The chat will start when you send the first message.
1Kisha nikapewa mwanzi uliofanana na fimbo, nikaambiwa: Inuka, ulipime Jumba la Mungu na meza ya Bwana nao wenye kutambikia mlemle![#Ez. 40:3-5; Zak. 2:1-2.]
2Lakini ua ulioko nje penye Jumba la Mungu uuache nje, usiupime! Kwani huo wamizimu wamepewa, waukanyage mji mtakatifu miezi 42.[#Ufu. 11:3; 12:6,14; 13:5; Luk. 21:24.]
3Nami nitawapa mashahidi wangu wawili, wawafumbulie siku 1260 wakiwa wamevaa magunia.[#Ufu. 11:2.]
4Hao ndio ile michekele miwili na ile mienge miwili iliyosimama mbele ya Bwana wa nchi.[#Zak. 4:3,11-14.]
5Tena mtu akitaka kuwapotoa, hutoka moto vinywani mwao na kuwala hao wachukivu wao. Kila atakaye kuwapotoa sharti auawe hivyo.[#2 Fal. 1:10.]
6Hao wanazo nguvu za kuzifunga mbingu, mvua isinye siku za ufumbuaji wao. Tena wanazo nguvu za maji za kuyageuza kuwa damu na za kuipiga nchi mapigo yo yote napo po pote, watakapotaka.[#2 Mose 7:19-20; 1 Fal. 17:1.]
7Nao watakapoumalizia ushahidi wao, patatoka nyama mkali kuzimuni, atafanya vita nao, mpaka awashinde, awaue.[#Ufu. 13:1,7; 17:8; Dan. 7:7,21.]
8Kisha mizoga yao itakaa katika njia ya mji ule mkubwa unaoitwa kiroho Sodomu na Misri; ndipo, naye Bwana wao alipowambwa msalabani.[#Ufu. 16:19; Yes. 1:9,10; Luk. 13:34.]
9Nao watu wa makabila na wa mashina na wa misemo na wa wamizimu wataiona mizoga yao siku tatu na nusu, lakini hawataacha, mizoga yao izikwe kaburini.
10Kwa hiyo wakaao nchini watashangilia kwa ajili yao na kupiga vigelegele na kupelekeana matunzo, kwa sababu wafumbuaji wale wawili waliwatesa wakaao nchini.
11Lakini siku tatu na nusu zilipopita, roho ya uzima ilitoka kwa Mungu, ikawaingia; ndipo, waliposimama kwa miguu yao, woga mwingi ukawaguia waliowaona.[#Ez. 37:5,10.]
12Kisha wakasikia sauti kuu toka mbinguni iliyowaambia: Pandeni huku! Walipopanda mbinguni katika wingu, wachukivu wao walikuwa wanawatazama.[#2 Fal. 2:11.]
13Saa ileile pakawa tetemeko kubwa la nchi, nalo fungu la kumi la mji likafudikizwa, watu waliouawa na hilo tetemeko la nchi majina yao yalikuwa 7000. Nao waliosalia wakashikwa na woga, wakamtukuza Mungu wa mbingu.
14Pigo la pili limekwisha kupita. Tazama, la tatu linakuja upesi.[#Ufu. 9:12; 11:15; 12:12.]
15Malaika wa saba alipopiga baragumu, kukawa na sauti kuu nyingi mbinguni zikisema:
Ufalme wa ulimwengu umekwisha kuwa wake
Bwana wetu na wa Kristo wake;
ndiye atakayetawala kale na kale pasipo mwisho.
16Ndipo, wale wazee 24 waliokaa mbele ya Mungu katika viti vyao vya kifalme walipoanguka nyusoni pao, wakamsujudia Mungu[#Ufu. 4:4,10; 7:11.]
17na kusema:
Twayavumisha mema yako wewe, Bwana Mungu Mwenyezi,
Ndiwe aliopo naye aliyekuwapo! Umekwisha kuutwaa
ufalme kwa uwezo wako mwingi.
18Wamizimu walipopatwa
na makali ndipo, makali, yako yalipotokea, ndipo,
siku yako ilipotimia ya kuwahukumu wafu na ya
kuwapokeza watumwa wako walio wafumbuaji nao watakatifu
nao walioliogopa Jina lako, walio wadogo nao walio
wakubwa. Siku imetimia ya kuwaangamiza wenye kuiangamiza nchi.
19Kisha Jumba la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa, mkaonekana mlemle Jumbani mwa Mungu Sanduku la Agano lake. Kukapiga umeme na uvumi na ngurumo, kukawa na tetemeko la nchi na mvua nyingi sana ya mawe.[#Ufu. 4:5; 15:5.]