The chat will start when you send the first message.
1Petro, mtume wa Yesu Kristo, kwa wateule wa Utawanyiko, wakaao hali ya ugeni katika Ponto, na Galatia, na Kapadokia, na Asia, na Bithinia;[#Yak 1:1]
2kama vile Mungu Baba alivyotangulia kuwajua katika kutakaswa na Roho, hata mkapata kutii na kunyunyiziwa damu ya Yesu Kristo. Neema na amani na ziongezwe kwenu.[#Rum 8:29; Ebr 12:24]
3Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu;[#Yak 1:18]
4tupate na urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu.[#Kol 1:12]
5Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani ili mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho.[#Yn 10:28; 17:11; Rum 5:3,4; Gal 3:23; 1 Kor 2:5]
6Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa muda mfupi, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali;[#1 Pet 5:10; Ebr 12:11; Yak 1:2; 2 Kor 4:17]
7ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo.[#Mit 17:3; Mal 3:3; Rum 2:7,10; Yak 1:3]
8Naye mwampenda, ijapokuwa hamkumwona; ambaye ijapokuwa hamumwoni sasa, mnamwamini; na kufurahi sana, kwa furaha isiyoneneka, yenye utukufu,[#Yn 17:20; 20:29; 2 Kor 5:7; 2 Tim 4:8]
9katika kuupokea mwisho wa imani yenu, yaani, wokovu wa roho zenu.[#Rum 6:22]
10Kuhusu wokovu huo, manabii ambao walitabiri habari za neema itakayowafikia ninyi, walichunguza sana.[#Mt 13:17; Lk 10:24]
11Wakatafuta ni wakati upi, na wakati wa namna gani ulioonywa na Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao, ambaye alitangulia kuyashuhudia mateso yatakayompata Kristo, na utukufu utakaokuwako baada ya hayo.[#Zab 22:1; Isa 52:13—53:12; Lk 24:26]
12Wakafunuliwa ya kuwa si kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yenu walihudumu katika mambo hayo, ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiria ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Mambo hayo malaika wanatamani kuyaona.[#Efe 3:10; Lk 2:13]
13Kwa hiyo iweni tayari, na makini; mkiitumainia kwa utimilifu ile neema mtakayoletewa katika ufunuo wake Yesu Kristo.[#Lk 12:35; Efe 6:14; #1:13 Kigiriki ni ‘Vifungeni viuno vya nia zenu na kuwa na kiasi’.]
14Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu;[#Rum 12:2; Efe 2:3; 4:17]
15bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;
16kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.[#Law 11:44-45; 19:2; 20:7]
17Na ikiwa mnamwita Baba, yeye ahukumuye kila mtu pasipo upendeleo, kwa kadiri ya kazi yake, nendeni kwa hofu katika wakati wenu wa kukaa hapa kama wageni.[#Zab 89:26; Yer 3:19; Mal 1:6; Mt 6:9; Rum 2:11]
18Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu;[#Isa 52:3; 1 Kor 6:20; 7:23]
19bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na dosari wala waa, yaani, ya Kristo.[#Isa 53:7; Ebr 9:14]
20Naye amejulikana kweli tangu zamani, kabla haijawekwa misingi ya dunia; lakini alifunuliwa siku hizi za mwisho kwa ajili yenu;[#Rum 16:25; Efe 1:4]
21na kupitia kwake mmekuwa wenye kumwamini Mungu, aliyemfufua katika wafu akampa utukufu; hata imani yenu na tumaini lenu liwe kwa Mungu.[#Yn 14:6; Rum 4:24; Kol 1:27]
22Mkiisha kujitakasa roho zenu kwa kuitii kweli, hata kuufikia upendano wa ndugu usio na unafiki, basi jitahidini kupendana kwa moyo safi.[#1 Yoh 5:1]
23Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la Mungu lenye uzima, linalodumu hata milele.[#Dan 6:26; Yn 1:13; Yak 1:18]
24Maana,[#Isa 40:6-8; Yak 1:10,11]
Mwili wote ni kama majani,
Na fahari yake yote ni kama ua la majani.
Majani hukauka na ua lake huanguka;
25Bali Neno la Bwana hudumu hata milele.[#Isa 40:8]
Na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu.