Waroma 4

Waroma 4

Wongofu wa Aburahamu na wa Dawidi.

1Basi, tusemeje? Aburahamu, baba yetu wa kale, kimtu ameonaje?

2Kwani Aburuhamu, kama alipata wongufu kwa ajili ya matendo yake, kweli analo la kujivunia, lakini mbele ya Mungu haliko.

3Kwani Maandiko yanasemaje?

Aburahamu alimtegemea Mungu,

kwa hiyo aliwaziwa kuwa mwenye wongofu.

4Lakini mtu wa kazi haupati mshahara wake kama kipaji, anachogawiwa, ila kama malipo yanayompasa.[#Rom. 11:6; Mat. 20:7,14.]

5Lakini asiye mtu wa kazi akimtegemea anayewapatia wongofu nao wasiomcha Mungu, basi, huyo anapata wongofu kwa kumtegemea Mungu.

6Ndivyo, anavyosema hata Dawidi kwa kumshangilia mtu, Mungu amwaziaye kuwa mwenye wongofu, ijapo asiyatimize Maonyo.[#Sh. 32:1-2.]

7Akasema:

Wenye shangwe ndio walioondolewa mapotovu

nao waliofunikwa makosa.

8Mwenye shangwe ni mtu, Bwana asiyemhesabia makosa.

9Basi, wenye kushangiliwa hivyo ndio waliotahiriwa au wasiotahiriwa nao? Kwani twasema: Aburahamu aliwaziwa kuwa mwenye wongofu kwa kumtegemea Mungu.

10Ilikuwa lini, alipowaziwa hivyo? Alipokuwa ametahiriwa au alipokuwa hajatahiriwa bado? Sipo hapo, alipokwisha tahiriwa, ila hapo alipokuwa hajatahiriwa bado.

11Kisha akatahiriwa, apate kielekezo, kiwe kama muhuri ya wongofu uliotoka kwa kumtegemea Mungu, alipokuwa hajatahiriwa bado. Hivyo yeye ni baba yao wote watakaomtegmea Mungu wakiwa hawakutahiriwa; maana nao sharti wawaziwe kuwa wenye wongofu.[#1 Mose 17:10-11.]

12Vilevile ni baba yao waliotahiriwa; lakini waliotahiriwa nje tu sio; ni wale tu waliotahiriwa, kisha wakakaza kuzifuata nyayo za kumtegemea Mungu, baba yetu Aburahamu alikokuwa nako alipokuwa hajatahiriwa bado.[#Mat. 3:9.]

13Kwani Maonyo siyo yaliyompatia Aburahamu au wao wa uzao wake kiagio cha kwamba; Urithi wako ni ulimwengu wote; hicho amekipata kwa wongofu uliotoka kwa kumtegemea Mungu.[#1 Mose 18:18; 22:17-18.]

14Kama wenye kuyafuata Maonyo wangekuwa nao warithi, kumtegemea Mungu kungekuwa kwa bure, tena kile kiagio nacho kingekuwa kimekwisha kutanguliwa.

15Kwani Maonyo huleta makali tu; lakini pasipo Maonyo hata kuyakosea hakuna.[#Rom. 3:20; 5:13; 7:8,10.]

16Kwa hiyo wenye kumtegemea Mungu ndio watakaogawiwa; tena hivyo kile kiagio kinawatimilia wao wote walio uzao wake, sio wenye kuyafuata Maonyo tu, ila nao wenye kuifuata njia yake Aburahamu ya kumtegemea Mungu; hivyo ndivyo, anavyokuwa baba yetu sisi sote,

17kama ilivyoandikwa:

Nimekuweka, uwe baba yao mataifa mengi.

Ni kwa sababu alimtegemea Mungu anayewarudisha wafu uzimani, anayeviita visivyokuwapo, vikapata kuwapo.

18Napo hapo palipokuwa pasipo kingojeo cho chote, alifuliza kukitegemea kingojeo cha kwamba: Atakuwa baba ya mataifa mengi, kama ilivyosemwa: Hivyo ndivyo, wao wa uzao wako watakavyokuwa.[#1 Mose 15:5.]

19Tena kumtegemea Mungu hakukumpungukia napo hapo, alipouona mwili wake, ya kuwa umekufa; maana alikuwa wa miaka kama mia; wala hapo, alipomwona mama yetu Sara, ya kuwa mwili wake umekufa vilevile.[#1 Mose 17:17.]

20Hata kile kiagio cha Mungu hakupotelewa nacho, kwani kukitegemea hakukumshinda, ila akakaza kukitegemea kwa nguvu, akamtukuza Mungu.[#Ebr. 11:7,11.]

21Maana aliyashika moyoni, aliyoyatambua ya kuwa: Yeye ana nguvu ya kuyatimiza, aliyoyaagia.

22Hivyo ndivyo, alivyowaziwa kuwa mwenye wongofu.[#Rom. 4:3.]

23Lakini hilo halikuandikwa kwa ajili yake tu, ya kuwa ndivyo, alivyowaziwa,[#Rom. 15:4.]

24ila hata kwa ajili yetu, tutakaowaziwa vivyo hivyo tukimtegemea yeye aliyemfufua Bwana wetu Yesu katika wafu,

25aliyetolewa kwa ajili ya maanguko yetu, akafufuliwa kwa ajili ya wongufu wetu.[#Yes. 53:4-5; 1 Kor. 15:17; 2 Kor. 5:21.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania