolitanda, liwakamate wao; huo mwangamizo wa kustusha ukiwapata, na waangushwe nao.[#Sh. 9:16.]

9Ndipo, roho yangu itakapopiga vigelegele kwa kuwa na Bwana, na kuushangilia wokovu, iliouona.

10Ndipo, itakaposema nayo mifupa yangu yote: Bwana, afananaye nawe yuko wapi? Unamponya mnyonge mkononi mwake yeye ampitaye nguvu, kweli huponya mnyonge na mkiwa mikononi mwao wamnyang'anyao.

11Mashahidi wa ukorofi wananiinukia, wananiuliza mambo, nisiyoyajua.

12Mema, niliyowatendea, wanayalipa na kunifanyizia mabaya, ukiwa wa kuwa peke yake uipate roho yangu.[#Sh. 38:21.]

13Lakini vazi langu mimi lilikuwa gunia hapo, walipougua, nikajisumbua kwa kufunga na kwa kuwaombea na kujipiga kifua.[#Iy. 31:29; Rom. 12:15.]

14Niliwaendea, kama ni ndugu yangu, niliyempenda kweli, kama amwombolezeaye mama niliinamisha kichwa kwa kusikitika.

15Lakini wao hulifurahia anguko langu wakikusanyika; kweli walikusanyika kwa ajili yangu mimi, nao nisiowajua wananitukana pasipo kukoma.

16Kwao wenye ulafi wa matusi huyafyoza nayo ya Kimungu, kisha hukereza meno kwa ajili yangu mimi.[#Iy. 16:9.]

17Bwana, utawatazama tu mpaka lini? Irudishe roho yangu uzimani, wasiimalize! Nitoe kwenye wana wa simba! Kwani niko peke yangu.[#Sh. 22:21.]

18Kwa hiyo nitakushukuru, wengi wakutanikapo, na kukuimbia kwenye watu walio wenye nguvu.[#Sh. 22:23.]

19Wapendao uwongo wasinifurahie, wala wasinitazame na jicho baya wanichukiao bure![#Sh. 25:19; 69:5; Yoh. 15:25.]

20Kwani yawezayo kutupatanisha hawayasemi, nao walio watulivu katika nchi huwawazia mambo ya udanganyifu.

21Wananiasamia sana vinywa vyao kwa kusema: Macho yetu yamekuona! Weye! Weye![#Sh. 40:16.]

22Bwana, umeyaona, usiyanyamazie! Usinikalie mbali, Bwana wangu!

23Amka! Inuka, uniamulie! Mungu wangu na Bwana wangu, unigombee![#Sh. 44:24.]

24Niamulie kwa wongofu wako, Bwana Mungu wangu, wasinifurahie!

25Wasiseme mioyoni mwao: Weye! Ndivyo vinavyotupendeza! Wala wasiseme: Tumemmeza!

26Sharti watwezwe wakiumbuliwa wote pamoja waliofurahiwa na mabaya yaliyonipata, sharti wavikwe soni, nyuso ziwaive waliojikuza na kuninyenyekeza.[#Sh. 35:4.]

27Lakini wao waliopendezwa na wongofu wangu sharti wapige vigelegele kwa kufurahiwa! Sharti waseme pasipo kukoma: Mkuu ni Bwana, mtumishi wake akikaa na kutengemana, hupendezwa.[#Sh. 40:17.]

28Ulimi wangu sharti uusimulie wongofu wako, ukusifu wewe siku zote!

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania