Zakaria 7

Zakaria 7

Mungu hataki, watu wafunge mifungo, ila wahurumiane.

1Katika mwaka wa nne wa mfalme Dario ndipo, neno la Bwana lilipomjia Zakaria siku ya nne ya mwezi wa Kisilewu ulio wa tisa.

2Kwani watu wa Beteli walimtuma Sareseri na Regemu-Meleki na watu wao kuja kumnyenyekea Bwana

3na kuwauliza watambikaji waliomo Nyumbani mwa Bwana Mwenye vikosi na kuwauliza nao wafumbuaji kwamba: Tuomboleze katika mwezi wa tano na kujinyima menginemengine, kama tulivyofanya hii miaka yote iliyopita?[#Zak. 8:19; Yer. 52:12.]

4*Ndipo, neno la Bwana Mwenye vikosi liliponijia la kwamba:

5Waambie watu wote wa nchi hii nao watambikaji kwamba: Kama mmefunga na kuomboleza katika mwezi wa tano na wa saba hii miaka 70, je? Mmefunga kwa ajili yangu mimi?[#Zak. 8:19; Yes. 58:5.]

6Tena kama mnakula au kama mnakunywa, Je? Sio ninyi wenyewe mnaokula, tena mnaokunywa?

7Yafaayo siyo yale maneno, Bwana aliyoyatangaza vinywani mwa wafumbuji wa kwanza, Yerusalemu ulipokuwa umekaa watu na kutulia vema, navyo vijiji vyake vilipouzunguka, nayo nchi ya kusini ilipokaa watu, hata nchi ya pwani?

8Neno la Bwana likamjia Zakaria la kwamba:

9Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema kwamba: Kateni mashauri ya kweli yaliyo sawa, mhurumiane kila mtu na ndugu yake kwa kuoneana machungu![#Mika 6:8.]

10Wajane nao waliofiwa na wazazi, nao wageni na wanyonge msiwakorofishe, wala mtu na ndugu yake msiwaziane mabaya mioyoni mwenu!*[#2 Mose 22:21-22.]

11Lakini walikataa kuyasikia hayo, wakawatolea kosi zao ngumu, wakayaziba masikio yao, wasisikie.

12Wakaishupaza mioyo yao, iwe migumu kama almasi, wasiyasikie Maonyo wala maneno, Bwana Mwenye vikosi aliyoyatuma kwao kwa Roho yake na kuwatumia wafumbuaji wa kwanza. Ndipo, makali mengi yalipowajia toka kwa Bwana Mwenye vikosi.[#Yes. 48:4.]

13Ikawa hivyo: kama wao walivyokataa kusikia, alipowaita, ndivyo, nami nilivyokataa kuwasikia, waliponiita; ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema.

14Kwa hiyo nimewatawanya kwa nguvu kama za upepo mkali katika wamizimu wote, wasiowajua, nchi nayo ikageuka nyuma yao kuwa mapori tu, asipatikane mtu aliyeipita wala kwa kwenda wala kwa kurudi. Hivyo ndivyo, walivyoigeuza nchi hii nzuri mno kuwa mapori matupu.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania