The chat will start when you send the first message.
1Yataupata huo mji usiotii, uliojichafua kwa makorofi yake!
2Haukusikia ulipoambiwa neno, ukakataa kuonyeka,
haukumtegemea Bwana, ukakataa kumkaribia Mungu wake.
3Wakuu wake waliomo mwake ni simba wangurumao,
waamuzi wake ni mbwa wa mwitu wakila jioni hawaweki ya asubuhi.
4Wafumbuaji wake hujikuza kwa maneno, ni watu wasiotegemeka;
watambikaji wake hupachafua Patakatifu, tena huyapotoa Maonyo.
5Lakini Bwana ni mwongofu, yuko katikati yao, hafanyi upotovu;
kila kunapokucha hutokeza mwangani mashauri yake yaliyo sawa,
lakini mpotovu hataki kuyajua yamtiayo soni.
6Nimetowesha mataifa, maboma yao yenye minara yako peke yao tu;
nazo barabara za kwao nimezigeuza kuwa za bure,
kwani hakuna mtu tena apitaye hapo,
miji yao imebomolewa, hakuna watu wakaao humo hata mmoja.
7Nalisema: Sasa utaniogopa, uonyeke,
makao yasitoweshwe, yasitimizwe yote,
niliyoyataka kuwapatilizia;
lakini wao walijihimiza sana
kufanya maovu katika matendo yao yote.
8Ndivyo, asemavyo Bwana: Kwa hiyo ningojeni, hata siku ifike, nitakapoondokea kuteka mateka! Kwani shauri langu ni kukusanya mataifa na kuwapeleka mahali pamoja wenye nchi za kifalme, niwamwagie machafuko yangu na makali yangu yote yaliyo yenye moto, kwani ndipo, nchi hii yote nzima itakapoteketezwa kwa moto wa wivu wangu.[#Yoe. 3:2; Sh. 79:6.]
9Kwani hapo ndipo, nitakapoigeuza midomo ya makabila ya watu, iwe imetakata, wao wote pia walitambikie Jina la Bwana na kumtumikia kwa kuwa kundi moja.
10Toka ng'ambo ya pili ya mito ya Nubi watawaleta waninyenyekeao, wawe kipaji cha kunipa, ndio wana wangu waliotawanyika.[#Sh. 68:32; Tume. 8:27.]
11Siku hiyo hutapatwa na soni kwa ajili ya matendo yako yote, uliyonikosea, kwani hapo ndipo, nitakapowaondoa katikati yako walioyafurahia majivuno yako, usiendelee tena kujikuza mlimani penye Patakatifu pangu.
12Nitasaza mwako watu walio wanyonge na wanyenyekevu watakaolijetea Jina la Bwana.[#Ez. 6:8.]
13Masao ya Isiraeli hawatafanya upotovu, wala hawatasema uwongo, wala vinywani mwao hamtaonekana ndimi zenye udanganyifu, kwani wao watajilisha wenyewe, kisha watalala na kupumzika, pasipo kuona atakayewastusha.
14Piga vigelegele, binti Sioni! Shangilieni, ninyi Waisiraeli!
Nawe binti Yerusalemu, furahiwa kwa moyo wote!
15Bwana ameyatangua mashauri, uliyokatiwa, akamwondoa adui yako!
Mfalme wa Isiraeli ni Bwana alioko katikati yako,
hutaogopa mabaya tena.
16Siku hiyo Yerusalemu utaambiwa: Usiogope!
Nawe Sioni utaambiwa: Mikono yako isilegee tena!
17Bwana Mungu wako yuko katikati yako,
naye ni Mungu ajuaye kuokoa.
Atakufurahia na kukufurahisha, atatulia kwa kukupenda,
atakushangilia na kukuimbia.
18Wenye masikitiko wasioingia mikutano ya sikukuu nitawakusanya, kwani nao ni wa kwako, ingawa wawe wametwikwa yawatiayo soni.
19Mtaniona, siku hizo nikiwapatia mambo wote wanaokutesa, niwaokoe wachechemeao, niwakusanye nao waliofukuzwa, watukuzwe, nikiwapatia jina kuu katika hizo nchi zote, walikotiwa soni.[#Mika 4:7.]
20Siku hizo ndipo, nitakapowapeleka kwenu ni siku hizo, nitakapokwisha kuwakusanya, kwani nitawapatia ninyi jina kuu, mtukuzwe kwa makabila yote ya nchi hii, nitakapoyafungua mafungo yenu machoni pao. Bwana ndiye anayeyasema![#Yer. 29:14; Sef. 2:7.]