Mashangilio 97

Mashangilio 97

Ufalme ni wake Mungu.

1Bwana ni mfalme! Nchi na zishangilie! Navyo visiwa vilivyo vingi na vifurahi![#Sh. 93:1.]

2Mawingu yenye giza yanamzunguka, shikizo la kiti chake cha kifalme ni wongofu unyoshao maamuzi.[#Sh. 89:15.]

3Moto ndio unaomtangulia, nao unawateketeza wabishi wake po pote, walipo.[#Hab. 3:3-6.]

4Meme, azipigazo, zinamulika huku nchini, nazo nchi hustuka zikiziona.

5Milima inayeyuka kama nta mbele yake Bwana, mbele yake yeye azitawalaye nchi zote.

6Mbingu zinautangaza wongofu wake, nayo makabila yote ya watu huuona utukufu wake.[#Sh. 19:2.]

7Sharti wapatwe na soni wote watumikiao vinyago, wajivuniao miungu iliyo ya bure; mwangukieni yeye, ninyi miungu yote![#Ebr. 1:6.]

8Wasioni wanavisikia na kufurahi, binti Yuda hukupigia vigelegele, Bwana, kwa ajili ya maamuzi yako,[#Fil. 4:4-5.]

9Kwani wewe Bwana ndiwe uliye mkuu wa ulimwengu wote, wewe unatukuka sana kuliko miungu yote.[#Sh. 96:4.]

10Ninyi mmpendao Bwana, yachukieni mabaya! Huzilinda roho zao wamchao yeye, huwaopoa mikononi mwao wasiomcha Mungu.[#Amo. 5:14-15.]

11Mwanga unamzukia aliye mwongofu, nayo furaha inawazukia walionyoka mioyo.[#Sh. 112:4.]

12Ninyi waongofu, mfurahieni Bwana, mwakumbushe watu utakatifu wake!

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania