Ufunuo 7

144000 waliotiwa muhuri.

1Kisha nikaona malaika wanne waliosimama penye pembe nne za nchi, wakizishika pepo nne za nchi, maana upepo usivume nchini wala baharini wala penye mti wo wote.[#Dan. 7:2; Zak. 6:5; Mat. 24:31.]

2Nikaona malaika mwingine aliyepanda toka maawioni kwa jua, alikuwa na muhuri ya Mungu aliye Mwenye uzima, akawaita kwa sauti kuu wale malaika wanne waliopewa kuzipotoa nchi na bahari,

3akasema: Msizipotoe nchi wala bahari wala miti, mpaka tuishe kuwatia watumwa wa Mungu wetu muhuri penye mapaji yao.[#Ufu. 9:4; Ez. 9:4,6.]

4Ndipo, nilipoisikia hesabu yao waliotiwa muhuri, walikuwa 144000 wenye kutiwa muhuri ya mashina yote ya wana wa Isiraeli:[#Ufu. 14:1,3.]

5Waliotiwa

muhuri ya shina la Yuda walikuwa 12000,

muhuri ya shina la Rubeni walikuwa 12000,

muhuri ya shina la Gadi walikuwa 12000,

6muhuri ya shina la Aseri walikuwa 12000,

muhuri ya shina la Nafutali walikuwa 12000,

muhuri ya shina la Manase walikuwa 12000,

7muhuri ya shina la Simeoni walikuwa 12000,

muhuri ya shina la Lawi walikuwa 12000,

muhuri ya shina la Isakari walikuwa 12000,

8muhuri ya shina la Zebuluni walikuwa 12000,

muhuri ya shina la Yosefu walikuwa 12000,

muhuri ya shina la Benyamini walikuwa 12000,

Mkutano mwingi wao waliovikwa nguo nyeupe.

9*Kisha nikatazama, nikaona mkutano mwingi usiohesabika na mtu wo wote, ni watu wa wamizimu wote na wa mashina yote na wa makabila yote na wa misemo yote. Walisimama mbele ya kiti cha kifalme na mbele ya Mwana kondoo; walikuwa wamevikwa kanzu nyeupe, namo mikononi mwao walishika makuti ya mitende.[#Ufu. 6:11.]

10Nao wakatoa sauti kuu wakisema:

Wokovu ni wa Mungu wetu akaaye kitini mwa kifalme

na wa Mwana kondoo!

11Ndipo, malaika wote waliosimama na kukizunguka kiti cha kifalme na wale wazee na wale nyama wanne, walipoanguka nyusoni pao mbele ya kiti cha kifalme, wakamsujudia Mungu wakisema:[#Ufu. 5:11; 11:16.]

12Kweli, mapongezo na utukufu na werevu wa kweli

na shukrani na heshima na uwezo na nguvu

ni za Mungu wetu kale na kale pasipo mwisho! Amin.

13Mmoja wao wale wazee akaniuliza akisema: Hawa waliovikwa kanzu nyeupe ni akina nani? Nao wametoka wapi?

14Nikamwambia: Bwana wangu, wewe unajua. Akaniambia: Hawa ndio waliotoka katika maumivu makubwa, ndio waliozifua nguo zao na kuzing'aza kwa damu ya Mwana kondoo.[#Ufu. 3:10; Mat. 24:21; Ebr. 9:14.]

15Kwa hiyo wako mbele ya kiti cha kifalme cha Mungu na kumtumikia mchana na usiku Jumbani mwake. Anayekaa kitini mwa kifalme atakapotua kwao,[#Ufu. 11:19; 14:15,17; 15:5,8; 16:1; 21:3,22.]

16hawataona tena njaa wala kiu, wala jua halitawachoma wala jasho lo lote.[#Yes. 49:10.]

17Kwani Mwana kondoo aliomo katikati ya kiti cha kifalme atawachunga na kuwaongoza kwenye chemchemi za maji ya uzima. Naye Mungu atayafuta machozi yote machoni mwao.*[#Ufu. 5:6; 21:4; Sh. 23:2; Yes. 25:8.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania