Waroma 3

Waroma 3

Wayuda na Wagriki, wote ni wakosaji.

1Ikiwa hivyo, Wayuda wanapitaje wengine? Au kutahiriwa kunafaaje?

2Hufaa sana hapo na hapo. Kwanza waliagiziwa maneno yake Mungu.[#Rom. 9:4; 5 Mose 4:7-8; Sh. 147:19-20.]

3Au mwawazaje? Wengine wao wakikataa kuyategemea, huo ukatavu wao utautangua welekevu wake Mungu?[#Rom. 9:6; 11:29; 2 Tim. 2:13.]

4La, sivyo! Sharti Mungu ajulikane kuwa mwenye kweli, lakini kila mtu sharti ajulikane kuwa mwenye uwongo, kama ilivyoandikwa:

Sharti wongofu wako utokezwe na maneno yako,

upate kushinda utakapobishiwa.

5Lakini upotovu wetu ukiutokeza wongofu wake Mungu, tutasemaje? Je? Mungu naye siye mpotovu akitutolea makali? (Nasema kimtu.)

6La, sivyo! Mungu angaliwezaje kuuhukumu ulimwengu?

7Lakini kweli ya Mungu ikiongezwa utukufu na uwongo wangu, mimi tena ninahukumiwaje kama mkosaji?

8Hivyo sivyo, tunavyosingiziwa, wengine wakitusema sisi, kwamba tumesema: Na tuyafanye yaliyo maovu, yaliyo mema yapate kutokea? Hao hukumu yao inapasa kabisa.[#Rom. 6:1-2.]

9Sasa Je? Tumewapita? Hapana, hata kidogo tu. Kwani hapo mbele tumewasuta wote, Wayuda na Wagriki, kwamba: Wote ni wakosaji,[#Rom. 1:18—2:24.]

10kama ilivyoandikwa:

Hakuna aliye mwongofu hata mmoja.

11Hakuna aliye mwenye akili, hakuna anayemtafuta Mungu.

12Wote pamoja wamepotelewa na njia, wote ni waovu.

Hakuna anayefanya mema, hakuna hata mmoja.

13Makoo yao huwa makaburi yaliyo wazi,

ndimi zao huzitumia uwongo tu,

sumu ya pili imo midomoni mwao.

14Vinywa vyao hujaa matusi na uchungu,[#Sh. 10:7.]

15miguu yao hupiga mbio kuja kumwaga damu.[#Yes. 59:7-8.]

16Maangamizo na mavunjiko huzijulisha njia zao,

17lakini njia ya utengemenao hawaijui.

18Kumwogopa Mungu hakupo machoni pao.[#Sh. 36:2.]

19Lakini sisi twajua: Yote, Maonyo yanayosema, huwaambia wenye kuyashika Maonyo, kila kinywa kifumbwe, nao ulimwengu wote uwe umepaswa na hukumu ya Mungu.[#Rom. 2:12; Gal. 3:22.]

20Kwa hiyo hapo, alipo, hapana mwenye mweli wa kimtu atakayepata wongofu kwa kwamba: Ameyafanya Maonyo, kwa sababu Maonyo huleta utambuzi tu wa makosa.[#Rom. 7:7; Sh. 143:2; Gal. 2:16.]

Wongofu wa Kimungu.

21*Lakini sasa wongofu wa Kimungu umefunuliwa pasipo Maonyo; nao unashuhudiwa na Maonyo pamoja na Wafumbuaji kwamba:[#Rom. 1:17; Tume. 10:43.]

22Wongofu wa Kimungu ndio huu: mwanzo ni kumtegemea Yesu Kristo, nao mwisho: wote wanaomtegemea huupata. Kwani hawapitani,

23kwa sababu wote wamekosa, wakalipoteza fungu lao la utukufu wa Mungu.[#Rom. 3:9,19; 5:2.]

24Kwa hiyo wanapata wongofu bure tu, kwani ni gawio, Yesu Kristo alilowapatia hapo, alipoyalipa makombozi yao.[#Rom. 5:1; Ef. 2:8.]

25Ndiye, Mungu aliyemtoa, kusudi wenye kumtegemea wajipatie Kiti cha Upozi katika damu yake; hapo ndipo, alipoonyesha, wongofu wake ulivyo, akiwaondolea makosa ya kale,[#3 Mose 6:12-16; Ebr. 4:16.]

26ambayo Mungu alikuwa akiyavumilia. Hivi ndivyo, alivyouonyesha siku hizi za sasa wongofu wake kuwa hivyo: Mwenyewe ni mwongofu, tena mwenye kumtegemea Yesu humpa wongofu.

27Basi, majivuno yako wapi? Yamefungiwa! Kwa nguvu ya maonyo gani? Ni yale yanayotaka matendo? Hapana, ni Maonyo yanayotaka kutegemewa tu.[#1 Kor. 1:29,31.]

28Kwani tunalishika hili la kwamba: Mtu hupata wongofu kwa kumtegemea Mungu tu, ijapo asiyatimize Maonyo.*[#Gal. 2:16.]

29Au je? Mungu ni Mungu wao Wayuda tu? Siye Mungu wa wamizimu nao? Kweli, ni Mungu wa wamizimu nao,[#Rom. 10:12.]

30kwani Mungu ni mmoja tu; waliotahiriwa huwapatia wongofu, wakiwa wanamtegemea; vilevile wasiotahiriwa huwapatia wongofu, wakiwa wanamtegemea.[#Rom. 4:11-12.]

31Je? Ikiwa hivyo, tutayatangua Maonyo kwa kule kumtegemea? Sivyo, tutayasimamisha.[#Rom. 3:21; 4:3; 8:4; Mat. 5:17.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania