Zakaria 6

Zakaria 6

Magari manne.

1Nilipoyainua macho yangu tena, nichungulie, mara nikaona magari manne yaliyotoka katikati ya milima miwili, nayo milima hiyo ilikuwa ya shaba.[#Zak. 1:8; Ufu. 6:2-8.]

2Gari la kwanza lilikuwa na farasi wekundu, gari la pili lilikuwa na farasi weusi,

3gari la tatu lilikuwa na farasi weupe, gari la nne lilikuwa na farasi wenye nguvu, miili yao ilikuwa ya madoadoa.

4Nikaanza kusema na kumwuliza malaika aliyesema na mimi: Hao maana yao nini, Bwana wangu?

5Malaika akajibu, akaniambia: Hawa ndio pepo nne za mbinguni zinazotaka kutoka sasa kwa kuwa zimekwisha kusimama kwake Bwana wa nchi hii yote nzima.[#Zak. 4:14.]

6Gari lenye farasi weusi linatoka kwenda katika nchi ya kaskazini, nao weupe wanalifuata. Wale wenye miili ya madoadoa wanatoka kwenda katika nchi ya kusini.

7Nao wenye nguvu wanatoka kujitafutia mahali pa kwendea, wapate kutembea katika nchi. Alipowaambia: Haya! Nendeni katika nchi! ndipo, walipokwenda kutembea katika nchi.[#Zak. 1:10.]

8Kisha akapaza sauti na kuniita, akaniambia kwamba: Tazama, hawa wanaotoka kwenda katika nchi ya kaskazini wataituliza roho yangu katika nchi ya kaskazini.

Kiagio cha Masiya.

9Neno la Bwana likanijia la kwamba:

10Watoze tunzo waliotekwa na kuhamishwa, akina Heldai na Tobia na Yedaya, ukija wewe mwenyewe siku hiyo kuingia nyumbani mwa Yosia, mwana wa Sefania, walimofikia walipotoka Babeli!

11Tunzo utakalowatoza ni fedha na dhahabu; kisha fanya taji, kamvike mtambikaji mkuu Yosua, mwana wa Yosadaki, kichwani!

12Umwambie kwamba: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema kwamba: Tazama, yuko mtu atakayekuja, jina lake Chipukizi, maana atachipukia mahali pake; ndiye atakayelijenga Jumba la Bwana.[#Zak. 3:8.]

13Kweli yeye ndiye atakayelijenga Jumba la Bwana na kujipatia utukufu; atakaa katika kiti chake cha kifalme na kutawala, tena atakuwa mtambikaji katika kiti chake cha kifalme, nalo shauri, hao wawili watakalolipiga, litakuwa la mapatano.[#Sh. 110:4.]

14Nazo hizo taji na zikae katika Jumba la Bwana kuwa ukumbusho wa Helemu na wa Tobia na wa Yedaya na wa Heni, mwana wa Sefania.

15Nao walioko mbali watakuja kusaidia kulijenga Jumba la Bwana. Ndipo, mtakapojua, ya kuwa Bwana Mwenye vikosi amenituma kwenu. Haya yatatimia, mkiisikia sauti ya Bwana Mungu wenu na kuitii.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania