Waroma 7

Waroma 7

Nguvu ya Maonyo.

1Na niseme nanyi, kwa kuwa mnayatambua Maonyo: Hamjui, ndugu: Maonyo humshika mtu siku zote za maisha yake?

2Kwani mwanamke aliye na mume siku za kuishi kwake mumewe ana mwiko kwa ajili ya Maonyo; lakini nguvu ya hayo Maonyo hukoma, mumewe anapokufa, hana mwiko tena wa mwanamume mwingine.

3Siku za kuishi kwake mumewe, yeye akiwa wa mume mwingine, huitwa mzinzi. Lakini mumewe anapokufa, amefunguliwa na Maonyo, asiwe tena mzinzi akiwa wa mume mwingine.

4Ndugu zangu, hapo Kristo alipokufa, mliuawa nanyi, mkayafia Maonyo; kwa hiyo mmefunguliwa nanyi kuwa wa mwingine, maana ni wa yule aliyefufuliwa katika wafu, kusudi tumzalie Mungu matunda.[#Kol. 2:14.]

5Kwani hapo, mwenendo wetu ulipokuwa wa kimtu, tamaa mbaya zikatuumiza sana, nazo nguvu zao zikaongezeka tu katika viungo vyetu kwa kukatazwa na Maonyo, tukakizalia kifo matunda.[#Rom. 6:21; 7:7-25.]

6Lakini sasa tumefunguliwa, hiyo nguvu ya Maonyo isitushike, tukamfia yule aliyetupinga; hivyo ndivyo, utumikizi wetu ulivyopata kuwa mpya wa kiroho, wa kale uliokuwa wa utumwa wa maandiko ukome.[#Rom. 8:1-2; 6:2,4.]

7*Sasa tusemeje? Maonyo hukosesha? La, sivyo! Lakini kosa singelitambua pasipo Maonyo. Kwani hata tamaa singeijua, kama Maonyo yasingesema: Usitamani![#2 Mose 20:17; Yak. 1:14.]

8Lakini ukosaji ulianzia hapohapo penye agizo hilo, ukakuza moyoni tamaa yo yote, ukaitia nguvu; kwani pasipo Maonyo ukosaji ni mfu.[#Rom. 5:13; 7:11.]

9Nami kale nilikuwa ninaishi pasipo Maonyo; lakini agizo lilipokuja, ukosaji ukafufuka,

10nami nikafa; hivyo agizo lililotokea, linipe uzima, likaonekana, ya kuwa ni lilo hilo lililoniua.[#3 Mose 18:5; Yak. 1:15.]

11Kwani ukosaji ulianzia hapohapo penye agizo hilo, ukanidanganya, ukaniua kwa hilo agizo.[#1 Mose 3:3-12; Ebr. 3:13.]

12Kwa hiyo Maonyo ni matakatifu, nalo agizo ni takatifu lenye wongofu na wema.[#1 Tim. 1:8.]

Utumwa wa ukosaji.

13Basi, inakuwaje? Lililo jema ndio lililoniua mimi? La, sivyo! Ila ukosaji ndio ulioniua; lakini kusudi uonekane kuwa ukosaji, ukaniua kwa lile lililo jema; kwa hivyo, ukosaji ulivyolitumia lile agizo, ukatokea wazi kuwa ukosaji wenyewe usiozuilika kabisa.[#Rom. 5:20.]

14Kwani Maonyo tunayajua, ya kuwa ni ya Kiroho; lakini mimi ni wa kimtu, nikauzwa kuwa mtumwa wa ukosaji.[#Rom. 7:18; Yoh. 3:6.]

15Kwani siyatambui, ninayoyatenda: kwani ninachokitaka sikifanyi, ila ninachokichukia, ndicho, ninachokifanya.

16Nami nisichokitaka, ninapokifanya hichohicho, basi, ninayaitikia Maonyo kuwa mazuri.*[#Rom. 7:12.]

17Sasa si mimi ninayekifanyiza hicho, ila ndio ukosaji unaonikalia moyoni.

18Kwani najua: Humu ndani yangu, maana mwilini mwangu, hamna chema cho chote; kama ni kutaka, ninako, lakini kama ni kukifanya kilicho kizuri, sinako.[#1 Mose 6:5; 8:21.]

19Kwani kilicho chema, ninachokitaka, sikifanyi; ila kilicho kiovu, nisichokitaka, ndicho, ninachokifanyiza.

20Lakini mimi nisichokitaka, ninapokifanya hichohicho, basi, si mimi tena ninayekifanya, ila ndio ukosaji unaonikalia moyoni.

21Hivyo mimi ninayetaka kukifanya kilicho kizuri, ninaona nguvu ngeni kwangu inayonishurutisha kukifanya kilicho kiovu.

22Kwani ninayaitikia Maonyo yake Mungu na kuyashangilia huku ndani moyoni.

23Lakini naona, yamo maonyo mengine viungoni mwangu yanayoyagombeza Maonyo yaliyomo rohoni mwangu, yakaniteka kuwa mtumwa wa maonyo yanayonikosesha, ndiyo yale yaliyomo viungoni mwangu.[#Gal. 5:17.]

24Yamenipata mimi mtu mkiwa! Yuko nani atakayenikomboa utumwani mwa mwili huu wa kufa?

25Mungu atolewe shukrani kwa ajili ya Bwana wetu Yesu Kristo! Basi, kwa akili zangu mimi mwenyewe nayatumikia kitumwa Maonyo yake Mungu, lakini mwilini ni mtumwa wa maonyo ya ukosaji.[#1 Kor. 15:57.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania