Ufunuo 14

Wimbo mpya wa watu waliokombolewa.

1Kisha nikamwona Mwana kondoo, akisimama mlimani kwa Sioni juu. Pamoja naye kulikuwako watu 144000 waliokuwa wameandikwa Jina lake na Jina la Baba yake mapajini pao.[#Ufu. 3:12; 7:4; Yoe. 2:32.]

2Nikasikia sauti toka mbinguni kama uvumi wa maji mengi na kama uvumi wa ngurumo kuu. Hizo sauti, nilizozisikia, zilikuwa kama za wapiga mazeze, wakiyapiga mazeze yao.[#Ufu. 1:15.]

3Wakaimba wimbo mpya mbele ya kiti cha kifalme penye wale nyama wanne na wale wazee. Hakuwako mtu aliyeweza kujifunza ule wimbo, wasipokuwa wale 144000 waliokombolewa na kuondolewa nchini.[#Ufu. 5:9.]

4Hawa ndio wasiochafuliwa na wanawake; kwa hiyo huwa kama vijana. Tena ndio wamfuatao Mwana kondoo po pote, anapokwenda, kwa kuwa walikombolewa kwenye watu, wawe malimbuko yake Mungu nayo yake Mwana kondoo.[#Ufu. 5:9; 2 Kor. 11:2; Ef. 5:27.]

5Vinywani mwao hamkuonekana uwongo; wako pasipo kilema.

Mbiu za hukumu.

6Kisha nikaona malaika mwingine, akiruka mbinguni kati na kuushika Utume mwema wa kale na kale wa kuwatangazia nchini wamizimu wote na mashina yote na misemo yote na makabila yote.[#Ufu. 8:13.]

7Naye akasema kwa sauti kuu: Mcheni Mungu na kumtukuza! Kwani saa ya hukumu yake imekuja. Mwangukieni yeye aliyeziumba mbingu na nchi na bahari na chemchemi za maji!

8Pakafuata mwingine, ni malaika wa pili, akasema: Umeanguka! Umeanguka mji mkubwa wa Babeli uliowanywesha wamizimu wote mvinyo ya ugoni wake itokezayo makali.[#Ufu. 18:2; Yes. 21:9; Yer. 25:15-16; 51:7-8.]

9Pakawafuata mwingine, ni malaika wa tatu, akasema kwa sauti kuu: Mtu akimwangukia yule nyama na kinyago chake na kujitia chapa chake pajini pake au mkononi pake,[#Ufu. 13:12-17.]

10huyo atakunywa mvinyo yenye makali ya Mungu, iliyoandaliwa pasipo kuchanganywa na maji katika kinyweo cha makali yake, kisha ataumizwa motoni mwenye viberitiberiti mbele ya malaika watakatifu na mbele ya Mwana kondoo.[#Ufu. 16:19; 19:20; Sh. 75:9; Yer. 25:15.]

11Moshi wa maumivu yao hupanda kale na kale, hawapati mapumziko mchana na usiku hao waliomwangukia yule nyama na kinyago chake, nao waliojitia chapa cha jina lake.[#Ufu. 19:3.]

12Hapa ndipo, watakatifu watakapovumilia, wayashikao maagizo ya Mungu wakifuliza kumtegemea Yesu.[#Ufu. 12:17; 13:10.]

13Kisha nikasikia sauti toka mbinguni, ikisema: Andika: Wenye shangwe ni wafu waliokufa na kumtegemea Bwana tangu sasa. Kweli Roho anasema: Huyapumzikia masumbuko yao, kwani matendo yao hufuatana nao.[#Yes. 57:2; Ebr. 4:10.]

Mndu mkali na kamulio.

14Nilipotazama tena nikaona wingu jeupe, humo winguni juu palikaa aliyefanana na mwana wa mtu; alikuwa na kilemba cha dhahabu kichwani pake, mkononi mwake alishika mndu mkali.[#Dan. 7:13; 10:16; Mat. 13:39,41.]

15Hapo akatoka malaika mwingine Jumbani mwa Mungu, akapiga sauti kuu ya kumwambia yule aliyekaa winguni juu kwamba: Tuma mndu wako, uvune! Kwani saa ya kuvuna imekuja, kwa kuwa mavuno yaliyoko nchini yamekauka.[#Yoe. 3:13.]

16Ndipo, yule aliyekaa winguni juu alipoutupa mndu wake nchini, nayo nchi ikavunwa.

17Kisha pakatoka malaika mwingine katika Jumba la Mungu lililoko mbinguni, huyu naye alishika mndu mkali.

18Pakatoka na malaika mwingine penye meza ya Bwana; yeye alikuwa na nguvu ya moto, akapiga sauti kuu ya kumwambia mwenye mndu mkali akisema: Tuma mndu wako mkali, uvichume vichala vya mizabibu ya nchini, kwani zabibu zake zimeiva.[#Ufu. 14:15.]

19Ndipo, malaika alipoutupa mndu wake nchini, akazichuma zabibu zilizoko nchini, akazitia katika kamulio kubwa lililojaa makali ya Mungu.[#Ufu. 19:15.]

20Namo humo kamulioni zikakamuliwa nje ya mji, ndipo, humo kamulioni mlipotoka damu, ikapajaa, ikafika mpaka penye hatamu za farasi; mtu akipazunguka ni mwendo wa siku mbili mchana kutwa.[#Yes. 63:3,6.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania