Waroma 1

Waroma 1

Anwani.

1Mimi Paulo nilye mtumwa wa Kristo Yesu nimeitwa kuwa mtume kwa hivyo, nilivyochaguliwa, niutangaze Utume mwema wa Mungu.[#Tume. 9:15; 13:2; Gal. 1:15.]

2Huo aliuagia kale kwa vinywa vya Wafumbuaji wake waliouandika katika barua takatifu;[#Rom. 16:25-26; Tit. 1:2.]

3ni mambo ya Mwana wake Yesu Kristo, Bwana wetu. Huyu alizaliwa kimtu katika uzao wa Dawidi,[#Rom. 9:5; 2 Sam. 7:12; Mat. 22:42.]

4tena hapo, alipofufuliwa katika wafu, ikatokea waziwazi, ya kuwa ni Mwana wa Mungu kwa nguvu ya Kiroho iliyo yenye kutakasa.[#Mat. 28:18; Tume. 13:33.]

5Yeye ndiye aliyetugawia kuwa mitume, tuwafundishe wamizimu wote usikivu wa kumtegemea, Jina lake litukuzwe.[#Rom. 15:18; Tume. 26:16-18; Gal. 2:7,9.]

6Miongoni mwao mlikuwa nanyi, mkaitwa na Yesu Kristo.

7Nawaandikia nyote mnaokaa Roma, mlio wapenzi wa Mungu, mlioitwa kuwa watakatifu: Upole uwakalie na utengemano unaotoka kwa Mungu, Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo![#4 Mose 6:25-26; 1 Kor. 1:2; 2 Kor. 1:1; Ef. 1:1.]

Nguvu ya Utume.

8Kwanza ninamshukuru Mungu wangu katika Yesu Kristo kwa ajili yenu ninyi nyote, kwa kuwa hivyo, mnavyomtegemea, hutangazwa ulimwenguni mote.[#Rom. 16:19; 1 Tes. 1:8.]

9Kwani Mungu, ninayemtumikia moyoni mwangu kwa kuutangaza Utume mwema wa Mwana wake, huyu Mungu ni shahidi wangu, ya kuwa sikuacha kuwakumbuka ninyi[#Ef. 1:16; Fil. 1:8.]

10siku zote po pote, ninapoomba. Ninalojiombea ni hili: Mungu apendezwe kunifungulia ile njia nzuri ya kuja kwenu,[#Rom. 15:23,32; Tume. 19:21.]

11kwani ninatunukia kuonana nanyi, nipate kuwagawia nanyi kipaji chochote cha Kiroho, mshupazwe vizuri.[#Tume. 28:31.]

12Hivyo tutatulizana mioyo pamoja nanyi na kuonyeshana mategemeo yetu, tunayoyakalia ninyi na mimi.[#2 Petr. 1:1.]

13*Lakini ndugu zangu, sitaki, mkose kujua, ya kuwa nilijielekeza mara nyingi, nije kwenu, nione pato hata kwenu, kama nilivyoliona kwa wamizimu wengine; lakini nimezuiliwa mpaka leo hivi.

14Nimeingia udeni kwa Wagriki hata kwa washenzi, kwa wajuzi hata kwa wapuzi.

15Kwa hivyo, nilivyo mimi, nimekwisha kujifunga, niwapigie nanyi ile mbiu njema huko Roma.

16Maana sioni soni ya kuutangaza Utume mwema wa Kristo, kwani unayo nguvu ya Mungu ya kuwaokoa wo wote wanaoutegemea, kwanza Wayuda, kisha Wagriki nao.[#Sh. 119:46; Tume. 13:46; 1 Kor. 1:18,23-24.]

17Kwani humo unafunuliwa wongufu wa Kimungu, wanaopewa wenye kumtegemea, wajikaze kumtegemea. Ndivyo vilivyoandikwa ya kuwa:

Mwongofu atapata uzima kwa kumtegemea Mungu.

Makosa ya wamizimu.

18Kwani makali ya Mungu yanashuka toka mbinguni, yawatokee watu wote wasiomcha Mungu nao wenye upotovu, wanaoyazuia yaliyo ya kweli kwa upotovu wao;

19kwani mambo ya Mungu yametambulikana kwao, maana yalifumbuliwa, naye Mungu ndiye aliyewafumbulia.[#Tume. 14:15-17; 17:24-28.]

20Kwani hivyo, ambavyo macho ya watu hayajaviona, maana nguvu yake ya kale na kale na Kimungu chake, hujulikana, tena huonekana, mtu akivitazama, Yeye alivyovifanya tangu hapo, alipouumba ulimwengu; kwa hiyo hawana la kujikania.*[#Sh. 19:2; Ebr. 11:3.]

21Wangawa walimtambua Mungu, hawakumtukuza kwamba: Ni Mungu, wala hawakumshukuru, Kwa hiyo mawazo yao yakawa ya bure, nayo mioyo yao isiyoyajua yaliyo ya kweli ikaingiwa na giza.[#Ef. 4:18.]

22Walipojiwazia kuwa werevu wa kweli, ndipo, walipopumbazika.[#Yer. 10:14; 1 Kor. 1:20.]

23Wakaugeuza utukufu wa Mungu asiyeoza, wakamfananisha na mfano wa sura ya mtu anayeoza na wa ndege na wa nyama na wa wadudu.[#2 Mose 20:4; 5 Mose 4:15-19.]

24Kwa hiyo Mungu akawatupa, wajichafue wakizifuata tamaa za mioyo yao na kujipujua, mpaka wakifujiana miili yao wao kwa wao;[#Tume. 14:16.]

25ni wao hao walioigeuza kweli ya Mungu kuwa uwongo, wakakitambikia kiumbe na kukitumikia kuliko Muumbaji aliye mwenye kutukuzwa kale na kale. Amin.

26Kwa hiyo Mungu aliwatupa, waingiwe na tamaa za upujufu. Kwani hata wanawake wao wakayageuza matumikio yao ya kimtu, wakazusha mengine yasiyo ya kimtu.

27Vile vile hata waume wakaacha kuwatumia wanawake kimtu, tena kwa hivyo, tamaa zao zilivyowachoma kama moto, wakatumiana waume na waume wenzao; wakafanya hayo yasiyopasa kamwe, wakapata malipo ya upotevu wao yaliyowapasa.[#3 Mose 18:22; 20:13; 1 Kor. 6:9.]

28Tena kwa hivyo, walivyokataa kumshika Mungu na kumtambua, Mungu aliwatupa, wafuate mawazo ya ujinga na kufanya yasiyompasa mtu.

29Wakaenea upotovu wote na ubaya na choyo na uovu, wakajaa kijicho na uuaji na magombano na manyatio na mazoezo maovu.

30Ndio watetaji, wabishi, wasingiziaji, wenye kumbeza Mungu na kubeza watu, wenye kujivuna na kujitukuza, wenye maoneo maovu na wenye kuwakataa wazee.

31Hawana utambuzi wala welekevu wala upendo wala huruma.

32Nao walikuwa wameyambua yaliyoongoka mbele ya Mungu kwamba: Wanaoyatenda mambo hayo wamepaswa na kuuawa; tena hawayafanyi tu hayo, lakini nao wengine wakiyatenda, wanapendezwa.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania