Zakaria 5

Zakaria 5

Barua irukayo angani.

1Nilipoyainua macho yangu tena, nichungulie, mara nikaona barua irukayo angani.

2Akaniuliza: Unaona nini? Nikasema: Mimi ninaona barua irukayo angani, urefu wake ni mikono ishirini, nao upana wake ni mikono kumi.

3Akaniambia: Hii ndio kiapizo kilichotika kuifikia nchi yote nzima, kwani kila mwizi ataondolewa huku, kama yalivyoandikwa upande wake mmoja, hata kila aapaye kiapo cha uwongo ataondolewa huku, kama yalivyoandikwa upande wake wa pili.

4Ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi: Nimeitoa, ije kuingia nyumbani mwa mwizi namo nyumbani mwake aapaye kiapo cha uwongo na kulitaja Jina langu, nayo itatua katikati ya nyumbani mwake, hata iiangamize yote pamoja na miti yake na mawe yake.

Mwanamke ndani ya pishi kubwa.

5Kisha malaika aliyesema na mimi akatoka, akaniambia: Yainue macho yako, uone, kama ndio nini litakalotokea.

6Nikauliza: Ndio nini? Akasema: Hili ndio pishi kubwa sana linalotokea. Tena akasema: Hili ndio mfano wa watu walioko katika nchi hii yote nzima.[#Mika 6:10.]

7Mara nikaona, kifuniko cha risasi kilivyonyanyuliwa, akaonekana mwanamke mmoja aliyekaa ndani ya hilo pishi kubwa, kisha akatupa jiwe la risasi juu ya domo lake.

8Yule akasema: Huyu ndio uovu; naye akamtupa ndani ya hilo pishi kubwa, kisha akatupa jiwe la risasi juu ya domo lake.

9Nikayainua macho yangu, nikachungulia mara nikaona, wanawake wawili wakitokea, upepo ukaingia katika mabawa yao, kwani walikuwa na mabawa kama ya korongo, wakalichukua lile pishi kwenda nalo katikati ya nchi na ya mbingu.

10Nikamwuliza malaika aliyesema na mimi: Hili pishi kubwa hawa wanalipeleka wapi?

11Akaniambia: Wanakwenda kulijengea nyumba katika nchi ya Sinari; itakapokuwa tayari, yeye mwanamke atawekwa mle ndani mahali pake, alipotengenezewa.[#1 Mose 11:2.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania