The chat will start when you send the first message.
1*Kwa hivyo, tulivyopewa wongofu kwa kumtegemea Mungu, tumekwisha kupata utengemano kwake Mungu; naye aliyetupatia ni Bwana wetu Yesu Kristo.[#Rom. 3:24,28; 4:24; Yes. 53:5.]
2Kwa kumtegemea yeye tumefunguliwa njia ya kulifikia gawio hili, tunalolikalia, tukajivunia kingojeo cha utukufu, Mungu atakaotupa.[#Ef. 3:12; 1 Yoh. 3:21-22.]
3Lakini si hiki tu, ila twajivunia hata maumivu, kwani twajua ya kuwa: Maumivu huleta uvumilivu;[#Ebr. 10:36; Yak. 1:2-3.]
4nao uvumilivu huleta welekevu; nao welekevu huleta kingojeo;
5nacho kingojeo hakitudanganyi, kwani upendo wa Mungu umemiminiwa mioyoni mwetu na Roho Mtakatifu, tuliyepewa sisi.[#Ebr. 6:18-19.]
6Kweli sisi tulikuwa tukingali wanyonge, lakini papo hapo, palipotimia, Kristo alikufa kwa ajili yetu sisi tusiomcha Mungu.
7Kwa watu mtu hushindwa kuuawa kwa ajili ya mwongofu; labda atapatikana anayejipa moyo wa kufa kwa ajili yake yeye aliye mwema.
8Lakini jinsi ulivyo upendo wake Mungu wa kutupenda sisi, vimetokea waziwazi hapo, Kristo alipokufa kwa ajili yetu sisi, tukingali wakosaji.[#Yoh. 3:16; 1 Yoh. 4:10.]
9Sasa je? Kwa hivyo, damu yake ilivyotupatia wongofu, hatutazidi kuokolewa naye, makali yasitupate kamwe?[#Rom. 1:18; 2:5,8.]
10Hapo, tulipokuwa tunamchukia Mungu, Mwanawe akawa kole, akatukomboa kwa kufa kwake; sasa je? Kwa hivyo, tulivyokwisha kukombolewa, hatutaokolewa po pote kwa nguvu ya uzima wake?[#Rom. 8:7.]
11Lakini si hili tu, tunalojivunia, ila twajivunia hata Mungu kwa ajili ya Bwana wetu Yesu Kristo, kwa sababu hata sasa tunapata makombozi kwake.*
12Kwani ni hivi: Makosa yaliingizwa ulimwenguni na mtu mmoja, kisha kufa kuliingizwa na makosa, nako kufa kumewafikia watu wote, kwa maana walikosa wote.[#Rom. 6:23; 1 Mose 2:17; 3:19; Ebr. 2:15.]
13Hapo, Maonyo yalipotokea, makosa yalikuwamo ulimwenguni; lakini makosa hayahesabiwi pasipo Maonyo.[#Rom. 4:15.]
14Lakini tangu Adamu mpaka Mose kifo kilishika ufalme hata kwao wale wasiokosa, kama Adamu alivyokosa kwa kubeza agizo. Naye ni mfano wake yeye aliyetazamiwa, atokee siku za halafu.[#1 Kor. 15:21-22,45,55.]
15Lakini kuanguka kulivyo, sivyo nako kugawiwa mema kulivyo. Maana wengi walikufa kwa ajili ya anguko la yule mmoja; lakini magawio ya Mungu tumegawiwa bure, ni kipaji cha yule mtu mmoja Yesu Kristo, kikawafurikia wengi.
16Tena nguvu ya kipaji hiki na nguvu ya yule mkosaji mmoja hazifanani: maana kuhukumiwa kwa mmoja kuliwaletea wote maangamizo; lakini hilo gawio linaondoa maanguko mengi, likigawia wongofu.
17Kwani anguko la mmoja ndilo lililokipatia kifo ufalme, kikaushika kwa ajili yake yeye mmoja; lakini wao waliogawiwa mafuriko ya hicho kipaji kikubwa cha kupewa wongofu bure tu watashika ufalme uzimani kuupita ule kwa ajili yake yeye mmoja Yesu Kristo.
18Basi, ni hivi: Anguko la mmoja liliwapatia watu wote maangamizo, vivyo hivyo wongofu wa mmoja uliwapatia watu wote wongofu unaowapa uzima.[#1 Kor. 15:22.]
19Kwani kama wengi walivyotokezwa kuwa wakosaji kwa ajili ya ukatavu wa mtu mmoja, vivyo hivyo wengi wanatokezwa kuwa wenye wongofu kwa ajili ya usikivu wake yule mmoja.[#Yes. 53:11.]
20Lakini Maonyo yaliingia hapo kati, maanguko yaongezeke. Lakini makosa yalipokuwa mengi, ndipo, magawio yalipofurika.[#Rom. 4:15; 7:8; Gal. 3:19.]
21Kama makosa yalivyoshika ufalme wa kuua watu, vivyo hivyo nayo magawio sharti yashike ufalme wa kuwapa watu uzima wa kale na kale kwa nguvu ya wongofu, aliotupatia Bwana wetu Yesu Kristo.[#Rom. 6:23.]