Mashangilio 51

Mashangilio 51

Majuto ya Dawidi.

(Wimbo wa juto wa 4.)

1Nihurumie, Mungu, kwa upole wako!

2-3Kwa uchungu wako mwingi, unaotuonea, yafute mapotovu yangu![#2 Sam. 12; Luk. 18:13.]

4Kaza kuniogesha, manza, nilizozikora, zinitoke! Kusudi makosa yangu yaondoke kwangu, na unitakase!

5Kwani mapotovu yangu ninayajua, nayo makosa yangu ninayatazama siku zote.[#Sh. 32:5.]

6Wewe peke yako ndiwe, ambaye nimemkosea, nikayafanya yaliyo mabaya machoni pako; sharti wongofu wako utokezwe na maneno yako, nayo maamuzi yako yakutokeze kuwa mtakatifu.[#Rom. 3:4,19.]

7Unaona, wao, niliozaliwa nao, walikuwa wenye manza, mama yangu aliipata mimba yangu kwa kukosa.[#Yoh. 3:6.]

8Lakini wewe unapendezwa nayo ya kweli, yakiwa ndani moyoni; unifunze, hata mambo yajifichayo yanielekee.

9Nieue ukininyunyizia kivumbasi, nipate kutakata! Niogeshe, nipate kung'aa kama chokaa juani![#3 Mose 14:6-7; Yes. 1:18.]

10Nipe, nisikie tena shangwe za furaha, mifupa, uliyoivunja, ipige vigelegele!

11Ufiche uso wako, usiyaone hayo makosa yangu! Yafute manza zote, nilizozikora!

12Mungu, niumbie moyo utakatao! Nayo roho uirudishie upya kifuani mwangu, ipate nguvu![#Ez. 36:26; Mat. 5:8.]

13Usinitupe na kuniondoa usoni pako, wala Roho yako takatifu usiitoe mwangu!

14Nifurahishe tena na kuniokoa! Kwa kunipa roho ipendayo kutumika unishikize!

15Hivyo nitawafundisha wapotovu njia zako, wakosaji wapate kurudi kwako wewe!

16Mungu, nikomboe katika manza za damu, nilizozikora! maana u Mungu aniokoaye, ulimi wangu ukushangilie kwamba: U mwongofu!

17Bwana, ifumbue midomo yangu, kinywa changu kiyatangaze matukuzo yako!

18Kwani hupendezwi na ng'ombe za tambiko, ningekupa; nayo ng'ombe ya tambiko iteketezwayo nzima huitaki.[#Sh. 40:7; 50:8-13.]

19Ng'ombe za tambiko, Mungu apendazo, ni roho ivunjikayo, moyo uliovunjika kwa kupondeka, wewe Mungu, hutaubeza.[#Sh. 34:19.]

20Na vikupendeze kufanya, pale Sioni pawe pazuri, nayo maboma ya Yerusalemu yajenge tena!

21Kisha utapendezwana ng'ombe za tambiko zilizo za kweli, ni zile za kuchomwa motoni nazo za kuteketezwa nzima; hapo ndipo, watakapokupelekea ng'ombe mezani pako pa kutambikia.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania